Na Augusta Njoji, Dodoma
MAKAMU wa Rais wa Jamhuri wa
Muungano, Mhe. Dk. Mohammed Gharib Bilal, amewataka viongozi wa dini kuwakemea
wanasiasa na watu wanaotaka kuingia madarakani kwa manufaa ya binafsi kupitia
migongo ya wanyonge.
Dk. Bilal alitoa kauli hiyo
jana katika sherehe za kumuapisha Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki jimbo kuu la Dodoma, Mhashamu Askofu Beatus Kinyaiya.
"Ni vyema tukakumbuka
kigezo kikubwa cha kiongozi bora ni yule mwenye hofu ya Mungu na anaewajali
watu anaowaongoza bila ubaguzi wowote,"alisema.
Alisema mwaka huu ni wa
uchaguzi na chaguzi zimekuwa zikiibua hisia tofauti miongoni mwa wananchi,
hivyo aliwaomba viongozi wa dini zote
nchini kuliombea taifa katika kipindi hiki ili wananchi waweze
kufanya uamuzi sahihi.
"Uamuzi huu utawafanya
kuchagua watu ambao wataliongoza taifa kwa kuendeleza misingi ya amani, umoja, upendo
na mshikamano,"alisema.
Aliwahakikishia wananchi kuwa serikali
imejipanga vilivyo kuhakikisha inasimamia zoezi lote la uchaguzi kwa misingi
ya haki, amani na utulivu.
"Tunaamini zoezi hilo
litafanyika kwa amani na utulivu mkubwa na mwisho wa siku Watanzania watapata viongozi wazuri,
wanaowataka ili washirikiane nao kusukuma mbele gurudumu la maendeleo yetu,”alisema.
Aliwataka Watanzania kudumisha amani,umoja, upendo na mshikamano.
“Mungu ameibariki sana nchi
yetu, tumeishi kwa muda mrefu kama taifa moja lenye amani na mshikamano mkubwa bila kujali
tofauti za rangi, kabila, dini wala hali
za watu, amani ni sharti la kwanza katika maendeleo ya binadamu.Kuna baadhi ya watu wanadhani
wanapozungumzia kulinda amani ya nchi ni
hila za siasa tu, hao wamepotoka wapuuzwe na kuwaombea kama alivyosema Yesu Kristu pale
msalabani,"alisema.
Kwa upande wake Askofu Mkuu wa kwanza
wa jimbo hilo,Kinyaiya, aliwataka wazazi
kutimiza wajibu wao katika kusimamia maadili ya watoto hao ili kupunguza mmonyoko wa maadili.
No comments:
Post a Comment