Na Mwantanga Ame
Katibu Mkuu wa Chama cha
Mapinduzi,Abdulrahman Kinana, amewataka viongozi wa upinzani waliomo ndani ya
serikali kuiendesha serikali kwa kuwapatia maendeleo wananchi na sio kuonesha
ubabe, vurugu za kusukumiana maneno.
Kinana, aliyasema hayo katika
uwanja wa Gereji, wakati akiwahutubia wananchi walioshiriki mkutano wa hadhara,
wilaya ya magharibi Unguja.
Alisema wanaCCM, wana kila
sababu ya kujiandaa kuyarejesha majimbo yalio mikononi mwa wapinzani, kwa kile
kinachoonekana baadhi ya viongozi wameshindwa kuwajibika vyema, na kutumia
nafasi zao kuwajengea hasama wananchi.
Alisema hivi sasa, baadhi ya
shughuli za serikali katika wizara zimedorora, kiasi ambacho hakuna sababu ya
kuogopa kuyarudisha majimbo hayo ndani ya mikono ya CCM.
Alisema CCM kina ilani yake,
ambayo inalazimika kutekelezwa na viongozi walio madarakani, lakini
kinachoonekana bado kuna waliopewa dhamana hawataki kutimiza hilo kwa kudai
kuwa wanasubiri serikali yao iingie madarakani.
Alisema huo sio uwajibikaji
uliokuwa unatakiwa utekelezwe katika serikali ya umoja wa kitaifa, kwa vile
utaratibu unawataka walio madarakani kushirikiana kuwaletea maendeleo wanachi.
Alisema maendeleo ya Zanzibar
hayapaswi kuletwa kwa maneno, wakati kuna watu walieleza kuwa wana uwezo wa
kuwapatia maendeleo na kuwaahidi vijana kuwapa ajira, lakini kwa kutangaza
masharti hadi washike serikali, jambo ambalo haliwatendei haki.
“Sisi tukiamka tunafikiria nini
tuwafanyie wananchi, wao wanafikiria kuwaambia maneno ya kudai
wananyanyaswa,wakiondoka wanasindikizwa na ving’ora nataka kuwaambia waliopewa
dhamana ndani ya serikali ya umoja wa kitaifa onyesheni mfano,” alisema.
Aidha, Kinana, aliwataka
wanaCCM kujiandaa kushiriki katika kura ya maoni pamoja na kujiandaa na
uchaguzi mkuu ujao.
Hata hivyo,aliwaonya viongozi
wa chama hicho kutochangia kuuharibu uchaguzi mkuu ujao, kwani chama
hakitawavumilia.
Naibu Katibu Mkuu wa UVCCM
Zanzibar, Shaka Hamdu, , alisema ipo haja ya Msajili wa Vyama vya Siasa
Tanzania, kuvionya vyama vinavyokiuka taratibu kwa kutumia bendera na nyimbo
ambazo vyama vyake vilishafutwa.
Naye Balozi Ali Karume, ambaye
ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa, alisema ipo haja ya kuangaliwa upya
mfumo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa baada ya kumalizika kwa uchaguzi mkuu.
Nae Mjumbe wa Kamati Kuu,
Shamsi Vuai Nahodha, alisema CCM hakina sababu ya kutounga mkono kura ya maoni
kwa vile kutofanya hivyo ni kuvunja Muungano.
Mapema Kinana alifanya ziara
katika miradi mbali mbali ya chama kwa kufungua na kuweka mawe ya msingi katika
maskani za chama na kuahidi kuzisaidia mabati pamoja na mifuko ya saraju.
No comments:
Post a Comment