Habari za Punde

Wanachama EAC kutumia mtandao mmoja wa simu

Na Joseph Ngilisho,Arusha
Uamuzi wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kutumia mtandao mmoja wa  simu za mkononi ifikapo  Julai  2015, utasaidia kurahisisha huduma za  mawasiliano katika nchi hizo.

Hayo yalisemwa mwishoni mwa wiki na Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya hiyo, Dk. Enock Bukuku,  wakati akizindua mfumo wa malipo kwa nchi za EAC kwa kutumia kadi ya  Umoja  iliyofanyika mjini hapa.

Alisema   hivi sasa wamekuwa wakitumia mitandao tofauti ya  simu  kwa kila nchi ambapo  mchakato wa kuwepo mtandao  mmoja wa simu kwa nchi hizo utarahisisha huduma za mawasiliano.

 Aliongeza  pamoja na nchi hizo kutumia mtandao  mmoja wa simu pia  wataweza kutumia kadi za Umoja  kwa kupata huduma za kibenki katika  nchi zote na katika benki ambazo zimeunganishwa na mfumo wa Umoja Switch.


 Alisema   mteja yeyote mwenye kadi ya Umoja ataweza  kupata huduma za kibenki kwa benki yeyote katika nchi za EAC  na  kuepuka usumbufu wa kuwa na kadi nyingi.


Wakati huo huo, Mkurugenzi  Mtendaji wa Mitandao ya Umoja Switch,Danford  Mbilinyi, alisema walianza na mabenki sita yaliyoanza kutumia huduma  hiyo ambapo hadi sasa hivi yamefikia mabenki 27 huku wakianza na ATM za  umoja 30 hadi kufikia 2000 katika nchi za EAC.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.