Habari za Punde

Shamuhuna: Tumieni ujuzi kujiajiri

Na Miza Othman- Maelezo Zanzibar 14/01/2015
 
Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Ali Juma Shamuhuna amewashauri wahitimu wa vyuo vikuu nchini kutumia elimu na ujuzi wanaopata  kujiajiri wenyewe badala ya kusubiri ajira Serikalini.
 
Hayo aliyasema   Chuo Kikuu cha Abdurrahaman Al-Sumaait Memorial  Chukwani  (Sumait University) wakati wa  kuwatunuku shahada   ya uwalimu wanafunzi waliohitimu mafunzo hayo katika  mahafali ya 14 ya chuo hicho.
 
Amesema kumekuwa na upungufu mkumbwa wa ajira  Serikalini, huku wahitimu wakiendelea kuongeza kila mwaka.  hivyo amewataka  kutumia taaluma  yao  kujiajiri wenyewe na kuisaidia jami zao.
 
“Nnawakumbusha  kwamba kuna baadhi ya taaluma soko lake la ajira limepungua, hivyo msikae  kusubiri ajira Serikalini  bali itumieni  elimu na ujuzi wenu ili kujitengezea ajira”, Alisisitiza Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali..
 
Waziri Shamhuna ameupongeza uongozi wa chuo hicho kwa kukipanua na kukipa hadhi zaidi kutoka Chuo cha Elimu na sasa kuwa chuo Kikuu kamili na kupewa jina jipya la Sumait University.
 
Alisema anaamini kazi hiyo haikuwa rahisi  kwa uongozi na wafanyakazi kuitekeleza  bali ni matokeo ya kazi ngumu  na ushirikiano uliokuwepo kwa kipindi cha miaka mitatu ya mageuzi hayo.
 
Katika kukiimarisha Chuo Kikuu cha Sumait Waziri Shamhuna ameshauri  kuongezwa fani za utafiti na masuala ya ushauri ili kukipa hadhi zaidi na kutoa wanafunzi waliobora.
 
Aidha aliutaka uongozi wa Chuo hicho kutafuta njia mbadala za kukiendesha  badala ya  kutegemea  zaidi malipo ya wanafunzi na misaada ya wahisani.
 
Akimkaribisha mgeni rasmi kutunuku shahada kwa wahitimu, Mwenyekiti wa Baraza Kuu la chuo Dkt. Abdulrahman Al-Muhailan  alimpongeza Kaimu Makamu Mkuu wa chuo hicho Professa Hamad Rashid Hikmany na wasaidizi wake kwa kazi kubwa waliofanya katika kukifanyia mageuzi chuo hicho..
 
Aliishukuru Serikali ya Muungano wa Tanzania kupitia Kamisheni ya Vyuo Vikuu  Tanzania (TCU)  kwa  ushauri  na maelekezo mazuri  waliowapa na hatimae kupata usajili katika Kamisheni hiyo.
 
Alisema sera za chuo hicho katika kipibndi cha miaka mitano inayomalizika mwaka 2017 ni kuwekeza miradi ambayo itaingiza mapato na tayari wameanzisha jingo la ofisi itakayokuwa na ehemu ya kutoa huduma kwa wageni  mjini Dar es salaam.
 
Ameongeza kuwa hivi sasa wanaimarisha Idara ya Uchapaji  ya chuo hicho na kuiendesha  kibiashara  ili kuwavutia wateja kutoka taasisi za umma na binafsi.
 
Jumla ya wahitimu 266 walikabidhiwa shahda  zao katika mahafali hiyo na kufikisha idadi ya wahitimu 1704 tokea kuanzishwa mwaka 1998.
 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.