Na Abdulla Ali Maelezo-Zanzibar 28/01/2015
Aliyekuwa Mshauri wa Rais wa Serikali ya
Mapinduzi Zanzibar katika mambo ya Utalii Mhe. Issa Ahmed Othman amefariki
dunia baaada ya kuugua kwa muda mrefu.
Marehemu Issa Ahmed alifariki siku ya
tarehe 25/01/2015 akiwa katika matibabu nchini India na amezikwa jana katika
kijiji cha Kianga nje kidogo ya Mji wa Zanzibar ambapo kifo chake kimeleta
mshtuko, huzuni na masikitiko makubwa kwa Chama Cha Mapinduzi na Serikali ya Mapinduzi
ya Zanzibar.
Marehemu alizaliwa mnamo tarehe 24 Julai,
1951 katika kijiji cha Pandani Wilaya ya Wete, Mkoa wa Kaskazini Pemba na
kupata elimu yake ya msingi katika Skuli ya Pandani Pemba na baadae kupata
elimu ya sekondari Uweleni Pemba na kufaulu kidato cha nne pamoja na masomo ya Qur-aan
aliyoyapata hapohapo kijijini kwao.
Katika jitihada za kupanua elimu yake Marehemu
alijiunga na Chuo cha Uhasibu na kufaulu kuwa mhitimu wa Taaluma ya Uhasibu katika
ngazi ya Stashahada.
Kwa upande wa utumishi Marehemu alishika
nyazifa mbalimbali katika Serikali ya Mapinduzi Zanzibar zikiwemo; Mkaguzi wa Ndani
(1969-1974), Mhasibu Wizara ya Biashara Pemba (1975-1984), Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi
(1985-1995), Naibu Waziri wa Kilimo, Mifugo na Maliasili Zanzibar (1988-1995), Mwenyekiti
wa Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la Bima Zanzibar (1987-2000), Makamo
Mwenyekiti Bodi ya Wakurugenzi Shirika la Bandari (1988-1999), Mwenyekiti wa Kamisheni
ya Utalii Zanzibar (2000-2010), Mshauri wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar
katika mambo ya Utalii 2010 hadi mauti yalipomfika.
Kwa upande wa chama, Marehemu alikuwa
ni Mwanachama wa Afro Shirazi Party (ASP) na baada ya kuungana kwa vyama vya TANU
na ASP mwaka 1977 akawa Mwanachama mwanzilishi wa Chama Cha Mapinduzi.
Katika kuendeleza jitihada zake za
kisiasa na kupata ushirikiano mzuri na wanachama wenzake Marehemu alichaguliwa
kuwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama Cha Mapinduzi nafasi ambayo
ilimjengea umaarufu na kumuwezesha kushika nafasi za juu za Uongozi katika Serikali
ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Chama Cha Mapinduzi na Serikali ya Mapinduzi
ya Zanzibar inatambua mchango mkubwa wa Marehemu Issa Ahmed katika Utumishi na Uongozi
wa Chama hicho katika maisha yake kwa kuwa alikuwa ni Kiongozi mwenye Kuheshimu
watu, Mchapakazi mahiri, Mweledi na aliyekuwa akitegemewa na wengi nchini
Zanzibar na bila ya shaka kifo cha Marehemu kimeacha pengo kubwa katika Chama
Cha Mapinduzi na Taifa kwa ujumla.
Aidha Chama na Serikali vimewataka Viongozi,
Ndugu, Jamaa na Marafiki wa Marehemu kuwa na moyo wa subira katika wakati huu
mgumu wa maombolezo ya mpendwa wao huyo.
Hadi kufariki kwake, Marehemu Issa
Ahmed Othman alikuwa ni mshauri wa Rais katika mambo ya Utalii Zanzibar, na
ameacha Kizuka 1, Watoto 7, na Wajukuu 25.
Mwenyezi Mungu aiweke roho ya Marehemu mahala
pema Peponi.
IMETOLEWA NA HABARI MAELEZO ZANZIBAR
Hee jamani hata picha!....
ReplyDeleteKumbu kumbu zangu ni kwamba zamani sauti ya tzania Zanzibar walikua na kitengo cha kutunza kumbukumbu zikiwemo picha za viongozi mbalimbali sijui imeishia wapi?
Huyu hakua kiongozi
ReplyDelete