Habari za Punde

Wasifu wa Marehemu Issa Ahmed Othman


Na Abdulla Ali Maelezo-Zanzibar                              28/01/2015

Aliyekuwa Mshauri wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar katika mambo ya Utalii Mhe. Issa Ahmed Othman amefariki dunia baaada ya kuugua kwa muda mrefu.

Marehemu Issa Ahmed alifariki siku ya tarehe 25/01/2015 akiwa katika matibabu nchini India na amezikwa jana katika kijiji cha Kianga nje kidogo ya Mji wa Zanzibar ambapo kifo chake kimeleta mshtuko, huzuni na masikitiko makubwa kwa Chama Cha Mapinduzi na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Marehemu alizaliwa mnamo tarehe 24 Julai, 1951 katika kijiji cha Pandani Wilaya ya Wete, Mkoa wa Kaskazini Pemba na kupata elimu yake ya msingi katika Skuli ya Pandani Pemba na baadae kupata elimu ya sekondari Uweleni Pemba na kufaulu kidato cha nne pamoja na masomo ya Qur-aan aliyoyapata hapohapo kijijini kwao.

Katika jitihada za kupanua elimu yake Marehemu alijiunga na Chuo cha Uhasibu na kufaulu kuwa mhitimu wa Taaluma ya Uhasibu katika ngazi ya Stashahada.

Kwa upande wa utumishi Marehemu alishika nyazifa mbalimbali katika Serikali ya Mapinduzi Zanzibar zikiwemo; Mkaguzi wa Ndani (1969-1974), Mhasibu Wizara ya Biashara Pemba (1975-1984), Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi (1985-1995), Naibu Waziri wa Kilimo, Mifugo na Maliasili Zanzibar (1988-1995), Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la Bima Zanzibar (1987-2000), Makamo Mwenyekiti Bodi ya Wakurugenzi Shirika la Bandari (1988-1999), Mwenyekiti wa Kamisheni ya Utalii Zanzibar (2000-2010), Mshauri wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar katika mambo ya Utalii 2010 hadi mauti yalipomfika.


Kwa upande wa chama, Marehemu alikuwa ni Mwanachama wa Afro Shirazi Party (ASP) na baada ya kuungana kwa vyama vya TANU na ASP mwaka 1977 akawa Mwanachama mwanzilishi wa Chama Cha Mapinduzi.

Katika kuendeleza jitihada zake za kisiasa na kupata ushirikiano mzuri na wanachama wenzake Marehemu alichaguliwa kuwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama Cha Mapinduzi nafasi ambayo ilimjengea umaarufu na kumuwezesha kushika nafasi za juu za Uongozi katika Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Chama Cha Mapinduzi na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inatambua mchango mkubwa wa Marehemu Issa Ahmed katika Utumishi na Uongozi wa Chama hicho katika maisha yake kwa kuwa alikuwa ni Kiongozi mwenye Kuheshimu watu, Mchapakazi mahiri, Mweledi na aliyekuwa akitegemewa na wengi nchini Zanzibar na bila ya shaka kifo cha Marehemu kimeacha pengo kubwa katika Chama Cha Mapinduzi na Taifa kwa ujumla.

Aidha Chama na Serikali vimewataka Viongozi, Ndugu, Jamaa na Marafiki wa Marehemu kuwa na moyo wa subira katika wakati huu mgumu wa maombolezo ya mpendwa wao huyo.

Hadi kufariki kwake, Marehemu Issa Ahmed Othman alikuwa ni mshauri wa Rais katika mambo ya Utalii Zanzibar, na ameacha Kizuka 1, Watoto 7, na Wajukuu 25.

Mwenyezi Mungu aiweke roho ya Marehemu mahala pema Peponi.


IMETOLEWA NA HABARI MAELEZO ZANZIBAR

2 comments:

  1. Hee jamani hata picha!....
    Kumbu kumbu zangu ni kwamba zamani sauti ya tzania Zanzibar walikua na kitengo cha kutunza kumbukumbu zikiwemo picha za viongozi mbalimbali sijui imeishia wapi?

    ReplyDelete
  2. Huyu hakua kiongozi

    ReplyDelete

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.