Habari za Punde

Waziri Zainab ataka udhalilishaji ukomeshwe

Na Abdi Suleiman, Pemba
Waziri wa Uwezeshaji, Ustawi wa Jamii, Vijana, Wanawake na Watoto, Mhe. Zainab Mohammed Omar, amewataka wanachama wa Jumuiya ya UVIMAWE wilaya ya Wete, kuendelea kukemea na kuelimisha jamii juu ya athari za vitendo vya udhalilishaji na ubakaji wa watoto.
 
Alisema hayo baada ya kuuzinduwa Umoja wa Vijana na Maendeleo wilaya ya Wete (UVIMAWE), katika hafa iliyofanyika Kipangani wilaya ya Wete.
 
Aliwataka wanawake watokubali vitendo vya udhalilishaji na kupiga vita kwa nguvu zote.
 
Aidha aliwataka wananchi wa Wete kushirikiana katika malezi ya watoto wao, ili kuweza kuwaepusha na vitendo viovu.
 
Waziri huyo aliwahimiza vijana kujituma ili kuweza kuondokana na utegemezi wa ajira kutoka serikalini.

Ofisa Mdhamini wa wizara hiyo, Mauwa Makame Rajab, alisema wizara yake iko bega kwa bega na UVIMAWE,na kuwasifia vijana wa Wete jinsi walivyochangamkia fursa mbali mbali zinazojitokeza.

Naye Mwenyekiti wa UVIMAWE, Rashid Shamata, aliiomba serikali na viongozi kuwasaidia kwa hali na mali ili umoja huo uweze kufikia malengo iliyojiwekea.
Katibu wa UVIMAWE, Maalim Mohamed Saidi, aliwashukuru vijana wenzake wa Wete, kwa juhudi yao ya kuanzisha umoja huo utakaosaidia kupunguza changamoto zinazowakabili.


No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.