Habari za Punde

ZFA wilaya ya mjini yafanya uchaguzi wa viongozi

Na Mwajuma Juma
 
CHAMA Cha Soka Zanzibar (ZFA) Wilaya ya Mjini juzi kilifanya uchaguzi wake wa kuchaguwa viongozi wake huku mwandishi wa habari wa kujitegemea Mwajuma Juma akiibuka kidedea katika uchaguzi huo.
 
Katika uchaguzi huo mwanahabari huyo  alikuwa ni miongoni mwa wagombea wa nafasi ya kamati Tendaji ya ZFA Wilaya ya Mjini ambapo aliibuka kuwa mshindi wa pili kwa kupata kura 56 huku wa kwanza akiwa ni Ali Othman Kibichwa Rais wa timu ya Jang’ombe Boys ambae alipata kura 66, wakati wa tatu ni Hassan Ali Kiske akipata kura 53 na Kijo Nadir Nyoni akipata kura 52.
 
Uchaguzi huo ambao ulifanyika katika ukumbi wa shule ya Bilali Islamic Seminary ulisimamiwa na kamati ya Uchaguzi ya chama hicho chini ya Mwenyekiti wake Asha Mzula.
 
Katika uchaguzi huo ulijumuisha nafasi ya Mwenyekiti, Makamo Mwenyekiti, Katibu, Msaidizi Katibu, Mshika Fedha, mjumbe wa kamati Tendaji ZFA Taifa na wajumbe wanne wa Kamati  Tendaji ZFA Wilaya ya Mjini.
 
Akitangaza matokeo ya uchaguzi huo Katibu wa kamati ya Uchaguzi Nahoda Haji alisema kuwa jumla ya kura zote zilizopigwa ni 106.
 
Nahoda alimtangaza Hassan Haji Hamza ‘Chura’ kuwa Mwenyekiti wa ZFA Wilaya ya Mjini kwa kupata kura 105, wakati nafasi ya Makamo Mwenyekiti nayo ikarudi tena kwa Juma Abdalla aliyepata kura 52 na kuwaangusa wapinzani wake Saidi Khalfan aliyepata kura 32, Ramadhan Pandu kura 15 na  Ali Suleiman Nassor kura sita.
 
Nafasi ya katibu ilirudi tena kwa Yahya Juma Ali ‘Kaduguda’ aliyepata kura 96 na kumshinda mpinzani wake Mbarouk Juma aliepata kura tano, nafasi ya Katibu Msaidizi nayo ilirudi tena kwa Omar Mohammed Omar aliyepata kura 103, huku Mshika fedha ni Ali Abdalla ambae alipata kura 105.
 
Kwa upande wa nafasi ya Mjumbe wa Kamati Tendaji ZFA Taifa kutoka wilaya ya mjini ilichukuwa na Hussein Ali Ahmada  kwa kupata kura 54 ambae aliwaangusha Hashim Salum  aliyepata kura 48 na Maulid Abdalla aliyepata kura nne.
 
Wajumbe hao waliochaguliwa kwa kura juzi wanatarajiwa kukitumikia chama hicho kwa muda wa miaka minne ijayo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.