Wakati Wazanzibari leo wakiadhimisha miaka 51 ya Mapinduzi, wanasiasa na wasomi wametaka wananchi hao kufanya mikakati muhimu ya maendeleo na kuacha fikra mgando zinazoathiri maendeleo yao na nchi yao.
Wasomi na wanasiasa hao amesema Zanzibar imepiga hatua kubwa za maendeleo kiuchumi, kijamii na kisiasa lakini zinaweza kuendelezwa au kuharibiwa na Wazanzibari wenyewe iwapo wataendekeza tofauti zao za kihistoria zinazohusiana na mapinduzi.
Zanzibar inaadhimisha sherehe hizo huku kukiwa na matukio mawili makubwa ya kitaifa yanayoisubiri ikiwamo Kura ya Maoni ya Katiba Mpya na Uchaguzi Mkuu wa Oktoba, ambayo kwa namna moja au nyingine yanatajwa kuwa kipimo kikuu cha mwelekeo wa visiwa hivyo kisiasa.
Maadhimisho hayo yatakayoongozwa na Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein kwenye Uwanja wa Amaan, yatahudhuriwa pia na Rais Jakaya Kikwete na viongozi wengine waandamizi wa Serikali ya Mapinduzi na ile ya Muungano.
Mhadhiri wa Kitivo cha Sheria cha Chuo Kikuu cha Zanzibar, Ali Uki alisema pamoja na kwamba Zanzibar imepiga hatua katika ujenzi wa miundombinu, huduma za kijamii, sheria, kilimo na maendeleo ya kisiasa kudumisha amani ndilo jambo la msingi.
“Suala la maendeleo hayo yamefikiwa kwa kiwango gani? Kila mtu anatazama kwa jicho na mtazamo wake,” alisema Uki na kuongeza kuwa kisiasa kuna mafanikio makubwa.
Alisema tangu kuanza mfumo wa vyama vingi mwaka 1992, Zanzibar imekuwa ikijitahidi kuhimili misukosuko mbalimbali ya kisiasa ukiwamo upinzani mkali baina ya CCM na CUF uliosababisha kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK).
Alisema mbali na mafanikio hayo, kuna haja ya kufanya mkutano wa kitaifa wa kukubaliana kiwango cha sera za kufuatwa kutoka katika kila chama kwani licha ya kuwa na SUK hivi sasa, sera za CCM ndizo zinazofuatwa.
Iwapo itaonekana hili ni tatizo katika mwaka huu wenye changamoto za Kura ya Maoni na Uchaguzi Mkuu, Uki alisema kila chama kinaweza kukaa katika kamati zake na wataalamu na kuamua kuhusu kujumuisha sera zao ili kujenga mustakabali bora wa kisiasa Zanzibar.
“Watu waache fikra mgando kwamba hili ni suala langu na lile ni la yule, wafanye maendeleo kwa ushirikiano kwa kuwa mustakabali wa Zanzibar utatengenezwa na wao wenyewe,” alisema.
Mhadhiri katika Idara ya Sayansi ya Siasa ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Richard Mbunda alisema Mapinduzi ya Zanzibar yana mafanikio makubwa na yameendelea kuwapo bila mapinduzi mengine, jambo linaloonyesha yalikubalika vizuri.
Alisema mapinduzi yalifanikiwa kuendana na misukosuko ya kisiasa ukiwamo mfumo wa vyama vingi vya kisiasa ulioleta uga wa kisiasa usiotabirika wa nani atakuwa mshindi katika uchaguzi mkuu wowote.
Kuhusu mwaka huu wa uchaguzi, Mbunda alisema CUF na CCM vina nguvu sawa, hivyo ni lazima hali hiyo itawagawa Wazanzibari.
Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu alisema mustakabali wa Muungano kati ya Zanzibar na Tanganyika upo mikononi mwa wananchi wote na kwamba Kura ya Maoni ya Katiba inaweza kuamua hatima yake.
“Wananchi wenyewe ndiyo watakaoamua lakini lazima mazingira yote ya upigaji kura yawekwe sawa. Utaratibu wa kampeni uwe sahihi, watu wote wazungumze kwa uhuru, vyombo vya habari vitumike vizuri bila kuunga mkono upande wowote hapo ndipo tutasikia Wazanzibari wanataka Muungano wa aina ipi,” alibainisha Lissu.
Maadhimisho
Katibu Mkuu Wizara ya Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Dk Khalid Mohamed Salum alisema milango ya Uwanja wa Amaan itafunguliwa kuanzia saa 12 asubuhi na viongozi wataanza kuwasili na saa tatu asubuhi.
Viongozi wengine wa kitaifa wanaotarajiwa kuhudhuria sherehe hizo ni Makamu wa Rais, Dk Mohamed Gharib Bilal, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, Makamu wa Kwanza Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad na Makamu wa Pili, Balozi Seif Ali Iddi.
Wengine ni mawaziri wakuu wa zamani Edward Lowassa na Frederick Sumaye, Waziri Kiongozi mstaafu, Shamsi Vuai Nahodha.
Dk Shein atapokea heshima na salamu kutoka kwa askari wa vikosi vya ulinzi na usalama kabla ya kukagua gwaride na kulihutubia Taifa.
Tofauti na miaka ya nyuma, Baraza za CUF pamoja na ofisi zake, zimepambwa katika maeneo mbalimbali kama Michenzani huku vijana wa chama hicho wakishiriki kufanya usafi wa mazingira kwa ajili ya shughuli hiyo.
Dk Shein anatarajiwa kuzungumzia mwelekeo wa uchumi wa Zanzibar, huduma za kijamii, hali ya kisiasa katika kuelekea Kura za Maoni, Uchaguzi Mkuu pamoja na mafanikio ya SUK na changamoto
Taarifa za nyongeza na Mwinyi Sadallah
Chanzo: Mwananchi
wallahi yakhe sisi tunapiga kelele tu mapinduzi mapinduzi tukiulizwa yamekunufaisha nini? tunapwesa tu.
ReplyDelete