Na Amina Omari,Tanga
ASKARI polisi watano
waliojeruhiwa kwenye tukio la kurushiana risasi katika ya polisi na kikundi cha
wahalifu kwenye mapango ya Mleni jijini Tanga, wameruhusiwa kutoka hospitali
baada ya hali zao kuimarika.
Akizungumza na Zanzibar
Leo kwa njia ya simu, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Freisser Kashai, alisema
majeruhi hao waliruhusiwa mapema jana baada ya madktari kuridhishwa na hali
zao.
Akizungumzia hali ya
usalama katika eneo la tukio, alisema eneo hilo kwa sasa hali ni ya usalama
huku vikosi vya polisi vikiendelea na doria za kawaida za kuimarisha amani.
"Kwa sasa hali ni
ya amani tunaendelea na upelelezi wetu wa kuwahoji watuhumiwa tulio wakamata
huku vikosi vya jeshi vikendelea kufanya doria ili kuwabaini watuhumiwa wengine,”
alisema.
Alisema kinachoendelea
kwa sasa ni upelelezi na misako ili kuwakamata watuhumiwa wengine na kuendelea
kuitafuta silaha moja ambayo bado haijapatikana.
Alisema kwa sasa vikundi
vya jeshi ambavyo vilikuwa wanashirikiana navyo kwenye oparesheni vimepungua
kwenye eneo la mapango hayo.
Katika hatua nyingine
Kamanda Kashai alisema ameridhishwa na mafanikio ya oparesheni hiyo
yalivyofanyika na kufanikiwa kuwakamata baadhi ya watuhumiwa pamoja na silaha
moja katika ya mbili zilizoporwa.
"Niwaombe wananchi
wa Tanga waendelee kuwa na imani ya jeshi lao kwani tunafanya kazi usiku na
mchana ili kuhakikisha mkoa huu unakuwa na amani na utulivu,"alibainisha.
Pia aliwataka wananchi
kuwa na subra katika kipindi hiki kwani baada ya upelelezi kukamilika taarifa
kamamili kuhusiana na watuhumiwa wataitoa na kueleza kama ni watu wa namna
gani.
Kwa upande wa wakazi wa Mleni
wamekiri kuwa kwa siku ya jana doria za magari makubwa ya jeshi hazikuwepo
kabisa ila walikuwepo askari wachache kwa ajili ya kuendelea na upelelezi.
No comments:
Post a Comment