Na Mwandishi wetu
TUME ya Haki za Binadamu
na Utawala Bora (THBUB) imesikitishwa na mauaji ya kikatili ya mtoto Yohana
Bahati, aliyetekwa nyara hivi karibuni katika kijiji cha Ilelema, Chato mkoani
Geita.
Pia tume hiyo imelaani
kuumizwa kwa mama yake, Ester Jonas, wakati anatetea uhai wa mwanae wakati wa
tukio lililotokea Februari 15 mwaka huu.
Taarifa iliyosainiwa na
Mwenyekiti wa tume hiyo,Bahame Tom Nyanduga,imesema kwa
ujumla vitendo vya ukatili wanaofanyiwa watu wenye ulemavu wa ngozi, ni matukio
ya ukiukwaji wa sheria na haki za kibinadamu.
Alisema matukio hayo
yanaonesha yamekuwa yakichagiwa na imani za kishirikina hivyo tume inakemea
matendo haya na kutaka yapigwe vita.
Mwenyekiti huyo alisema
chini ya katiba na mikataba ya kimataifa ya haki za binadamu serikali inao
wajibu wa kulinda raia wake hivyo aliiomba serikali kuwatafuta wale wote wanaohusika
na vitendo hivyo na kuwafikisha mbele ya vyombo vya sheria.
Aidha alisema tume
inaungana na wananchi, wadau mbalimbali na serikali kulaani vikali mauaji ya
mtoto Yohana na kujeruhiwa vibaya mama yake wakati akitetea haki ya mwanae
kuishi katika jamii huru.
Aliikumbusha serikali
kuwa wakati umefika wa kufanyia marekebisho makubwa sheria ya uchawi (sura ya
18 ya 1928) au kutunga sheria mpya ili kupiga marufuku vitendo vyote
vinavyoendeleza imani za uchawi na ushirikina.
Alisema tume inatoa wito
kwa wananchi na jamii yote kwa ujumla kuachana na imani potofu zenye mtizamo
hasi kwamba mafanikio yoyote yanaweza kupatikana kwa njia za kishirikina.
“Tume inakumbusha
wananchi kuwa mafanikio yoyote yatapatikana kwa kufanya kazi zote halali kwa
bidii, na siyo kwa njia za kishirikina ikiwemo kutumia viungo vya watu wenye
ulemavu wa ngozi,” alisema.
Wakati huo huo, Kamishna
wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa, Zeid Ra'ad Al Hussein, amekemea mauaji
ya walemavu wa ngozi nchini Tanzania.
No comments:
Post a Comment