STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar
9.2.2015

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi Mhe. Dk. Ali Mohamed Shein amefungua kiwanja kipya na cha kisasa cha
mchezo wa Gofu na kusema kuwa ufunguzi huo unakwenda sambamba na jitihada zinazochukuliwa
na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Awamu ya Saba ya kufufua michezo nchini.
Dk. Shein aliyasema
hayo, katika hotuba yake iliyosomwa kwa niaba yake na Waziri wa Nchi Ofisi ya
Rais na Utawala Bora, Mhe. Dk. Mwinyihaji Makame katika sherehe za ufunguzi wa kiwanja cha
mchezo wa Gofu katika Hoteli ya Sea Cliff, iliyopo Kiombamvua, Wilaya ya
Kaskazini B, Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Katika hotuba
hiyo, Dk. Shein alisema kuwa lengo na jitihada hizo ni kuona kuwa vuguvugu la
michezo linarejea Zanzibar na kuweza kutoa wanamichezo wenye vipaji mbali mbali
wenye uwezo wa kushinda katika mashindano ya Kimataifa.
Alisema kuwa
imani yake ni kuwa uwanja huo wa gofu utapelekea Zanzibar kuwa na wanamichezo
wenye vipaji vya kucheza mcheo huo na kushinda katika michuano ya Kimataifa.
“Bado ni mapema
kufikia kuwa na Tiger Woods kutoka Zanzibar, lakini hakuna sababu ya kuondoa
matumaini kwamba hatuwezi kuwa na mchezaji mahiri katika mchezo huo”, alisema
Dk. Shein.
Aidha, Dk. Shein
alisema kuwa ufunguzi wa kiwanja hicho cha Gofu chenye hadi ya Kimataifa
utachangia sana katika kurejesha sifa na umaarufu wa Zanzibar katika michezo
ukiwemo mchezo wa gofu.
“Nafahamu kwamba
hivi sasa si watu wengi wanaofahamu kuwa Zanzibar ilikuwa ni miongoni mwa nchi
za mwanzo kabisa barani Afrika kuwa na Kiwanja cha Mchezo wa Gofu ambacho kilikuwa
katika eneo la MnaziMmoja, Mivinjeni hadi upande wa uwanja wa Maisara, Mjini
Unguja”,alisema Dk. Shein.
Pamoja na hayo,
Dk. Shein alisema kuwa amefurahi kupata taarifa kuwa wamiliki wa hoteli hiyo
hawaoni kama kiwanja hicho ni mali yao pekee yao bali wanaona kama ni mali ya
Zanzibar na watu wake wote kutokana na kupata hisia kuwa kuzingatia kuwa uzuri
wa kiwanja hicho utatumika katika kuitangaza Zanzibar kiutalii na kimichezo
duniani kote.
Dk. Shein alitoa
nasaha kwa wananchi kuendelea kuwaunga mkono na kuwapa mashirikiano
yanayohitajika wawekezaji wote walioekeza hapa nchini ili nao waendelee kufanya
mambo makubwa yenye manufaa kwa maendeleo ya kila mmoja.
Alisisitiza kuwa
ni dhahiri kuwa ufunguzi wa kiwanja hicho unakwenda sambamba na juhudi
zinazochukuliwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Awamu ya Saba za
kuimarisha Sekta ya Utalii, ambayo ndio sekta kiongozi kwa uchumi wa Zanzibar.
Alisema kuwa
utalii hivi sasa unachangia asilimia 80 ya fedha za kigeni na una mchango wa
asilimia 27 katika pato la Taifa.
Sambamba na hayo,
Dk. Shein aliwasihi wamiliki wa hoteli hiyo waongeze kasi katika kukitangaza
kiwanja hicho na vivutio mbali mbali vya utalii viliopo Zanzibar katika sehemu
mbali mbali za dunia kupitia mitandao, televisheni na vyombo mbali mbali vya
habari.
Kwa mara nyengine
Dk. Shein aliuhimiza uongozi wa Wizara ya Habari, Utamaduni na Utalii na
Michezo pamoja na uongozi wa Kamisheni ya Utalii Zanzibar kuendelea
kushirikiana na wawekezaji wa ndani na nje ya anchi katika kuitangaza Zanzibar.
Dk. Shein
alitumia fursa hiyo kuwahakikishia wawekezaji walioekeza hapa nchini kuwa
Serikali itaendelea kulinda na kuendeleza hali ya amani na utulivu, jambo
ambalo limeipatia sifa kubwa Zanzibar na kuendelea kuwavutia wageni kutoka
pande zote za dunia.
Aidha, alisema
kuwa Serikali ityaendelea kwualinda watalii, wawekezaji pamoja na mali na
rasilimali zao zilizopo nchini.
Katika hotuba
yake hiyo, Dk. Shein alitumia fursa hiyo kutoa pongezi kwa mtengenezaji maarufu
wa viwanja vya Gofu duniani, Bwana Peter Matkvich kutoka Afrika ya Kusini
ambaye ndie aliekitengeza kiwanja hicho.
Mapema Bwana
Peter Matkovich alitoa shukurani na pongezi kwa kupata fursa hiyo na kueleza
kuwaujenzi wa kiwanja hicho utasaidia kwa kiasi kikubwa kuimarisha mchezo huo
unaopendwa duniani na ni miongoni mwa viwanja bora katika ukanda huu wa bara la
Afrika.
Alisema kuwa
uwanja huo una vishimo 18 ambayo ni idadi ya vishimo vinavyokuwemo kwenye
viwanja vinavyotumika kwa mashindano makubwa ya Kimataifa.
Nae Mwenyekiti wa
Kampuni ya ‘Sea Cliff Resort and Spa
Zamzibar’, Bwana Subhash Patel alitoa pongezi kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
pamoja na uongozi wake kwa mashirikiano yao mazuri katika kuhakikisha mafanikio
hayo yanapatikana.
Aidha, Bwana
Patel alisema kuwa hatua hiyo itasaidia kuongeza kasi ya michezo nchini
sambamba na kuinua sekta ya utalii bila ya kusahau soko la ajira na kujenga
urafiki.
Viongozi mbali
mbali walihudhuria katyika hafla hiyo akiwemo Waziri wa Ardhi, Makaazi, Maji na
Nishati, Mhe. Ramadhan Abdalla Shaaban, Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja Mhe.
Meja Mstaafu Juma Kassim Tindwa, viongozi wa serikali, wageni mbali mbali wa
mchezo huo kutoka ndani na nje ya Zanzibar.
Rajab Mkasaba, Ikulu
Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024
2231822
E-mail:
rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment