Na Joseph Ngilisho,Arusha
CHAMA cha Mapinduzi wilaya ya
Arusha, kimesema hakitasita kuchukua hatua kali kwa wanachama wake watakaofanya
kampeni mapema kwa kugawa msaada wowote utakaoashiria kampeni.
Aidha chama hicho kimepiga
marufuku wagombea ‘njaa’ wasio na kipato na kuwataka wajitathimini kabla ya
kuonyesha nia ya kuwania nafasi yoyote.
“CCM haihitaji wagombea
wachovu,kama mgombea hana uwezo hata wa kugharamia kipaza sauti asishiriki, tunataka
mgombea mwenye uwezo na hata kama hana
uwezo basi awe na watu wanaomuunga mkono,” alisema Katibu wa CCM wilaya hiyo,Feruz
Banno.
Alizungumza kwenye maadhimisho
ya siku ya Jumuia ya Wazazi,ambapo pamoja na mambo mengine aliwataka makada
walioonesha nia ya kugombea kiti cha ubunge jimbo la Arusha mjini,kutoshiriki
kampeni zozote kwa sasa.
Alikiri chama kutafunwa na
makundi ya wagombea uchaguzi uliopita ambayo hadi sasa hayajavunjika na usaliti
ndani ya chama,huku akieleza kuwa mabalozi wake wengi wamekuwa wasaliti na wamepandikizi
ndani ya chama hatua ambayo imesababisha CCM kuangushwa.
Alisema hadi sasa jumla ya
makada wake wanane wameonesha nia ya kugombea ubunge katika jimbo la Arusha
mjini,akiwemo kamanda wa UVCCM mkoa, Philemon Mollel.
Katibu wa jumuiya ya wazazi
mkoa wa Arusha, Mayasa Kimbau, alionyesha mashaka ya kuendelea kupoteza jimbo
la Arusha,iwapo wananchama hawatobadilika kwa kuvunja makundi.
Alisema japo makundi ni muhimu
kwa mgombea yoyote lakini ni vyema yakavunjwa baada ya uchaguzi kumalizika.
“Tangu nihamishiwe Arusha wiki
mbili zilizopita kwa kweli nimegundua Arusha kuna makundi makubwa ya tangu
uchaguzi wa mwaka 2010 na msipo yavunja hatutaweza kulichukua jimbo hili na
tutaendelea kupoteza maeneo mengi kwa sababu ya chuki zetu na usaliti,”
alisema.
No comments:
Post a Comment