Na Abdi Shamnah
MAHAKAMA ya wilaya Makunduchi,
imeahirisha tena kesi ya shambulio la
kuumiza mwili, inayomkabili mshitakiwa Ivan Kode (35), raia wa Ufaransa hadi
Februari 12 mwaka huu, ili kupata muda wa kupitia ombi linalobishaniwa na
upande mbili za mahakama.
Mshitakiwa Ivan Kode,
anatuhumiwa kuwashambulia kwa kuwapiga bastola yenye risasi za chubwi, Nadir
Ali Juma, Ashraf Suleiman Yussuf, Wadi Ame Khamis na Ally Ramadhan Mohammed na
kuwasababishia maumivu makali mwilini.
Katika mahakama hiyo iliokuwa
chini ya hakimu Mohammed Ali Haji, Wakili wa
mshitakiwa huyo Elizabeth Lazaro Mayalla, aliiomba mahakama kutoa idhini
ya kukabidhiwa paspoti mteja wake ili aweze kusafiri nje ya nchi kwa matibabu.
Alidai hali ya afya mteja wake ambae hajafika
mahakamani hapo kwa takriban vikao vinne sasa
tangu alipotoka mahabusu na kupewa dhamana, haiko vyema hivyo anahitaji
matibabu ya ziada nje ya nchi.
Wakili huyo
(bila ya kueleza maradhi yanayomsumbua mteja wake), alidai mbali na mshitakiwa kuwepo Zanzibar, ameshindwa kufika
mbele ya mahakama hiyo kutokana na sababu za kiafya.
Mayalla aliwasilisha mahakamani
hapoi ‘board pass’ pamoja na kipande cha tiketi alichotumia mshitakiwa katika
safari yake, kuthibitisha ukweli wa hoja yake na nia aliyokuwanayo kuhudhuria
katika kikao hicho.
Hata hivyo, ombi la Wakili huyo
lilipata upinzani mkubwa kutoka upande wa mashataka, pale Muendesha mashtaka,Mkaguzi
Msaidizi wa Polisi, Abdulkadir Miradj
alipoiomba mahakama kuwa makini na ombi lililowasilishwa kwani huenda kuna
mbinu zimepangwa kumpa fursa mshitakiwa kutoroka.
Aliiomba mahakama kuzingatia
mwenendo wa mshitakiwa mahakamani hapo
ambao alidai unatia mashaka, hivyo kuwepo wasiwasi wa kutoroka na kuwakosesha
watu wengine haki, pale atakakabidhiwa paspoti hiyo.
Alidaini vikao vinne sasa mshitakiwa
hajafika mahakamani kwa kizingizio cha ugonjwa, hali inayotia mashaka juu ya
hatma ya kesi hiyo.
Akitoa ufafanuzi baada ya
kuibuka hoja zinazopingana, Hakimu Mohammed aliwataka wadhamini wa mshitakiwa kuhakikisha
wanamfikisha mahakamani siku iliopangwa.
“Wadhamini wahakikishe siku
hiyo mshitakiwa anafika mahakamani bila ya kukosa na ndipo nitatoa uamuzi juu ya hoja inayobishaniwa ya
kumkabidhi paspoti yake ili aweze kwenda nje kwa matibabu,” alisema.
Aidha alisema mashahidi wa kesi
hiyo nao watawajibika kufika mahakamani kwa ajili ya kutoa ushahidi katika siku
itakayopangwa baada ya kutolewa mamauzi ya hoja ya msingi.
Katika shauri hilo, mshatkiwa
Ivan Kode ameshtakiwa kwa kosa la shambulio la kuumiza mwili, kinyume na
kifungu cha 247 sheria namba 6 ya 2004, sheria za Zanzibar, ikidaiwa aliwashambulia
watu wanne kwa kuwapiga bastola yenye risasi za chubwi na kuwasababishia
maumivu.
No comments:
Post a Comment