Na Faki Mjaka, Mascut Oman 02/02/2015
Maonesho ya Kimataifa ya Sanaa,Ubunifu na Utamaduni yanayoendelea Mascut
nchini Oman yamechukua sura mpya baada ya Nchi Washiriki kupeleka Wasanii wake wa
Ngoma za Asili kwenda kutumbwiza katika wiki mbili za mwisho ya Maonesho hayo.
Tanzania ni moja ya nchi washiriki ambapo Wasanii wake 15 Usiku wa jana walipata nafasi
ya kuburudisha kwenye Jukwaa kuu la Maonesho hayo.
Akizungumza kuhusu ujio wao Kiongozi wa Wasanii hao wa Ngoma Bi Asha Khatib
amesema wamejiandaa vizuri kuhakikisha wanazikonga vyema nyoyo za Waomani kwa
burudani ya nguvu.
Amefafanua kuwa Waoman wengi wanapenda Ngoma zenye asili ya Zanzibar hivyo
wamefanya Mazoezi ya kutosha ili kuwafurahisha Mashabiki wao pale wanapopanda
Jukwaani kwa ajili ya kutumbuiza.
“Kwa kweli tumejiandaa vizuri tu na tumekuja hapa Mascut kwa kazi moja tu ya kutoa
Burudani hivyo Waoman wazidi kuja kwa wingi kuja kujionea burudani ya aina yake yenye
Asili ya Tanzania-Zanzibar”Alisema Bi Asha.
Bi Asha amebainisha kuwa katika Jukwaa watapiga baadhi ya Ngoma zenye Asili ya
Zanzibar kama vile Msewe, Uringe, Gonga, Kyaso,Kitua tua,Kibunguu na Kidumbaki
ambapo anaamini zitakidhi kiu ya burudani kwa Waomani.
Jana ikiwa ni siku ya mwanzo kwa Watanzania hao hivyo walipewa muda wa nusu saa kwa
ajili ya kusalimia jukwaa na kutumbuiza ambapo walipiga Ngoma ya Msewe na Kitua tua.
Kabla ya Watanzania kupanda Jukwaani kwenda kutumbuiza walitanguliwa na Wasanii
kutoka Ufaransa ambapo baada ya Watanzania kumaliza Wasanii kutoka Urusi ndio
waliochukua nafasi kutumbuiza.
Nchi nyingine zilizopata nafasi ya kutumbuiza katika Jukwaa kwenye Maonesho hayo ya
Kimatifa ya Sanaa, Ubunifu na Utamaduni ni pamoja na China, Iran, Thailand, India,
Uzbekistani na Misri.
Kwa wiki mbili mfululizo kuanzia jana Wasanii wa Nchi hizo zinazoshoriki Maonesho ya
Kimataifa ya Sanaa,Ubunifu na Utamaduni watakuwa wakipanda katika Jukwaa kuonesha
vipaji vyao vya Muziki wa Asili ya nchi zao husika.
Wasanii hao wa Ngoma waliofika Juzi kutoka Tanzania wanaungana na Wenzao
waliokuwepo Oman kwa zaidi ya wiki mbili sasa kushiriki Maonesho hayo ambapo Wasanii
huonesha bidhaa zao wanazozitengeneza kwa Mikono na kuwauzia Wateja mbalimbali
wanaofika katika Maonesho hayo.
No comments:
Post a Comment