Na Abdulla Ali Maelezo-Zanzibar
Idara ya Ardhi na Mazingira inatarajia kufanya Uzinduzi wa Mfumo wa Mtandao wa Upatikanaji
Taarifa za Ardhi Zanzibar (Zanzibar Land Information Service) (ZALIS) itakayosaidia
upatikanaji wa taarifa sahihi za Ardhi nchini.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Idara hiyo uzinduzi huo utafanyika siku ya Jumatano ya tarehe
18/02/2015 katika jengo la Ardhi liliopo Forodhani Mjini Zanzibar.
Kwa mujibu taarifa hiyo imesema mtandao huo wenye teknolojia rahisi itakayosaidia
kwa kiasi kikubwa upatikanaji wa habari na taarifa zote za Ardhi ikiwemo
usajili, utambuzi, upimaji, uhaulishaji eneo, kijografia, mipaka na kuongeza
ufanisi wa shughuli zote ardhi kwa kiasi kikubwa.
Sambasamba na hayo taarifa hiyo imeeleza kuwa mfumo wa ZALIS utarahisisha
upatikanaji wa taarifa na takwimu zinazohitajika Kijamii na Kiuchumi juu ya
masuala ya Ardhi na kuzifanya shughuli hizo kuwa rahisi na nyepesi zaidi.
Aidha Serikali ya Finland
kupitia Wizara yake ya Mambo ya Nchi za Nje imekuwa ikiisaidia Zanzibar katika masuala mbalimbali ikiwemo Maji,
Mazingira, Misitu pamoja na Ardhi kwa zaidi ya miaka 10 hadi sasa.
Taarifa hiyo imefahamisha kuwa Shughuli za usajili wa Ardhi zilizinduliwa
rasmi mnamo mwaka 2013 na Rais wa Zanzibar
ambae pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dr. Ali Mohamed Shein zikiwa zinaendelea vizuri nchini.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo imeeleza maendeleo ya usajili wa Ardhi yamekuwa
yakiendelea vizuri nchini ambapo hadi sasa jumla ya vikataa 34,000
vimeshapatiwa usajili wa kudumu.
Taarifa hiyo imesema hadi sasa tayari kumeshaanzishwa Sera ya Taifa ya Ardhi,
Mkakati wa Kitaifa wa Maendeleo ya Matumizi ya Maeneo ya Ardhi, Mipango Kimkoa
Kaskazini na Kusini, Upitiaji wa Sheria zinazohusu Ardhi na Sera ya Mazingira na
ile ya Misitu zimeshafanyiwa mapitio na marekebisho.
Mfumo wa ZALIS umefadhiliwa na Serikali ya Finland
ambao umegharimu zaidi ya shilingi milioni 100 ambapo mgeni rasmi katika
Uzinduzi huo anatarajiwa kuwa Balozi wa Finland nchini Tanzania Bi. Sinnika
Antilla.
IMETOLEWA NA HABARI MAELEZO ZANZIBAR
No comments:
Post a Comment