Habari za Punde

Wasifu wa Marehemu Salmin Awadh Salmin Aliyekuwa Mwakilishi wa Jimbo la Magomeni Zanzibar.

WASIFU WA MAREHEMU MHESHIMIWA SALMIN AWADH SALMIN, MWAKILISHI WA JIMBO LA MAGOMENI
 Baraza la Wawakilishi Zanzibar, limepokea kwa mshtuko na masikitiko makubwa, kifo cha Mwakilishi wa Jimbo la Magomeni Zanzibar, Mheshimiwa Salmin Awadh Salmin kilichotokea baada ya kuugua ghafla hapo  jana Alkamis tarehe 19. 02. 2015 wakati akiwa katika kikao cha kikazi cha kichama. Mheshimiwa Salmin Awadh ambaye alikuwa Mwakilishi tangu Octoba 2005, alizaliwa tarehe 06. 06. 1958 huko Makunduchi, Wilaya ya Kusini, Mkoa wa Kusini Unguja.

Marehemu Salmin Awadh alipata elimu yake ya msingi katika Skuli ya Kiongoni kuanzia mwaka 1963 na baadaye kuendelea na masomo ya sekondari katika Skuli ya Sekondari ya Makunduchi. Vile vile  Marehemu alijiunga na Chuo cha  Uchumi Zanzibar mwaka 1971 hadi mwaka 1974.

Marehemu Mheshimiwa Salmin Awadh aliwahi kujiunga na kazi ya Ulinzi kupitia Jeshi la Wananchi JWTZ kuanzia 1976 hadi 1986 na  kufikia cheo cha Sergent. Mbali ya kazi ya hiyo ya Ulinzi, Marehemu aliwahi kuwa Meneja katika Hoteli ya Narrow Street, Zanzibar baina ya mwaka 2000 na mwaka 2005.

Katika shughuli za kisiasa, marehemu amewahi kushika nyadhifa mbali mbali katika Chama cha Mapinduzi ikiwemo Ujumbe wa Halmashauri Kuu ya tawi la Magomeni kuanzia mwaka 1982 hadi 1992, Mjumbe wa Kamati ya Siasa ya Jimbo la Magomeni tangu mwaka 1992. Mnamo mwaka 1995 hadi mwaka 2000 marehemu Salmin Awadh alikua Diwani wa Magomeni.


Mheshimiwa Salmin alikuwa Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi wa Jimbo la Magomeni, kupitia Chama cha Mapinduzi tangu Uchaguzi Mkuu wa  mwaka 2005 na kuendelea na wadhifa huo hadi kufariki kwake. Aidha Marehemu alichaguliwa Kuongoza Kamati mbali mbali  ikiwemo Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Fedha na Uchumi ya Baraza la Wawakilishi pamoja na Kamati ya Fedha, Biashara na Kilimo ya Baraza la Wawakilishi, Kamati ambayo alikuwa anaiongoza hadi kufariki kwake. 

Vile vile kutokana na umakini wake na nidhamu ya utendaji kichama mnamo mwezi Juni, 2011 Marehemu alichaguliwa kuwa Mnadhimu wa Chama cha Mapinduzi ndani ya Baraza la Wawakilishi ambapo kwa nafasi hiyo alikuwa pia Mjumbe wa Halmashauri Kuu na Kamati Kuu ya Chama cha Mapinduzi wadhifa ambao ameendelea nao hadi kufarika kwake.

Marehemu Salmin Awadh pia alikuwa miongoni mwa Mjumbe wa Bunge Maalum la Katiba na alitowa mchango mkubwa katika Bunge la Katiba ambapo alikuwa    Makamo Mwenyekiti wa Kamati namba 10 ya Bunge hilo. Aidha kutokana na uelewa wake wa masuala mbali mbali  Marehemu alichaguliwa kuwa Makamo Mwenyekiti wa Bodi ya Gazeti la Zanzibar leo  tokea mwaka 2009 hadi kufariki kwake.

Katika kipindi  chote cha kuwawakilisha wananchi wa Jimbo la Magomeni, Marehemu alikuwa mtetezi mkubwa wa maslahi ya wananchi wa jimbo hilo pamoja na wananchi wote wa Zanzibar na aliifanya kazi yake hiyo kwa moyo wake wote, uadilifu na mashirikiano makubwa na Wajumbe wenzake wa Baraza la Wawakilishi.

Ni dhahiri kuwa Baraza la Wawakilishi, Chama cha Mapinduzi,  Wananchi wa Jimbo la Magomeni na wananchi wote kwa jumla, wameondokewa na mtu muhimu na mahiri mwenye kujiamini katika kusimamia anachokiamini katika kuleta maendeleo ya Taifa.

Marehemu ameacha kizuka  na  watoto saba.

Tunamuomba Mwenyezimungu aijaalie familia ya Marehemu pamoja na wananchi wa Jimbo la Magomeni, subira na utulivu katika kipindi hiki kigumu cha msiba.  Tukielewa kwamba sote ni waja wa Mwenyezi Mungu na hapana shaka marejeo yetu ni kwake. 

Mwenyezi Mungu aiweke roho ya Marehemu mahali pema peponi. Amin.

Amour M. Amour
MKUU WA UTAWALA
BARAZA LA WAWAKILISHI
ZANZIBAR.
20 Februari, 2015.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.