Habari za Punde

Dini ya Kiislamu haipingani na uzazi wa mpango

 Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar Dkt Issa Haji Zidi akizungumza na vijana katika mjadala kuhusu uzazi wa mpango katika uislamu ulioandaliwa na Kitengo cha Shirikishi cha Afya ya mama na mtoto kwenye ukubi wa Chuo cha Mafunzo Kilimani Mjini Zanzibar. Picha na Makame Mshenga-Maelezo Zanzibar.

 Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar Dkt Issa Haji Zidi akizungumza na vijana katika mjadala kuhusu uzazi wa mpango katika uislamu ulioandaliwa na Kitengo cha Shirikishi cha Afya ya mama na mtoto kwenye ukubi wa Chuo cha Mafunzo Kilimani Mjini Zanzibar. Picha na Makame Mshenga-Maelezo Zanzibar.
 Mkufunzi kutoka Chuo cha  Sayansi ya Afya ya Mbweni Asha Ali Khamis akionyesha moja ya dawa za kisasa za uzazi wa mpango katika mjadala huo.

Mmoja wa washiriki wa mjadala kuhusu uzazi wa mpango katika uislamu  Dosa Omar Machano akitoa mchango wake kuhusu umuhimu wa uzazi wa mpango.

Na Ramadhan Ali, Maelezo      

Mhadhiri  na Mtafiti wa masuala ya Kiislamu kutoka Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) Dkt. Issa Haji Zidi amesema Dini ya Kiislamu haipingani na uzazi wa mpango na ulikuwepo  tokea wakati wa Mutume Muahmmad hivyo amewashauri waislamu kuzitumia kwa ajili ya kulinda afya zao.

Akizungumza katika mjadala kuhusu uzazi wa mpango katika Uislamu ulioandaliwa na Kitengo Shirikishi cha Afya ya uzazi na mtoto katika ukumbi wa Chuo cha Mafunzo Kilimani, Dkt. Zidi alisema  lengo la uzazi wa mpango ni kulinda afya ya mama na mtoto aliezaliwa kabla ya  mtoto mwengine.

Alisema zipo njia za asili za uzazi wa mpango  zilizokuwa zikitumiwa na masahaba wakati wa Mtume Muhammad lakini hivi sasa njia hizo zinaonekana kuwa ngumu  kwa watumiaji na  zipo njia za kisasa ambazo ni salama na za uhakika zaidi.


Alisema  tafiti   zinaonyesha kuwa familia  nyingi, hasa za vijijini zenye kipato kidogo,  ambazo zinapinga  mpango huo zimekuwa zikikabiliwa na  matatizo ya kiuchumi na afya  na kupelekea wanaume kuwatelekeza wake zao.

“ Uzazi wa mpango ni makubaliano ya mke na mume kutumia visaidizi katika uzazi ili kuchelewesha uzazi kutokana na matatizo ya kiuchumi na kiafya na wala sio njia ya  kuua ama kupunguza watoto,” alisisitiza Dkt.  Zidi.

Ameongeza kuwa lengo jengine la  uzazi wa mpango ni kulinda hadhi ya mwanamke na  kuhofia kukosa utulivu ndani ya nyumba kutokana na watoto wengi wasioweza kuhudumiwa.

Mwalimu wa  chuo cha  Sayansi ya Afya  Asha Ali Khamis  alisisitiza umuhimu wa wazazi  wawili kukubaliana kunyonyesha  mtoto miaka miwili na kupata mapumziko ya mwaka mmoja kabla ya kuzaliwa mtoto mwengine.

Aliwaeleza washiriki wa mjadala huo ambao wengi ni wanafunzi wa  Vyuo vikuu vya Zanzibar, taasisi za Serikali na NGO kwamba zipo njia za muda mfupi, muda mrefu na njia ya kudumu na zote ni salama pamoja na  baadhi ya  watumiaji kupata mabadiliko madogo madogo ya kimwili.

“Mabadiliko ya kiafya yanayotokea kwa baadhi ya watu wanaotumia dawa hizi isiwe tatizo kwani mara nyingi hutokea katika siku za mwanzo wakati mwili bado haujazoea, ” alisema mwalimu Asha.

Akitoa takwimu za mama wanaopoteza maisha  wakati wa kujifungua Zanzibar , muwezeshaji kutoka UMATI  Mwanajuma Othman  alisema kila wanawake laki moja  288 hufariki.

Alsema idadi hiyo ya  vifo ni kubwa ikilinganishwa na nchi nyengine hasa ikizingatiwa kuwa  vifo hivyo vinaweza kuepukika ikiwa hatua muafaka zitachukuliwa mapema.

Baadhi ya washiriki wa mjadala huo  walionyesha  wazi  wazi kuwa  baadhi ya familia zimekuwa na mashaka ya kutumia dawa za uzazi wa mpango kutokana na imani zao za  dini na kuhofia matatizo ya afya zao .

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.