Habari za Punde

Mchezo wa Golf wakabiliwa na changamoto za kupotea

Na Mwajuma Juma, Zanzibar
 
PAMOJA na kufunguliwa kwa kiwanja cha mchezo wa Golf lakini mchezo huo unaonekana kupotea kutokana na mazingira ya gharama ya mchezo huo.
 
Hayo yamebainishwa na Katibu wa Chama Cha Mchezo huo Zanzibar Ikram Mohammed alopokuwa akizungumza na mwandishi wa habari hizi huko katika uwanja wa mazoezi Maisara.
 
Alisema kuwa pamoja na sababu hiyo pia mchezo huo utaweza kufa kutokana na kutojaliwa kwa kiwanja cha kufanyia mazoezi ambacho kimegeuzwa kuwa cha watu kujifundishia gari.
 

“Mchezo huu kiukweli unapotea japo hivi karibuni kulifunguliwa uwanja wa golf lakini kutokana na mazingira ya gharama za mchezo kwa wachezaji wetu hawa wa kawaida watakuwa wengi sana watashindwa kuzimudu na kuendelea na mchezo huo”, alisema.
 
Hata hivyo alisema kuwa mchezo huu asili yake huchezwa katika majani lakini kutokana na sasa viwanja kuendeshewa gari viwanja vimekosa hiaba yake na wakati mwengine inakuwa ni vigumu kufanyia mazoezi kwani wakati mpo katika mazoezi mara gari zinapita jambo ambalo linakuwa ni hatari kwa wachezaji na hata wenye magari.
 
 
“Uzuri wa michezo kama mpira wa miguu na huu wa golf ni kuchezwa katika majani si katika michanga lakini utakuta viwanja vyetu sisi vinatoweka kutokana na kuendeshwa magari”, alisema.
 
 Alisema kuwa suala hilo wamekuwa wakilipigia kelele sana wao kama wanamichezo lakini halijaweza kudhibitiwa wala hakuna mwenye kujali kwa sababu wengi sio wanamichezo kwa uhalisia wa hapa Zanzibar.
 
Alisema kuwa chama chake kinashindwa kutoa wachezaji katika michezo ya mashule kama vile UMISETA tofauti na michezo mengine kutokana na kukosekana kwa viwanja kwani hapo awali viwanja vya maisara vilikuwa ni kiwanja cha Golf.
 
Aidha alisema kuwa kila miaka ikiendelea kusonga mbele viwanja hivyo vimezidi kuchukuliwa na wachezaji mpira  na sasa hivi kimekuwa cha ufundishaji wa magari  na utakuta mchezo wao unatoweka nah ii si kwa Golf tu bali michezo mengi midogo midogo inaonekana kutoweka kutokana na kutovijali viwanja vya michezo.
 
Hata hivyo alisema kuwa mchezo huo ni wa gharama lakini kama kungalikuwa na kiwanja cha Serikali gharama zingalionekana kupunguwa na wachezaji wangalikuwa wengi zaidi.
 
Akizungumzia kuhusu kiwanja kilichofunguliwa hivi karibu katika hotle ya Sea Cliff Kiomba Mvua alisema kuwa si rahisi kwa mchezaji wa nyumba kuweza kukitumiakiwanja hicho kwani mchezaji ili aweze kukitumia alipie dola 40 kwa mtanzania, kiasi ambacho alikisemea ni ghali kwa mchezaji wa kawaida.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.