Tukijaaliwa
siku ya Ijumaa tarehe 20/03/2015 katika nchi ya Uingereza, na sehemu nyengine
za Ulaya jua litapatwa majira ya asubuhi kuanzia saa 3.30 kwa mujibu wa wakati
wa Uingereza.
Kupatwa
kwa jua ni jambo nadra sana kutokea kwani mara ya mwisho hapa Uingereza jua
lilipatwa mwaka 1999. Na kwa mujibu wa wataalamu jua litapatwa tena mwaka 2026
bi ithni Llaah.
Nini
anapaswa Muislamu kufanya jua likipatwa?
Kwa
mujibu ya hadithi aliyoisimulia Al Mughiyrah , Allaah amuwie radhi, amesema:
Mtume swalla Allaahu ‘alayhi wasallam amesema:
‘Hakika jua na mwezi ni
alama mbili miongoni mwa alama za Allaah, Hayapatwi kwa sababu ya mauti ya mtu
au uhai wake na mkiona (kupatwa huku), ombeni du’aa kwa Allaah na msali mpaka
litakapoachiwa’
Bukhaari na Muslim.
Sala
hii, kwa mujibu wa Maulamaa, ni Sunnah iliyotiliwa mkazo na ni miongoni mwa Sala
za sunnah za nadra kutokea katika uhai wa binadamu kwani imesimuliwa kwamba Mtume
swalla Allaahu ‘alayhi aliisali sala hii mara moja tu katika uhai wake siku
alipofariki mwanawe Ibraahim, na watu wakaunganisha tukio la kufa mwanawe na
kupatwa kwa jua mpaka ikambidi atoe ufafanuzi kwamba vitu hivi viwili havihusiani.
Vipi
Sala ya Kusuuf husaliwa:
Husaliwa
Jamaa msikitini na ndio vizuri zaidi (wanawake wanaweza kutoka na kwenda kusali
msikitini ikiwa hakutokuwa na fitna pia wanaweza kusali majumbani)
Haina
adhana wala Iqaamah.
Baada
ya sala hufuatiwa na Khutbah na kuomba du’aa.
Ina
Rakaa mbili kila rakaa huwa na rukuu mbili, visimamo viwili na visomo viwili (tofauti na sala za kawaida zenye rukuu moja, kisimamo kimoja na kisomo kimoja)
Utaratibu
wake kwa ufupi
- Unaleta takbiiratul Ihraam
- Unasoma Suuratul Faatihah
- Unasoma sura nyengine ( vizuri iwe ndefu mfano wa baqarah)
- Unarukuu rukuu iliyokuwa ndefu
- Unasimama baada ya kurukuu na kusema Samia Llaahu liman hamidah Rabbanaa walakal hamd
- Unasoma Suuratul Faatihah tena
- Unasoma Sura nyengine vizuri iwe ndefu chini ya sura ya mwanzo
- Unarukuu rukuu iliyokuwa ndefu chini ya urefu wa rukuu ya kwanza
- Unasimama baada ya kurukuu na kusema Samia Llaahu liman hamidah Rabbanaa walakal hamd
- Unasujudu sijda ya kwanza
- Unakaa kitako baina ya sijda mbili na kuomba dua kama kawaida
- Unasujudu sijda ya pili na kuomba du’aa
- Unainuka na kuanza rakaa ya pili na kufanya kama ulivyofanya rakaa ya kwanza hadi mwisho wa Sala kwa kuleta tashahhud na kisha kutoa salam.
Tujitahidi
kuhakikisha tunaisali sala hii tukijaaliwa kesho kwani tutakuwa tunahuisha
Sunna za Mtume wetu Swalla Allaahu ‘alayhi wasallam na pia kuonesha umuhimu wa
dini yetu yanapotokea matukio yasiokuwa ya kawaida kwamba tunarudi kwa Mola wetu
na kuomba.
Allaahumma
Aamiyn
SHEKH Allah akujaze kheri kwa kutufunza mimi nilikuwa hata sijui, lakini nikijaaliwa kesho nami nitashiriki kuitekeleza sunna hii inshaalah
ReplyDeleteShukran Maalim kwa ukumbusho uliobeba ujumbe mzito ndani yake, Allah akulipe kheri akhera na duniani, kwa wasiojaaliwa kuswali kuna nyiradi zozote ambazo wanaweza wakasoma?
ReplyDelete