STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar
29.3.2015
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein leo aliungana pamoja na Vijana wa Chipukizi
walioshiriki katika Sherehe za miaka 51 ya Mapinduzi ya Zanzibar ya Januari 12,
2015 katika chakula maalum cha mchana alichowaandalia vijana hao
na kuwapongeza kwa ushiriki wao huo.
Katika hafla hiyo
ya chakula cha mchana iliyofanyika katika ukumbi wa Hoteli ya Bwawani, viongozi
mbali mbali walihudhuria akiwemo Makamo wa Pili wa Rais Balozi Seif Ali Idd,
Mawaziri, viongozi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) pamoja na viongozi wengine wa
Serikali.
Akitoa neno la
shukurani kwa niaba ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.
Shein Ali Mohamed Shein, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Ikulu na Utawala Bora
Dk. Mwinyihaji Makame Mwadini alitoa pongezi kwa Vijana hao wa Chipukizi kwa
kushiriki kikamilifu katika Sherehe hiyo adhimu hapo Januari 12, mwaka huu huko
katika uwanja wa Amaan mjini Zanzibar.
Alisema kuwa
Sherehe ya miaka 51 ya Mapinduzi matukufu ilifanyika kwa ustadi mzuri na
ushiriki wa vijana hao ulikuwa mzuri katika gwaride, maandamano pamoja na
halaiki maalum iliyowashikirisha, na kuweza kuipamba sherehe hiyo adhimu ya
miaka 51 ya Mapinduzi Matukufu ya Januari 12, 1964 huku akiwasisitiza vijana
hao kuwa na uchungu na kuzidi kuipenda nchi yao.
Dk. Mwinyihaji
alisema kuwa kuna kila sababu ya kuyaenzi, kuyatunza na kuyasherehekea
Mapinduzi ya Januari 12, 1964 kwani ndio yaliyowakomboa wanyonge wa Zanzibar.
Aidha, Dk.
Mwinyihaji Makame aliwataka vijana hao pamoja na wananchi wote wa Zanzibar
kuendelea kuyapenda Mapinduzi ya Zanzibar sambamba na kuendelea kusherehekea
maadhimisho yake kila wakati unapofika kutokana na umuhimu wake mkubwa.
Pamoja na hayo,
Dk. Makame aliwasihi na kuwasisitiza vijana hao kuendelea kusoma kwa bidii
kubwa na huku akiwaeleza kuwa hatua za makusudi zilizochukuliwa na Rais wa
Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein kutangaza rasmi
kuondoa michango maskulini kuanzia mwaka huu ni jambo la busara ambalo
litawasaidia wao vijana pamoja na wazazi wao kwa jumla.
Alisema kuwa hiyo
ndio azma ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya kuondoa michango yote
iliyokuwa ikitolewa hapo kabla hatua ambayo imeweza kuungwa mkono na Waziri
husika wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Mhe. Ali Juma Shamuhuna kwa
kusisitiza kuwa hakuna mtoto hata mmoja atakae fika umri wa kuanza masomo na kukosa
elimu kwa sababu ya kutotoa mchango wa skuli.
Akiendelea kutoa
salamu kwa niaba ya Dk. Shein, Dk. Mwinyihaji alitumia fursa hiyo kwa kutoa
pongezi kwa Kamati ya Sherehe na Mapambo chini ya uongozi wa Makamu wa Pili wa
Rais, Balozi Seif Idd pamoja na viongozi wengine wa Wizara hiyo na nyenginezo
ambao wameshiriki kikamilifu katika maandalizi ya shehere hizo.
Pia, Alitoa
shukurani kwa waandaanji wa hafla hiyo pamoja na ile iliyofanyika hapo jana kwa
ajili ya vikosi vya Ulinzi vilivyoshiriki katika gwaride la kutimiziza miaka 51
ya Mapinduzi ya Januari 12, 2015, hafla ya chakula ambayo ilifanyika katika
Kambi ya Bavuai, Migombanai mjini Zanzibar.
Hafla hiyo ilipambwa
na taarab maalum ya kikundi cha ‘Diamond Taarab’ ambacho kiliweza kutumbuiza
kwa nyimbo zao mbali mbali za midundo ya kileo na ile midundo ya asili na
kuweza kutoa burudani safi kwa vijana na waalikwa wote waliofika katika hafla
hiyo.
Mapema Mkuu wa
Halaiki ya vijana hao, Bwana Ali Mohammed Baraka alitoa shukurani kwa Dk. Shein kwa
niaba ya vijana hao na kueleza kuwa kuwaandalia chakula hicho cha mchana vijana
hao ni kuonesha mapenzi makubwa aliyonayo Dk. Shein kwa vijana na kutumia fursa
hiyo kuwashukuru vijana hao kwa kuendelea kulitendea wema Taifa lao.
Hafla hiyo ni
muendelezo wa utamaduni aliouweka Dk. Shein wa kuwapongeza na kuwaandalia
chakula cha mchana vikosi vya ulinzi pamoja na Chipukizi ambao hushiriki katika
maadhimisho ya Sherehe za Mapinduzi matukufu ya Zanzibar zinazofanyika kila
ifikapo Januari 12 ya kila mwaka.
Rajab
Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024
2231822
E-mail:
rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment