Habari za Punde

Walimu jimbo la Uzini wafanya ziara ya kimasomo Mkoa wa Lindi


Mke wa Rais wa Jamuhuri ya Mungano wa Tanzania Mama Salma Kikwete amefurahishwa na hatuwa iliyochukuliwa na Walimu wa Jimbo la Uzini Zanzibar ya kufanya ziara ya kimasomo Mkoani Lindi kwani ni njia moja wapo ya kujifunza na kujiongezea elimu kwa vitendo.


Hayo ameyasema Jana wakati akiwakaribisha walimu wa Jimbo hilo Mkoani hapo kwa ajili ya kuanza rasmi ziara yao ambayo inatarajiwa kuchukuwa takribani wiki moja.   


Aidha Mama Salma amesema ziara za kimasomo ni njia moja ya kuleta mashirikiano na kudumisha Muungano wa Watanzania katika kuboresha Sekta ya Elimu Nchini hiyo ni kwa sababu  Elimu ya Juu na Sekondari nchini Tanzania ni moja ya mambo yaliyo chini ya Serikali ya Muungano.

                                                        

Akizungumzia Changamoto zinazowakabili Walimu hao  katika Sekta ya Elimu  kwa upande wa Mkoa wa Lindi ni upungufu wa walimu wa masomo ya Sayansi jambo ambalo  husababisha kukosekana kwa wataalamu wa fani mbalimbali za Kisayansi kwa maendeleo ya Taifa ambapo  hurudisha nyuma jitihada zao za kutaka kuzalisha wataalamu watakaokwenda sambamba na ulimwengu wa Sayansi na Teknolojia.

                                                                                                                                                    

Nae Afisa Uendeshaji wa Wizara ya Elimu Zanzibar Nd. Muhussin Sufiani Mkanga amesema lengo kuu la ziara hiyo ni kujifunza njia mbalimbali zilizobora za kielimu ikiwa ni njia za kuwafundishia wanafuzi wa Zanzibar katika kuimarisha ufaulu mzuri kwa wanafunzi wa Kidato cha Nne.


Hata hivyo amewataka walimu wenzake waliopata fursa kuwepo katika ziara hiyo kuwa makini katika kujifunza masomo hayo kwa lengo la kupata njia zilizo bora za  utoaji wa  elimu kwa  wanafunzi wao ikiwa ni mfano mzuri wa kuigwa na walimu wengine Nchini.

 

Jumla ya walimu 36 kutoa Zanzibar wamepata fursa ya ziara ya kimasomo Mkoani Lindi na wanatarajiwa kuwa mabalozi wazuri kwa walimu wenzao waliokosa fursa hiyo kwa kuwapa yale yote mazuri waliyoyapata na kuyafanyia kazi kwa maendeleo ya Nchi yao.


                                                                                      IMEHARIRIWA NA HABARI MAELEZO-ZANZIBAR

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.