Habari za Punde

Dk Bilal akutana na waziri wa Waziri wa Nchi Maendeleo na Francophonie wa Ufaransa Mhe. Annick Girardin

 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akisalimiana na kumkaribisha Ofisini kwake Waziri wa Nchi Maendeleo na Francophonie wa Ufaransa Mhe. Annick Girardin, wakati alipofika Ofisini kwake Ikulu Dar es salaam leo April 09, 2015.

 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akizungumza na Waziri wa Nchi Maendeleo na Francophonie wa Ufaransa Mhe. Annick Girardin aliyeongoza ujumbe wa watu tisa, wakati alipofika Ofisini kwake Ikulu Dar es salaam leo April 09, 2015.
 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Mohammed Gharib Bilal katikati, Waziri wa Nchi Maendeleo na Francophonie wa Ufaransa Mhe. Annick Girardin kushoto na Balozi wa Ufaranza Nchini Tanzania Mhe. Malika Barak, wakiwa kwenye picha ya pamoja nje wa Ofisi ya Makamu wa Rais Ikulu Dar es salaam leo April 09, 2015.
 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akiagana na Waziri wa Nchi Maendeleo na Francophonie wa Ufaransa Mhe. Annick Girardin, baada ya kumaliza Mazungumzo yao Ofisini kwake Ikulu Dar es salaam leo April 09, 2015. (Picha na OMR)

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Mohammed Gharib Bilal amekutana na ujumbe kutoka serikali ya Ufaransa ambapo wamezungumzia mchango wa Tanzania na Afrika kwa ujumla katika kuhimili mabadiliko ya tabianchi na kupunguza gesi joto.
Ujumbe huo wa watu tisa ambao unaongozwa na Waziri wa Nchi wa Maendeleo ya  Francophonie anayeshughulika na masuala ya mazingira wa Ufaransa Mheshimiwa Annick Girardin ulikutana na Dkt. Bilal leo ofisini kwake Ikulu.
Waziri Annick alimweleza Dkt. BiLal kuwa lengo la ziara yake katika nchi za Ethiopia, Tanzania na Kenya ni kuhimiza baadhi ya nchi za Afrika ambazo zinaweza kutoa mchango mkubwa katika kufikia makubaliano ya Mkataba Mpya wa Mabadiliko ya Tabianchi unaotarajiwa kupitishwa mjini Paris, Ufaransa.  
Alisema mwaka huu Ufaransa inaandaa mkutano wa 21 wa Mkataba wa Mabadiliko ya Tabianchi na kuiomba Tanzania iendelee kushiriki kikamilifu kwa kutoa mchango wake katika maandalizi ya Mkataba Mpya katika mkutano huo.
Makamu wa Rais aliuambia ujumbe huo kuwa Tanzania itaendelea kushirikiana na nchi nyingine za Afrika katika kuhakikisha mkutano huo unakuwa wa mafanikio hasa kwa sababu ya kazi kubwa Tanzania iliyofanya kama Mwenyekiti wa Kamati ya Marais wa Afrika ya Mabadiliko ya Tabianchi (CAHOSCC) na kusimamia kamati mbalimbali za Mkataba Mpya.
Alisema katika maandalizi ya mkutano huo Tanzania imeanza mchakato katika kuainisha maeneo muhimu ya mchango wake kwa juhudi za dunia za kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi (INDC) yakiwamo ya sekta za kilimo, mifugo, maji, misitu na ardhi.
Aidha alisema sekta za nishati, usafirishaji, udhibiti wa taka zimeainishwa pia kama maeneo yanayoweza kuchangia kupunguza gesi joto..
Hata hivyo, Dkt. Bilal aliiomba Ufaransa kuisaidia Tanzania kwa utaalam na teknolojia ili nchi iweze kufanikisha azma yake ya kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi na kutoa mchango wake wa kupunguza gesi joto bila kuathiri maendeleo jambo ambalo Waziri Annick alilikubali.
Akizungumzia kwa upande wa Afrika kwa ujumla Makamu wa Rais alisema karibu nchi nyingi za Afrika zimeathirika kutokana na mafuriko ya mara kwa mara na ongezeko la kina cha bahari kiasi cha kusababisha baadhi ya visiwa vidogo kuzama. Alisema  ukame na mmomonyoko wa udongo ni tatizo kubwa kwa nchi za Afrika.
Dkt. Bilal alitumia fursa hiyo kuishukuru Serikali ya Ufaransa kwa misaada yake katika sekta za elimu, nishati, mabadiliko ya tabianchi na maji na kutoa mfano wa mradi wa maji wa Musoma ambao utanufaisha wananchi wa mji huo baada ya kukosa maji safi na salama kwa muda mrefu.
Waziri Annick na ujumbe wake wanatarajia kwenda Kenya ambapo kesho pamoja na mambo ya mengine atagusia masuala ya ugaidi.
 
Imetolewa na Ofisi ya Makamu wa Rais
Dar es salaam
9/4/2015

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.