STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar 13 Aprili, 2015
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amepongeza mshikamano na moyo wa kujitolea miongoni mwa wanachama na wapenzi wa Chama cha Mapinduzi ambao umewezesha chama hicho katika mkoa wa kichama wa Mjini, Unguja kukukusanya michango ya jumla ya shilingi milioni 387.21.
Katika hotuba yake fupi kuwashukuru wachangiaji katika hafla ya chakula cha jioni kuchangia Mfuko wa Maendeleo wa Chama cha Mpinduzi Mkoa wa Mjini, Unguja jana, Dk. Shein alisisitiza umuhimu wa kuimarisha mshikamano na kurejesha moyo na ari ya kujitolea miongoni mwa wanachama na wapenzi wa chama hicho katika mnasaba wa kukiimarisha chama hicho.
“mapenzi na mshikamano wa kukichangia chama chetu ni muhimu sana katika kukiimarisha hususan wakati huu tukielekea uchaguzi mkuu” Dk. Shein aliwaeleza wageni waliohudhuria hafla hiyo akiwemo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi.
Aliwakumbusha wageni waliohudhuria hafla hiyo kuwa kuchangia shughuli za chama ni utaratibu uliozoeleka tangu wakati wa vyama vya Afro Shirazi na TANU na kwamba ni kutokana na michango ya wanachama na wapenzi wake vyama hivyo viliimarika na kufanikiwa kuleta ukombozi wa wanyonge.
Alieleza kuwa amefarijika na kutiwa moyo na jinsi washiriki wa hafla hiyo walivyoonesha ari ya kuchangia kadri ya uwezo wao na kuwezesha chama kukusanya kiasi hicho cha fedha.
Kwa hivyo aliipogeza Kamati ya Maandalizi ya hafla hiyo iliyoongozwa na Mwenyekiti wake Ndugu kwa maandalizi mazuri hadi kufikia matokeo hayo.
“Sikuwa na shaka hata kidogo na Kamati hii na imedhihirika hapa kama mlivyoona shughuli imeandaliwa vyema na kwa mipangilio mahsusi na nilitarajia lengo la shilingi mioni 300 lililowekwa na mkoa lingevukwa na ndivyo ilivyotekea” Dk. Shein alisema.
Kwa hivyo alieleza matumaini yake kuwa fedha hizo zitatumika kwa kutekeleza malengo yaliyowekwa ya kukiimarisha chama katika mkoa huo na kusisitiza haja ya chama hicho katika ngazi zote kuwa na mipango thabiti kukidhi matarajio ya wananchi.
“CCM ni chama kinachotegemewa na wananchi wengi kwa kuwa ni chama chenye uwezo mkubwa wa kupanga na kutekeleza mipango madhubiti kwa mafanikio makubwa hivyo ni lazima turejeshe imani hiyo ya wananchi kwa kufanya kile ambacho wananchi hao wanakitarajia” Dk. Shein alisisitiza.
Katika kuchangaia vitu mbalimbali vilipigwa mnada mojawapo ni Kitabu cha Miaka 50 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ambacho kilinunuliwa kwa shilingi milioni 15.
Katika hafla hiyo iliyofanyika katika hoteli ya Bwawani Dk. Shein ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar alichangia shilingi milioni 15 na mke wake mama Mwanamwema Shein alichangia milioni 5.
Alitumia fursa hiyo kuwapongeza wachangiaji mbalimbali wakiwemo viongozi na wafanyabishara wa Zanzibar na Tanzania bara pamoja na taasisi mbalimbali zilizoshiriki.
Miongoni mwa wachangiaji ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Jakaya Mrisho Kikwete na Mke wake Mama Salma Kikwete, Waziri Mkuu Mizengo Pinda, Makamu wa Pili wa Rais Balozi Seif Ali Iddi, familia ya Rais Mstaafu Alhaj Ali Hassan Mwinyi, Waziri Mkuu wa zamani Edward Lowassa, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Mahusiano na Uratibu) wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Stephen Wasira pamoja na makampuni na watu binafsi.
Akitoa maelezo kuhusu hafla hiyo Katibu wa Chama cha Maapinduzi Mkoa wa Mjini Mohamed Omari Nyawenga alieleza kuwa lengo la kuanzisha Mfuko wa Maendeleo wa Chama mkoa huo ni kukiwezesha chama mkoani humo kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi.
Katibu huyo alieleza kuwa miongoni mwa matumizi ya fedha hizo ni kuendeleza ujenzi wa jengo la chama mkoa, ujenzi wa nyumba ya Katibu wa Mkoa na kuanzisha kituo cha redio kitakachosaidia mafunzo kwa wanafunzi wa Chuo cha Mwenge ambacho kinamilikiwa na chama mkoa.
No comments:
Post a Comment