STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar 9.4.2015
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein leo amefanya ziara ya kutembelea na kuangalia
maendeleo ya ujenzi wa uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume.
Dk. Shein alifanya
ziara hiyo mapema leo asubuhi akiwa ameongozana na viongozi wa Wizara ya Miundombinu na Mawasiliano, Wizara ya Nchi
Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Idara Maalum, uongozi wa Wizara ya Fedha na
viongozi wengineo wa Mamlaka ya Uwanja huo.
Mapema Dk. Shein
alipata maelezo kutoka kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Miundombinu na Mawasiliano
Dk. Malick Akili ambaye alimueleza hatua zinazoendelea katika ujenzi wa jengo
jipya la abiria pamoja na mradi wa ujenzi wa uzio katika uwanja huo.
Katika maelezo
yake, Dk. Malick alisema kuwa ujenzi wa jengo la abiria unaendelea vizuri hivi
sasa chini ya Kampuni ya Kichina ya Beijing Construction Engineering Group Co.
Ltd (BCEG).
Katibu Mkuu huyo
alitoa maelezo juu marekebisho ya ujenzi wa jengo jipya la uwanja wa ndege wa
Abeid Amani Karume pamoja na hatua za ujenzi wa uzio unaozunguka uwanja huo.
Akieleza kuhusu
mradi wa ujenzi wa uzio, Katibu Mkuu huyo alisema kuwa hadi kufikia hivi sasa
sehemu iliyowazi ambayo mkandarasi anaendelea na kazi ni takriban mita 500
iliopo sehemu ya Kaskazini Magharibi ya kiwanja na kusisitiza kuwa ili
kukamilisha eneo hilo la uzio kwa kipande cha mita hizo jumla ya TZS milioni
560 zinahitajika.
Aidha, Dk. Shein
kabla ya kuanza ziara hiyo alitembelea kituo cha Zimamoto na Uokozi kiliopo
uwanjani hapo na kupata maelezo juu ya
uimarishaji wa Kikosi cha Zimamoto kiwanjani hapo kutoka kwa uongozi wa Kikosi
hicho.
Katika ziara yake
kwenye ujenzi wa jengo jipya la abiria la uwanja wa ndege wa Abeid Amani
Karume, Dk. Shein alipata maelezo kutoka kwa viongozi wa Wizara ya Miundombinu
na Mawasiliano pamoja na kutoka kwa Mshauri Elekezi mpya wa Kampuni ya ADPI ya
Ufaransa bwana Verna Guillaume.
Kwa mujibu wa
maelezo ya Mshauri Elekezi wa Kampuni ya ADPI bwana Guillaume kutoka Ufaransa,
alimueleza Dk. Shein hatua za ujenzi zinazoendelea vizuri huku akitoa maelezo
juu ya marekebisho kadhaa ya ujenzi huo unaoendelea ambayo yatasaidia katika
kufikia lengo lililokusudiwa.
Nae, Msimamizi Mkuu wa Mradi wa Ujenzi wa jengo
jipya la abiria Bwana Yasser De Costa
alitoa maelezo kadhaa kwa Mhe. Rais juu ya ujenzi huo unaoendelea ambao
utasaidia kwa kiasi kikubwa kutoa huduma kwa wageni na wenyeji wanaosafiri
kupitia jengo hilo jipya na la kisasa.
Ongezeko la eneo
la jengo baada ya masawazisho hayo ya kiufundi yatapelekea kuongezeka kwa uwezo
wa jengo hilo kuhudumia jumla ya abiria milioni 1.6 badala ya abiria milioni
1.1 iliyopangwa kupitia mkataba wa awali.
Sambamba na hayo,
takwimu zinaonesha kuwa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Abeid Amani Karume
kinakadiriwa kuchukua abiria wapatao milioni 2 ifikapo mwaka 2025, hatua ambayo
pia, itachangia kukuza uchumi na kuimarisha
sekta ya utalii hapa Zanzibar.
Rajab
Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024
2231822
E-mail:
rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:
Post a Comment