Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, akikata utepe kuashiria uzinduzi rasmi wa “Green house” ya Bopwe Wete, ikiwa ni miongoni mwa Green House 10 za Jimbo la Gando.
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, akisisitiza jambo akiwa ndani ya “Green house” ya Bopwe Wete.
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, akizungumza na wajasiriamali wa jimbo la Gando, baada ya kuzindua “Green house” ya Bopwe Wete.
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, akiangalia bidhaa iliyotengenezwa na wajasiriamali wa jimbo la Gando, baada ya kuzindua “Green house” ya Bopwe Wete.
Mkurugenzi wa kampuni ya Affordable Green House ya nchini Kenya bw. Timothy Nyuguna kutoka nchini Kenya, akizungumza katika hafla hiyo ya uzinduzi. (Picha na Salmin Said, OMKR)
Na: Hassan Hamad, OMKR
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, amewataka wakulima kuongeza juhudi katika kilimo cha kisasa ili waweze kuongeza kipato chao.
Akizindua mradi wa kilimo cha mbogamboga kinachotumia teknolojia ya kisasa “green house” huko Bopwe jimbo la Gando, Maalim Seif amesema iwapo wakulima watatumia vyema elimu wanayopewa na wataalamu wa kilimo hicho, wanaweza kuongeza tija na kupata mafanikio kwa kipindi kifupi.
Kilimo hicho cha kisasa kimo katika mpango wa wajasiriamali wa jimbo la Gando (GEP), unaowahusisha wajasiriamali wapatao mia tisa wa Jimbo hilo.
Ameuhimiza uongozi wa Jumuiya hiyo kukuza mashirikiano na wadau wanaowaunga mkono, ikiwa ni pamoja na kuweka mikakati ya kurejesha madeni wanayokopa.
Maalim Seif ambaye ni mlezi wa Jumuiya hiyo ya wajasiriamali jimbo la Gando, amewashukuru wadau wa mradi huo wakiwemo benki ya CRDB, na kuahidi kuwa Serikali itatoa ushirikiano unaohitajika ili kuhakikisha kuwa malengo ya jumuiya hiyo yanafanikiwa.
Mapema akisoma risala ya wajasirimali hao, Bw. Salim Said Khalfan amesema mradi huo unaojumuisha vikundi 53 vya wajasiriamali wa jimbo la Gando, umepata mafanikio makubwa tangu kuanzishwa kwake.
Hata hivyo amesema bado wanakabiliwa na changamoto kadhaa zinazohitaji kupatiwa ufumbuzi ikiwa ni pamoja na mtaji mdogo wa kuendeshea mradi huo pamoja na vitendea kazi vya kisasa.
Akitoa taarifa ya kitaalamu kuhusu kilimo hicho cha kisasa cha mboga mboga, Mkurugenzi wa kampuni ya Affordable Green House ya nchini Kenya bw. Timothy Nyuguna kutoka nchini Kenya, amesema kilimo hicho kinaweza kuleta tija kubwa iwapo masharti yaliyowekwa yatazingatiwa.
Ametaja masharti hayo kuwa ni pamoja na udhibiti wa maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya kilimo hicho, ili yawemo katika uangalizi wakati wote ili kuepusha uharibifu unaoweza kujitokeza.
No comments:
Post a Comment