Na Miza Kona na Maryam Kidiko.-Maelezo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Ukimwi Zanzibar Ali Salum Ali amesema utumiaji wa dawa za kulevya hupoteza heshima ya mtu kwa jamii katika kipindi cha utumiaji wa dawa hizo pamoja na kukosa uaminifu ambao ni haki ya msingi katika maisha ya kila mwanajamii .
Hayo ameyasema huko katika ukumbi wa Hospital ya Kidongochekundu wakati akifunga mafunzo ya Ujasiriamali kwa Wasichana 25 Walioachana na Matumizi ya Dawa za Kulevya.
Amesema utumiaji na utegemezi wa dawa za kulevya hupoteza lengo na mwelekeo mzuri wa mtu katika maisha yake jambo ambalo linapaswa kuepukwa katika jamii.
Amefahamisha kuwa Utumiaji wa Dawa ya kulevya hupelekea mtu kuwa katika hali hatarishi ya kupata maradhi mbalimbali ikiwemo UKIMWI, Homa ya Ini na kuwataka Wasichana hao kutothubutu kurudia tena kutumia Dawa hizo.
Amefahamisha kuwa kuachana na matumizi ya dawa za kulevya husaidia kurudisha Imani na uaminifu kwa Jamii kwani hupelekea Mtu kujishughulisha na harakati za uchumi badala ya kuitegemea familia yake kimahitaji.
Aidha Mkurugenzi Ali ameeleza matumaini yake juu ya Mafunzo hayo ya ujasiriamali kuwa yataweza kuwasaidia washiriki hao katika kujitafutia kipato cha halali na kujikimu kimaisha.
Nao washriki wa mafunzo hayo wamesema watayatumia vyema mafunzo waliyoyapata na kuitaka jamii isiwatenge bali washirikiane katika kuleta maendeleo
“Tunaiomba Serikali itenge eneo maalum la kuweza kujenga sehemu ya wanawake nje ya mji ili kuweza kuondosha usumbufu wa kukosa nyumba za kukaa kwani tunapata tabu nyumba tunazoishi ni za kukodi na hiyo kodi yenyewe huzidishwa kila mara hivyo tunashindwa kutokana na kuwa fedha za kujikimu hazitoshi inabidi tutowe wenyewe na sisi tunafamilia zinatutegemea inakuwa mzigo mkubwa”, wamesisitiza washiriki hao.
Washiriki hao pia wameitaka jamii kuwafichuwa wale wote wanaohusika na uuzaji wa Dawa za kulevya kwa kupeleka taarifa katika vituo husika ili kuondosha tatizo hilo nchini.
Nae mwanzilishi na mlezi wa Nyumba za Kurekebisha Tabia Bi Fatma Sukwa amesema changamoto kubwa inayowakabili katika kazi yao hio ni ukosefu wa fedha za kujikimu katika kuwashughulikia waathirika pamoja na nyumba za kukaa wakati wa kutoa huduma hiyo
“Wanawake wa Zanzibar wanaotumia dawa za kulevya wanaokuja hapa wengi wao hawakusoma, katika kuwaendeleza inakuwa shida kwa upande mmoja kwani jamii inakuwa sio rahisi kuwasaidia hasa katika kuwalipia hivyo inabidi tuwaisaidie sisi kwa kujitolea na vile vile wanapotoka katika nyumba hizi za Kurekebisha Tabia Soba House wanaporudi katika familia zao huwa haziwakubali hivyo huwabidi kurudi kwa mabwana zao na kurejea tena katika utumiaji wa madawa ”, alifahamisha Bi Fatma.
Bi Fatma amewashauri vijana wanaotumia madawa ya kulevya kutumia methadon kwani hazina madhara yoyote ili waweze kuachana na madawa hayo na kuepukana na utegemezi kwa kujishughulisha na ujasiriamali ili kuweza kujikimu kimaisha.
Mafunzo hayo ya Amali ya siku sita ambayo yalijumuisha Wasichana 25 yamefadhiliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Idadi ya Watu UNFPA.
No comments:
Post a Comment