Habari za Punde

Tanzania yashiriki katika mkutano wa kamisheni kuhusu idadi ya watu na maendeleo

 Naibu Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa,  Balozi Ramadhan Mwinyi akizungumza wakati wa Mkutano wa 48 wa Kamisheni ya Idadi ya Watu na Maendeleo, Tanzania ni  mjumbe wa Kamisheni hii  ikiwa ni kati  ya nchi 12  kitoka Afrika zikiliwakilisha  Bara ya Afrika.  pamoja na naye ni Bw. Seif Shaban Mwinyi,  Kamishna wa Mipango  kutoka Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na Bw. Stephen Kiberiti kutoka Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii
Sehemu wa Wajumbe kutoka nchi 47 zinazounda  Kamisheni ya  Idadi ya Watu na  Maendeleo.  wajumbe wa  kamisheni hii, 12 wanatoka  nchi za Bara la Afrika , 11  kutoka Bara la Asia na Pacific, 5 kutoka nchi za  Ulaya Mashariki,  9 wanatoka Latini ya Amerika na  Visiwa na Karibiani, na 10 wanatoka Nchi za Ulaya  Magharibi na Mataifa mengine. Wajumbe  hawa huchaguliwa na Baraza Kuu la Uchumi la Umoja wa Mataifa ( ECOSOC).
Bi. Samira Diria,  Afisa kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa KImataifa,  na Bi. Esther Suvi kutoka Kamisheni ya Mipango, ambao ni sehemu ya Ujumbe wa Tanzania  katika Mkutano wa 48 wa Kamisheni  kuhusu Idadi ya  watu na maendeleo wakifuatilia majadiliano ya jumla


Na Mwandishi Maalum, New York

Mkutano wa  48 wa Kamisheni kuhusu idadi  ya watu na maendeleo  (CPD) unaendelea hapa Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa, ambapo   wajumbe  kutoka nchi 47 zinazounda  Kamisheni hiyo  wamekuwa wakibadilishana  mawazo, uzoefu na  namna ya kukabiliana na changamoto mbalimbali  kuhusu dhima nzima ya idadi ya watu  na maedeleo

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni  kati ya nchi 47 zinazounda Kamisheni  hiyo ikiwa   miongoni mwa  nchi 12  zinazoiwakilisha Bara la  Afrika,  wajumbe wa Kamisheni hiyo wanachaguliwa kikanda,  ambapo Afrika inawajumbe 12,  Asia na Pacific ikiwakilishwa na nchi 11,  Bara la Ulaya likiwakilishwa na  nchi 5,  Bara la Amerika na Visiwa vya Karibian  likiwakilishwa na  nchi 9  wakati kundi la nchi za  Ulaya Magharibi na Mataifa mengine  likiwakilishwa na  nchi 10.

Majadiliano ya jumla ya  mkutano huu wa 48 yamejielekeza zaidi  katika   kuelezea uzoefu wa kila nchi katika eneo hilo la idadi ya watu na maendeleo mkazo ukiwa  namna gani  masuala ya  idadi ya watu  na maendeleo yanavyoweza kuingizwa katika  suala zima la  maendeleo endelevu hususani  baada ya  mwaka 2015.

Ujumbe wa Tanzania katika Mkutabo huu  unawahusisha wawakilishi kutoka Wizara ya Afya,   kamisheni  ya Mipango, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, na Asasi isiyo ya Kiserikali inayohusiana na  masuala ya Vijana.


Pamoja na kubadilishana uzoefu wa kitaifa kuhusu  masuala ya idadi ya watu na maendeleo na namna gani nchi wanachama  zinavyotekeleza mipango mbalimbali ya maendeleo, wajumbe wa mkutano huu pia wamepata fursa ya  kupata taarifa za  kitaalamu kutoka  kwa wasomi na watafiti waliobobea katika  maeneo ya idadi ya watu, maendeleo,  ajira,  takwimu, mazingira na  mabadiliko ya tabia nchi pamoja na  mambo mengine.

Akizungumza wakati wa majadilino ya jumla,  Naibu Mwakilishi wa  Kudumu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Katika Umoja wa Mataifa, Balozi Ramadhan Mwinyi, amesema,  masuala ya idadi ya watu na maendeleo ni moja ya ajenda muhimu kwa Tanzania na kwamba  Tanzania iko katika mchakato wa kufanya marejeo ya  sera ya taifa ya idadi ya watu kwa lengo la kuimarisha mifumo ya takwimu.

Vile vile  amesema  katika kipindi cha mpito  baada ya 2015 ambao ndio  mwisho wa utekelezaji wa malengo ya maendeleo ya millennia,  ni kipindi  kinachokwenda sambamba na  muhula wa pili wa mpango wa miaka mitano wa maendeleo ambapo unalenga katika  mkakati wa kuifanya Tanzania kuwa nchi yenye uchumi wa kati kupitia visheni 2025.

Akabainisha kuwa ili kufikia azma hiyo,  serikali  imejipanga kushirikiana na wadau  kutoka sekta mbalimbali   yakiwamo mashirika yasiyo ya kiserikali.

Uwezeshwaji wa  wanawake ni moja ya eneo ambalo Tanzania imeelezea kama  moja ya vipaumbele vyake katika  suala zima la idadi ya watu na maendeleo. Pamoja na  changamoto ya kukabili tatizo la ajira kwa vijana .

Na kwa  sababu hiyo,  Balozi Radhani Mwinyi asema, Serikali imejiwekea mikakati na mipango inayolenga katika  kuwawezesha wanawake na vijana kiuchumi.

Kwa upande wa eneo la huduma za afya,  amesema serikali imejiwekea mipango na  mikakati inayolenga katika  kusambaza huduma za afya  kwa wananchi wake, zikiwamo afya ya uzazi, upunguzaji wa vifo vya watoto wachanga na wanawake wajawazito, elimu ya jumla kuhusu masuala ya uzazi na haki za  binadamu.

Tanzania  katika mchango wake  imesisitiza umuhimu wa ushirikiano wa kikanda  kwa madhmuni ya kubadilishana, kuhabarishana na  kuelimishana pamoja na  kubadilishana uzoefu kuhus masuala mtambuka yakiwano  ya maendeleo endelevu na uhusiano wake na idadi ya watu

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.