Na,
Himid Choko, BLW.
WAJUMBE
wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, wanatarajiwa kuaza kuchambua Bajeti ya
Serikali na ile ya kila wizara kwa mwaka
wa Fedha 2015/2016 kuanzia Alkhamis ijayo.
Akizungumza na
mwandishi wa habari hizi huko Afisini kwake Chukwani nnje Kidogo ya Mji wa
Zanzibar, Katibu wa Baraza la Wawakilishi
Zanzibar, Yahya Khamis Hamad amesema maandalizi yote kwa ajili ya
shughuli hiyo tayari yamekamilika.
Amesema shughuli zote
za kupitia Bajeti hizo
zitafanyika katika Afisi ya Baraza la Wawakilishi Chukwani, na zitaanza kwa
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Ikulu na Utawala Bora kuwasilisha Mpango wa
Maendeleo wa Mwaka 2015/2016 na baadae Waziri wa Fedha kuwasilisha Bajeti ya Serikali ya Mapinduzi
ya Zanzibar 2015/2016 mbele ya Kamati ya
Wenyeviti ya Baraza la Wawakilishi, siku ya Alkhamis ya Tarehe 30/5/2015.
Katibu Yahya
amefafanua kwamba Kamati hiyo ya Wenyeviti inaundwa na Wenyeviti wa Kamati
zote saba za Kudumu za Baraza la
Wawakilishi na itajadili Bajeti hiyo siku ya
Jumamosi ya tarehe 02/05/2015 na Jumapili ya tarehe
03/05/2015 na hatimae bajeti hiyo itawasilishwa
katika Baraza zima la Wawakilishi Jumatano ya tarehe 13/05/2015.
Aidha amesema kwa upande wa Bajeti za Kisekta, Kamati za
kudumu zitaanza kujadili Bajeti za Wizara zinazozisimamia kuanzia Jumatatu ya
tarehe 04/05/2015 hadi Alkhamis ya tarehe 07/05/2015 na baadae zitawasilishwa katika Baraza zima
wakati wa Mkutano wa Bajeti.
Katibu huyo wa Baraza la Wawakilishi amezidi kufafanua kwamba, Utaratibu wa
kuwasilisha, kujadili, na kupitisha bajeti
ya serikali kwenye Baraza la Wawakilishi la Zanzibar umewekwa kwenye
Katiba ya Zanzibar ya 1984 na umefafanuliwa kwa upana zaidi kwenye Kanuni za
Baraza la Wawakilishi, Toleo la 2012.
“Makadirio
ya jumla ya Bajeti ya Serikali kwanza hupelekwa kwenye Kamati ya Wenyeviti wa
Kamati za Kudumu za Baraza la Wawakilishi kwa mujibu wa Kanuni ya 95 (1)
(Kanuni za Baraza la Wawakilishi, Toleo la 2012) na baadae ndipo huwasilishwa
kwenye Baraza’’ Alisema Katibu Yahya.
Yahya
aliendelea kusema kwamba “Mapendekezo ya bajeti ya kila Wizara kwanza hupelekwa
kwenye Kamati husika ya kisekta kwa
mujibu wa Kanuni ya 96 (1) na baada ya Kamati
husika kumaliza kazi ya kushughulikia mapendekezo hayo ndipo huwasilishwa
kwenye Baraza na Waziri mwenye dhamana ya Wizara husika au Kaimu wake.”
Amesema
bajeti ni nyenzo muhimu na muhimili wa maendeleo na ustawi wa jamii hivyo amewaomba wananchi kufuatilia mchakato
wa Bajeti kwenye Baraza na kushirikiana
ipasavyo na Wawakilishi wao na
wahakikishe kwamba bajeti inaakisi
maisha yao ya kila siku kulingana
na wakati uliopo.
Aidha amesema hivi sasa ni wakati muwafaka wa wananchi
kuwatosheleza wawakilishi wao pamoja na Wajumbe wenyewe kufanya utafiti ili hatimae kuhakikisha
kwamba maudhui ya mijadala ya shughuli za kila Wizara yanalenge juu ya Sera na Sheria za Fedha, Utawala na Utendaji bora wa shughuli za
Umma.
“Pamoja na kuzingatia hizo sera na masuala ya Malengo ya
Milenium Mijadala yao pia inatakiwa ijikite katika kuwasilisha maoni na
mitizamo ya wananchi pamoja
na kero zinazowakabili katika kutathmini
vipaumbele vya Bajeti hiyo ” alisema
Katibu Yahya.
Mkutano ujao wa Baraza la Wawakilishi ambao utajadili
Bajeti, unategemewa kuanza Jumatano ya
tarehe 13/05/2015 na kuchukua takriban mwezi
mmoja na nusu.
MWISHO.
Imetolewa na.
Himid CHOKO,
O777436016
BLW,
zanzibar,
28/04/2015.
No comments:
Post a Comment