1.
Mheshimiwa Spika, kama ilivyo ada kwetu sisi waumini, naomba nianze kwa kumshukuru Mwenyenzi
Mungu muumba wa mbingu na ardhi kwa kutujaalia neema ya uhai na afya
zilizotuwezesha kukutana hapa. Baada ya kumshukuru Mwenyezi Mungu, naomba sasa
kutoa hoja kwamba, Baraza lako tukufu likae kama Kamati ya kujadili na hatimae
kuidhinisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar kwa mwaka wa fedha 2015/16, ili kutimiza matakwa ya Katiba ya Zanzibar
ya mwaka 1984 kama ilivyorekebishwa.
2.
Mheshimiwa Spika, leo asubuhi Mheshimiwa Dr Mwinyihaji Makame Mwadini Waziri wa Nchi (AR)
Ikulu na Utawala Bora amewasilisha mbele ya Baraza hili Taarifa ya Mwenendo na
Hali ya Uchumi wa Zanzibar, Utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa mwaka 2014/15
kwa kipindi cha miezi tisa hadi Machi mwaka 2015 na Mpango wa Maendeleo kwa
mwaka 2015/16. Makadirio ya mapato na matumizi ninayowasilisha yanakamilisha
mustakabali wetu kiuchumi, kimaendeleo na kifedha kwa upande wa mapato na
matumizi kwa mwaka wa fedha 2015/16.
3.
Mheshimiwa Spika, Naomba Hotuba hii, isomwe sambamba na Rasimu ya Mapendekezo ya Mapato
na Matumizi na kuingizwa kwenye kumbukumbu za Baraza.
4.
Mheshimiwa Spika, naomba pia nitumie fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Dr. Ali Mohamed
Shein, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kwa kumaliza mwaka
mwengine wa uongozi wake kwa nchi yetu. Tumeshuhudia katika mwaka huu kwa mara
nyengine tena, uongozi wake ulio bora, imara na wa uadilifu mkubwa. Nawapongeza
pia wasaidizi wake wakuu, Mheshimiwa Maalim Seif Shariff Hamad, Makamo wa Kwanza
wa Rais na Mheshimiwa Balozi Seif Ali Iddi, Makamo wa Pili wa Rais, kwa ushauri
na msaada wao kwa Mheshimiwa Rais. Sina budi pia kumshukuru sana Mheshimiwa
Rais kwa kuendelea kuniamini na kunikabidhi jukumu la kuiongoza Wizara ya
Fedha, wizara ambayo ina umuhimu wa kipekee kwa maendeleo ya nchi yetu.
Nawashukuru viongozi hawa wote kwa miongozo yao ya kila mara inayonirahisishia
utekelezaji wa majukumu yangu.
5.
Mheshimiwa Spika, kwa mara nyengine tena naomba nimkumbuke mwenzetu ambae tumekuwa nae
katika hotuba zote za Bajeti kwa miaka minne iliyopita na kupata mchango wake
adhimu lakini mara hii hatunae tena. Ninamuomba tena Mwenyezi Mungu, Subhana
Wataala, kumpa malazi mema mpenzi wetu, ndugu yetu na mwenzetu, Marehemu Salmin
Awadh Salmin alietangulia mbele ya haki tarehe 19 Februari 2015. Ninamuomba pia
amlipe vyema kwa mchango wake mkubwa alioutoa kwa maendeleo ya wanajamii
wenzake na ajaalie mchango huo uwe sadaka yake inayoendelea.
6.
Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo hayo ya utangulizi, naomba sasa nianze kwa kuzungumzia
kwa ufupi hali ya uchumi wetu.
B. MWENENDO WA UCHUMI WA ZANZIBAR
7.
Mheshimiwa
Spika; kama nilivyosema awali, tayari asubuhi ya leo tumewasilishiwa matokeo ya
mwenendo wa uchumi wetu kwa mwaka 2014 na mataraijio kwa mwaka 2015. Taarifa
hiyo imeeleza kuwa Uchumi wa Zanzibar umeendelea kukua kwa kiwango kizuri
pamoja na kuendelea kuwepo kwa utulivu wa bei za bidhaa na huduma.
8.
Mheshimiwa Spika, Kwa mwaka 2014 taarifa imeonesha kuwa uchumi wetu umekuwa kwa asilimia 7.0
ikionesha kupungua kidogo kwa kasi yake ikilinganishwa na ukuaji wa asilimia
7.2 kwa mwaka 2013. Kwa mafanikio hayo, wastani
wa Pato la Taifa la kila mtu limeongezeka na sasa limefikia TZS 1,552,000 sawa
na Dola za Kimarekani 939 mwaka 2014 kutoka TZS 1,384,000 sawa na Dola za Kimarekani
866 kwa mwaka 2013.
9.
Mheshimiwa Spika, kimuundo, uchumi wetu umeendelea kuchangiwa zaidi na Sekta ya Huduma
ikifuatiwa na Kilimo. Kwa mwaka 2014, Sekta ya Huduma ilichangia asilimia 44.7,
ikionesha kupanda kwa mchango wake kutoka asilimia 41.5 wa mwaka 2013. Hali hii
imetokana na kuimarika kwa Sekta ndogo za Habari na Mawasiliano; Fedha; na
Taaluma, Ufundi na Sayansi. Mchango wa sekta ya Kilimo kwa mwaka 2014 umepungua
na kufikia asilimia 27.9 kutoka asilimia
30.4 mwaka 2013 kutokana na kupungua kwa uzalishaji wa mpunga na mazao mengine
ya chakula pamoja na kupungua kwa uzalishaji wa mazao ya biashara, hasa
karafuu. Halikadhalika, mafanikio mazuri
ya Sekta ya Huduma yameshusha pia mchango wa Sekta ya Viwanda kutoka asilimia
18.0 mwaka 2013 hadi kufikia asilimia 16.8 mwaka 2014. Hali hii imetokana na
kushuka kwa mchango wa Sekta ndogo za Uzalishaji Viwandani, Ujenzi na Umeme na
Gesi.
10.
Mheshimiwa Spika, kwa upande wa sekta ya Nje kwa mwaka 2014, mwenendo wa biashara na nchi
za nje umezidi kuimarika kutokana na kuongezeka kwa thamani ya usafirishaji wa
bidhaa na huduma. Thamani ya
usafirishaji wa bidhaa nje ya nchi iliongezeka kutoka TZS 87.6 bilioni mwaka
2013 kufikia thamani ya TZS 133.6 bilioni mwaka 2014. Ongezeko hili limetokana
na kuongezeka kwa usafirishaji wa mazao ya biashara ya karafuu na mwani kutoka
TZS 75.4 bilioni mwaka 2013 hadi 104.0 bilioni mwaka 2014. Kwa upande wa thamani ya uagiziaji wa bidhaa
kutoka nje, kumekuwa na ongezeko la asilimia 34.4 kutoka TZS 208.1 bilioni
mwaka 2013 hadi kufikia thamani ya TZS 279.6 bilioni mwaka 2014, ambapo
uagiziaji mkubwa ulionekana katika vyombo vya usafiri na mashine. Hali hii
imepelekea kupanuka kwa urari wetu wa biashara za nje kwa kuongezeka nakisi
kutoka TZS 120.5 bilioni mwaka 2013 hadi TZS 146.0 bilioni mwaka 2014.
11.
Mheshimiwa Spika, kwa upande wa utulivu wa bei, mwaka wa 2014 tumeendelea kuwa na mfumko
wa bei ulio katika tarakimu moja. Hata hivyo, kiwango chake kimepanda kidogo
kutoka wastani wa asilimia 5.0 mwaka 2013 hadi asilimia 5.6 kwa mwaka 2014, kama
ilivyoelezwa kwa undani zaidi katika Mapitio ya hali ya Uchumi leo asubuhi.
12.
Mheshimiwa Spika, Katika kipindi cha miaka mitano (2010 hadi 2014), Pato la Taifa kwa bei
za miaka husika limekua kutoka TZS 1,050.8 bilioni hadi kufikia TZS 2,133.5 bilioni.
Kwa bei za kudumu, Pato la Taifa limekua kutoka TZS 848.2 bilioni hadi kufikia
TZS 1,115.4 bilioni sawa na ukuaji wa asilimia 31.5 kwa kipindi hicho sawa na wastani
wa ukuaji wa asilimia 6.3 kwa mwaka. Pato la Taifa kwa bei za miaka husika kwa
mtu mmoja limekua kutoka TZS 856,000 ($613) mwaka 2010 hadi kufikia TZS
1,552,000 ($939) kwa mwaka 2014.
13.
Mheshimiwa
Spika; Katika kipindi cha mwaka 2010/11 hadi 2014/15, mapato ya ndani
yameongezeka kutoka TZS 181.4 bilioni hadi kufikia TZS 360.4 bilioni 2014/15,
sawa na ukuaji wa asilimia 98.7 kwa kipindi hicho au wastani wa asilimia 19.7
kwa kila mwaka.
C. UTEKELEZAJI WA BAJETI
14.
Mheshimiwa Spika, itakumbukwa kuwa Serikali kwa mwaka wa fedha wa 2014/15 ilipanga
kukusanya TZS 707.8 bilioni. Kati ya fedha hizo TZS 386.8 bilioni ni kutoka
vianzio vya ndani, ambapo ZRB ilitarajiwa kukusanya TZS 181.5 bilioni na TRA
ilitarajiwa kukusanya TZS 166.0 bilioni. Mapato yaliyotarajiwa kukusanywa
kutokana na vianzio visivyokuwa vya kodi (mapato ya mawizara) ni TZS 18.4
bilioni na kodi ya mapato ya wafanyakazi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
wanaofanya kazi Zanzibar (PAYE) ni TZS 21 bilioni. Aidha, mapato yaliyotarajiwa
kutoka nje ni TZS 306.0 bilioni zikiwemo TZS 40.0 bilioni kutokana na Misaada
ya Kibajeti (GBS), TZS 66.3 bilioni kama ruzuku na TZS 199.1 bilioni ni mikopo
kwa ajili ya miradi ya maendeleo ambapo fedha kutokana na misamaha ya madeni ni
TZS 0.6 bilioni. Serikali ilipanga kuchukua
mikopo ya ndani ya muda mrefu ili kuziba nakisi ya TZS 15 bilioni.
Mheshimiwa Spika, Kwa upande wa matumizi, Serikali ilipanga kutumia kiasi hicho cha TZS
707.8 bilioni, ambapo kazi za kawaida zilipangiwa
kutumia TZS 376.5 bilioni wakati kazi za maendeleo zilitengewa TZS 331.3
bilioni. Kati ya fedha hizo za maendeleo, TZS 65.9 bilioni ni mchango wa Serikali
na zilizosalia ni kutoka kwa mashirika ya Kimataifa na Washirika wa Maendeleo.
Ukusanyaji halisi wa mapato ya ndani
16.
Mheshimiwa Spika, Hadi kufikia mwezi Machi 2015, Serikali ilitarajia kukusanya jumla ya
TZS 298.7 bilioni. Hata hivyo, jumla ya TZS 275.0 bilioni zimeweza kukusanywa ikiwa
ni sawa na asilimia 92.1 ya lengo la kipindi cha miezi tisa. Pamoja na
kutofikiwa lengo la ukusanyaji wa mapato, kiwango hicho cha utendaji
kinamaanisha ongezeko la mapato ya TZS 27.7 bilioni sawa na asilimia 10 ikilinganishwa
na TZS 247.3 bilioni zilizokusanywa kipindi kama hiki cha miezi tisa mwaka 2013/14.
Mapato ya Kodi
17.
Mheshimiwa Spika, Kwa kipindi cha miezi tisa hadi kufikia Machi 2015, mapato ya kodi
yamefikia TZS 242.5 bilioni sawa na asilimia 91 ya lengo la TZS 266.4 bilioni. Kati
ya mapato yaliyokusanywa, ZRB imeweza kukusanya jumla ya mapato ya kodi ya TZS 135.7 bilioni ikiwa ni
sawa na asilimia 95 ya makadirio ya miezi tisa na TRA imekusanya jumla ya TZS 106.8
bilioni sawa na asilimia 86 ya makadirio ya miezi tisa.
Mapato yasiyo ya Kodi
18.
Mheshimiwa Spika, Kwa upande wa makusanyo ya mapato yasiyokuwa ya kodi, jumla ya TZS 16.7
bilioni zimekusanywa sawa na asilimia 91 ya makadirio ya mwaka. Makusanyo hayo
yanajumuisha mapato ya mawizara ya TZS 12.8 bilioni pamoja na gawio la faida
kutoka Benki kuu ya Tanzania TZS 3.2 bilioni na Mashirika ya Serikali ya TZS
0.7 bilioni.
Mikopo ya Ndani
19.
Mheshimiwa Spika, Hadi kufikia mwezi wa Machi 2015, Serikali imekopa ndani jumla ya TZS
10.1 bilioni sawa na asilimia 67 ya makadirio ya mwaka 2014/15 ukilinganisha na
TZS 20.0 bilioni zilizokopwa katika kipindi kama hicho mwaka 2013/14.
Matarajio ya mapato hadi Juni 2015
20. Mheshimiwa
Spika, Matarajio ya makusanyo hadi kufikia
Juni 2015 ni TZS 375.4 bilioni sawa na asilimia 93 ya makadirio ya mapato kwa
mwaka wa fedha 2014/15. Kati ya Mapato hayo, TZS 360.1 bilioni ni mapato ya
kodi na yasiyo ya kodi na TZS 15.0 bilioni ni mikopo ya ndani. Inatarajiwa
kwamba ZRB itakusanya TZS 179.2 bilioni, TRA jumla ya TZS 140.7 bilioni, mapato
yasiyokuwa ya kodi TZS 19.5 bilioni, PAYE kutoka SMT ni TZS 21.0 bilioni.
Matumizi halisi
21.
Mheshimiwa Spika, Katika kipindi cha miezi tisa hadi Machi 2015, Serikali imetumia jumla
ya TZS 369.7 bilioni, ikiwa ni sawa na asilimia 52 ya malengo ya mwaka. Kati ya
matumizi hayo, jumla ya TZS 261.2 bilioni zimetumika kwa ajili ya kazi za
kawaida, sawa na asilimia 96 ya matarajio ya TZS 271.5 bilioni kwa kipindi
hicho. Uchambuzi wa matumizi hayo ni kama hivi ifuatavyo:
a)
Mishahara ni
TZS 136.0 bilioni, sawa na asilimia 74 ya makadirio ya mwaka.
b)
Matumizi
mengineo ni TZS 44.0 bilioni, sawa na asilimia 61 ya makadirio ya mwaka.
c)
Mfuko Mkuu
wa Serikali ni TZS 48.4 bilioni, sawa na asilimia 69.3 ya makadirio ya mwaka,
na
d)
Ruzuku ni
TZS 32.8 bilioni sawa na asilimia 65 ya makadirio ya mwaka.
22.
Mheshimiwa Spika, Kwa upande wa matumizi katika shughuli za maendeleo, katika kipindi cha
miezi tisa, Serikali imetumia jumla ya TZS 108.5 bilioni kwa ajili ya kazi za
maendeleo ikiwa ni sawa na asilimia 32.7 ya lengo la mwaka. Kati ya fedha hizo,
Washirika wa Maendeleo wametoa TZS 69.4 bilioni sawa na asilimia 26 ya
makadirio ya mwaka, (TZS 48.9 bilioni ni Ruzuku na TZS 20.5 bilioni ni Mikopo).
Mchango wa Serikali kwa ajili ya Miradi ya Maendeleo ulifikia TZS 39.1 bilioni
sawa na asilimia 59 ya lengo la mwaka. Upatikanaji mdogo wa fedha za Washirika wa
Maendeleo umetokana na changamoto zilizojitokeza katika utekelezaji wa baadhi
ya miradi kama vile ujenzi wa jengo jipya la abiria katika uwanja wa ndege wa
Abeid Amani Karume, ujenzi wa barabara za kati, Unguja na Mradi wa Huduma za
Mijini (ZUSP).
Deni la Taifa
23.
Mheshimiwa Spika, Deni la Taifa mpaka kufikia mwezi wa Machi 2015 limeongezeka hadi kufikia
TZS 317.2 bilioni, sawa na ukuaji wa asilimia 7.6 ukilinganisha na deni
lililokuwepo mwezi wa Machi 2014 la TZS 294.9 bilioni. Deni la Nje limefikia TZS
218 bilioni mpaka kufikia mwezi wa Machi 2015 ikilinganishwa na TZS 211.8 bilioni
kufikia mwezi wa Machi 2014. Kati ya jumla ya madeni ya nje, asilimia 88
ilidhaminiwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (SMT) na asilimia12
ilidhaminiwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ). Deni la ndani hadi
mwezi wa Machi 2015 liliongezeka hadi kufikia TZS 99.3 bilioni ikilinganishwa
na mwezi wa Machi 2014 la TZS 83.1 bilioni. Hali hii imetokana na kuongezeka
kwa deni la kiinua mgongo, deni la ZSSF na Hati Fungani kutoka Benki Kuu ya
Tanzania (BOT).
D. UTEKELEZAJI WA HATUA ZA KUIMARISHA
MAPATO 2014/15
24.
Mheshimiwa Spika, kwa mwaka wa fedha 2014/15, Serikali ilichukua hatua mbalimbali za
kuimarisha mapato yake. Utekelezaji wa hatua hizo ni kama ifuatavyo:
I.
Kuimarisha usimamizi wa kimaeneo (Block Management
System)
(i)
ZRB kwa kushirikiana
na TRA na Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali imefanya mgawanyo wa maeneo kwa
kutumia Teknohama (GPS) ili kupata taarifa za wafanyabiashara na maeneo walipo.
Mpaka kufikia Machi 2015 Jumla ya wafanyabiashara wapya 830 tayari wamesajiliwa
kulipa kodi kupitia utaratibu huu.
(ii)
Kuzitambua na kuzichukulia hatua nyumba zote
zinazotumiwa kulaza wageni ambazo hazijasajiliwa kulipa kodi: Katika zoezi la kuimarisha usimamizi wa kimaeneo,
nyumba 12 katika maeneo ya ukanda wa mashariki na Nungwi zimetambuliwa na
hatimae kusajiliwa kwenye mtandao wa kulipa kodi.
(iii)
Kuanzishwa kwa utaratibu wa zuio katika ushuru wa
stemp kutokana na mafanikio yaliyopatikana katika VAT: Tayari Kanuni zimekamilishwa na kusainiwa na
Waziri wa Fedha. Hatua za kuzitangaza katika Gazeti rasmi la Serikali
zinaendelea.
(iv)
Kuimarisha ukaguzi na upelelezi kwa walipakodi
katika maeneo ya mawasiliano, utalii na nishati ya mafuta: Watendaji 3 wa ZRB wamepatiwa mafunzo na TRA
(Tanzania Bara) juu ya upelelezi wa walipakodi na watendaji 23 wamepatiwa
mafunzo ya msingi ya ukaguzi katika sekta ya Utalii kupitia msaada wa Wizara ya
Fedha ya Marekani (US Treasury) na Shirika la Maendeleo la Japan (JICA).
(v)
Katika Kuimarisha matumizi ya Teknohama na usimamizi
(supervision) kati ya ZRB na TRA:
Kwa upande wa ZRB, Mtandao wa “Zanzibar Integrated Tax Administration System”
(ZITAS) umeimarishwa na tayari unatoa huduma za kielektroniki kama
ulivyokusudiwa. Idara ya Forodha imeendelea na matayarisho ya kutumia mfumo wa Tanzania Customs Information System (TANCIS)
badala ya ASYCUDA ++ na Idara ya Kodi za Ndani ya TRA nayo inatumia mfumo wa Integrated Tax (ITAX). Kwa sasa TRA na
ZRB zinaendelea na mchakato wa kupitia mifumo yao na kuihakiki ili kuweza kuifanya iweze kuwasiliana (interface).
1.
Kuimarisha Uthamini wa Forodha
25.
Mheshimiwa Spika, Eneo jengine lililoangaliwa na Serikali kwa hatua za kiutawala ni
uimarishaji wa uthamini wa bidhaa zinazoingizwa nchini (Valuation) kutokana na
kuwepo kwa baadhi ya wafanyabiashara wasio waaminifu ambao hufanya udanganyifu,
ukiwemo kushusha kiwango na thamani halisi ya bidhaa husika. Idara ya Forodha
TRA inaendelea kukabiliana na tatizo hili ambapo imeanzisha database maalum kwa
bidhaa zinazoingizwa mara kwa mara hapa Zanzibar. Kwa sasa, utiaji thamani wa
bidhaa unazingatia thamani zilizomo katika database hiyo.
Mapato yasiyokuwa ya kodi
2.
Gawio kutoka kwa Mashirika ya Serikali
26.
Mheshimiwa Spika, Serikali iliongeza kiwango cha gawio kutoka asilimia 10 hadi 20 kuanzia
mwaka wa fedha 2014/2015 kwa mashirika yanayomilikiwa na Serikali. Hadi kufikia
mwisho wa Machi 2015, jumla ya TZS 727 milioni zimekusanywa kama Gawio la faida
iliyopatikana na mashirika hayo.
3.
Kupunguza kiwango cha ushuru wa Mirathi
27.
Mheshimiwa Spika, Kwa mwaka wa fedha 2014/15, Serikali ilipunguza kiwango cha ushuru wa
mirathi kutoka asilimia 5 hadi asilimia 0.25, Lengo ni kusajili mali na
kupatikana kwa nyaraka halali za umiliki, ambazo zitawezesha kutumika katika
shughuli mbali mbali za kiuchumi na kupunguza matatizo ya kijamii katika
mirathi. Hatua zimechukuliwa pamoja na kufanyiwa marekebisho Kanuni ya Ushuru
wa Mirathi (Estate Duty), ambapo utekelezaji wake umeanza rasmi mwezi Februari
2015. Hadi kufikia Machi 2015, jumla ya TZS 4.2 milioni zimekusanywa.
Marekebisho ya Sheria za kodi
4.
Sheria ya Usimamizi wa kodi namba 7 ya mwaka 2009.
28. Mheshimiwa
Spika, Serikali ilifanya mabadiliko ya Sheria
ya Usimamizi wa kodi TAPA kwa kubadilisha tarehe ya kuwasilisha ritani na
kufanya malipo, ambapo awali tarehe ya kuwasilisha ritani ni tarehe 15 na
kufanya malipo tarehe 25. Marekebisho ya sasa ni kuwasilisha ritani tarehe 7 na
malipo ni tarehe 15. Marekebisho haya yamesaidia kuiwezesha Serikali kupata
mapato yake mapema zaidi na kuweza kuimarisha utoaji wa huduma kwa wananchi.
5.
Sheria ya Ada za Bandari namba 2 ya mwaka 1999
29.
Mheshimiwa Spika, Baraza liliidhinisha pia marekebisho ya Sheria ya Ada ya Bandari kwa kuongeza
Ada ya Usalama wa Uwanja wa Ndege kwa abiria anaesafiri ndani ya Tanzania kutoka
kiwango cha malipo kwa abiria wa ndani cha TZS 1,000 hadi TZS 3,000. Jumla ya TZS 2.07 bilioni zimekusanywa hadi
kufikia Machi 2015.
6.
Sheria ya Usafiri wa Barabara Namba 7 ya mwaka 2003.
30.
Mheshimiwa Spika, Baraza lako liliridhia kubadilisha muda wa utoaji wa leseni za udereva
na malipo ya leseni hizo. Chini ya marekebisho hayo, tayari leseni zinatolewa
kwa muda wa miaka miwili, mitatu na mitano na viwango vya malipo kwa leseni ni
TZS 35,000, TZS 45,000 na TZS 60,000 kwa lengo la kupunguza usumbufu kwa
madereva kulazimika kurudi kila mwaka kuhuisha leseni. Jumla ya TZS 979.1
milioni zimekusanywa katika kipindi cha miezi tisa sawa na ongezeko la asilimia
59.7 au TZS 366 milioni.
7.
Kupunguza Misamaha ya kodi
31.
Mheshimiwa Spika, Baraza pia lilikubali pendekezo la Serikali la kupunguza misamaha ya
kodi kwa wawekezaji kutoka asilimia 80 hadi asilimia 75 kwa uingizaji wa vifaa
vya uwekezaji nchini. Kutokana na mabadiliko hayo, tokea mwezi Julai 2014 wawekezaji
hulipa asilimia 25 ya kodi yote ya vifaa vilivyosamehewa kodi.
32.
Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo hayo kuhusu utekelezaji wa hatua za kuimarisha mapato
kwa mwaka 2014/15, naomba sasa nitoe mwelekeo wa Bajeti ya mwaka 2015/16.
E. MWELEKEO WA BAJETI 2015/16
Malengo Makuu ya Serikali
33.
Mheshimiwa Spika, Kwa mwaka wa Fedha wa 2015/16, Bajeti itaendelea kuzingatia malengo
makuu ya Serikali. Malengo hayo ni Kujenga jamii: (i) Iliyo elimika kwa Elimu bora na inayotoa wataalamu wenye hadhi ya
kimataifa; (ii) Yenye siha; (iii) Iliyoimarika kiuchumi; na (iv) Inayojali
umoja wa kitaifa na kufuata misingi ya utawala bora. Mambo haya ndio
yanayojenga falsafa iliyomo katika Dira ya Maendeleo ya 2020 ambayo
inatekelezwa kwa sasa kupitia MKUZA II na Mpango wake wa utekelezaji. Utendaji
wa Sekta zote umejielekeza katika kufikiwa kwa malengo hayo makuu.
F. MAKADIRIO YA MAPATO KWA 2015/2016
34.
Mheshimiwa Spika, Serikali imekadiria kukusanya jumla ya TZS 830.4 bilioni ambapo mapato
ya ndani yanatarajiwa kufikia TZS 450.5 bilioni na mapato ya nje kwa miradi ya
maendeleo ni TZS 347.1 bilioni. Aidha, fedha kutokana na msamaha wa madeni
yanatarajiwa kufikia TZS 1.3 bilioni na Mfuko wa Wafadhili ni TZS 1.5 bilioni.
Mikopo ya ndani inatarajiwa kufikia TZS 30.0 bilioni.
Makadirio ya Mapato ya Ndani
35.
Mheshimiwa Spika, kwa mwaka wa fedha 2015/16, Serikali inatarajia kukusanya jumla ya
mapato ya ndani ya TZS 450.5 bilioni sawa na ongezeko la asilimia 25 ya
matarajio ya mapato ya mwaka 2014/15 ya TZS 360.4 bilioni.
Mapato ya Kodi
36.
Mheshimiwa Spika, jumla ya TZS 404.5 bilioni zinatarajiwa kukusanywa kutokana na mapato
ya kodi mbalimbali. Mapato haya yanahusisha hatua mpya za mapato
zinazopendekezwa kutekelezwa kwa mwaka ujao wa fedha ambazo nitaziwasilisha
baadae. Kati ya kiasi hicho cha mapato, TRA inatarajiwa kukusanya TZS 178.6
bilioni sawa na ongezeko la asilimia 27 ya kiasi kinachotarajiwa kukusanywa
hadi Juni 2015 wakati ZRB inatarajiwa kukusanya jumla ya TZS 225.9 bilioni,
sawa na ongezeko la asilimia 26 ya matarajio
ya makusanyo ya mwaka 2014/15.
Kodi ya PAYE kutoka Tanzania Bara
37.
Mheshimiwa Spika, Jumla ya TZS 21.0 bilioni zinakadiriwa kukusanywa kutokana na mishahara
ya wafanyakazi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wanaofanya kazi Zanzibar.
Mapato yasio ya Kodi
38.
Mheshimiwa Spika, mapato yasiyokuwa ya kodi yanatarajiwa kufikia TZS 25 bilioni, yakimaanisha
ongezeko la asilimia 28 kutoka jumla ya TZS 19.5 bilioni zinazotarajiwa kukusanywa
hadi Juni 2015.
Mikopo ya Ndani
39.
Mheshimiwa Spika, kama nitakavyobainisha baadae, Serikali inategemea kukopa ndani TZS 30
bilioni kwa ajili ya kufidia nakisi iliyojitokeza katika bajeti ya mwaka
2015/16.
Mapato ya Nje (Ruzuku na Mikopo)
Misada ya Kibajeti
40.
Mheshimiwa Spika, Serikali imekuwa ikipokea Misaada ya Kibajeti (General Budget Support -
GBS) kutoka kwa Washirika wa maendeleo. Misaada hii imekuwa chachu muhimu
katika utekelezaji wa Bajeti yetu hususan katika kuimarisha uwezo wa Serikali kwenye
Miradi ya Maendeleo. Kwa bahati mbaya, kwa miaka kadhaa sasa kumekuwa na
changamoto kubwa ya upatikanaji wa GBS kutokana na sababu mbalimbali, miongoni
mwake ikiwa ni pamoja na hizi zifuatazo:
i.
Matatizo ya kifedha katika nchi za Washirika wenyewe;
ii.
Mwenendo wa kiuchumi ikiwemo mgogoro wa kifedha
duniani;
iii.
Masuala ya utawala bora nchini hasa tuhuma za rushwa
na matumizi mabaya ya fedha za umma.
41.
Mheshimiwa Spika, kadhia ya hivi karibuni iliyopelekea Washirika wa Maendeleo kuzuia
misaada ya GBS ni kashfa ya matumizi ya fedha katika Hesabu ya Escrow ya Tegeta
huko Tanzania Bara. Wafadhili wamezuia tena misaada ya GBS ili kuishinikiza Serikali
ya Jamhuri ya Muungano kuchukua hatua juu ya watu waliotuhumiwa kuhusika pamoja
na hatua nyengine za kuimarisha mfumo wa usimamizi. Pamoja na kwamba kashfa
zinazotokea Tanzania Bara hazikuihusu Zanzibar kwa namna yoyote ile, bado kuzuiwa
kwa GBS kumekuwa na athari kubwa kwa utekelezaji wa Bajeti ya Zanzibar.
42.
Mheshimiwa Spika, ili kuepusha athari kubwa kwa utekelezaji wa Bajeti, kuanzia mwaka wa
fedha wa 2015/16, imeamuliwa kutoingiza moja kwa moja makadirio ya GBS katika
Bajeti ya Serikali. Badala yake, utaratibu maalum umewekwa wa kuwezesha kupokea
na kutumia fedha hizo pindi zikipatikana.
Mikopo na Ruzuku kwa Miradi ya Maendeleo
43.
Mheshimiwa Spika, kwa mwaka wa fedha 2015/16, jumla ya TZS 347.1 bilioni zinatarajiwa
kupokelewa kutoka kwa Taasisi za Kimataifa na Washirika wa maendeleo kwa ajili
ya kutekeleza Programu na Miradi ya Maendeleo. Kiasi hicho kinaashiria kuongezeka
kwa Misaada kwa utekelezaji wa kazi za maendeleo kwa asilimia 48 kutoka TZS 127.9
bilioni zinazotarajiwa kupatikana hadi Juni 2015. Sababu kubwa ya ongezeko ni
ujenzi wa jengo la abiria katika uwanja wa ndege wa Abeid Aman Karume ambao
unatarajiwa kukamilika ndani ya mwaka ujao wa fedha. Sehemu kubwa ya fedha
zilizobakia kwa ujenzi huo zinatarajiwa kulipwa katika kipindi hicho. Kati ya
fedha zinazotarajiwa kwa mwaka 2015/16, Ruzuku ni TZS 98.2 bilioni na Mikopo ni
TZS 248.9 bilioni.
G. HATUA ZA KUIMARISHA MAPATO 2015/16
44.
Mheshimiwa Spika, kama nilivyotangulia kusema, Serikali inakusudia kuchukua hatua kadhaa
ili kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya ndani. Haja hii imetokana sio tu na
mwenendo usioridhisha wa Misaada ya Kibajeti (GBS) kama nilivyoelezea awali,
lakini pia dhamira ya Serikali ya kuharakisha maendeleo huku ikizidisha kasi ya
kupunguza utegemezi wa misaada. Kama ilivyo kawaida, ili kufikia lengo hilo,
kuna hatua za kiutawala na zile za kubadilisha Sheria zinapaswa kutekelezwa.
Hatua za Kiutawala
45. Mheshimiwa
Spika, Kwa upande wa hatua za kiutawala,
maeneo yatakayosimamiwa kwa karibu ni pamoja na haya yafuatayo:
1.
Upimaji wa Ardhi
46.
Mheshimiwa Spika, Moja ya misingi muhimu ya mfumo wa kodi ni kuwepo kwa usawa miongoni
mwa walipakodi. Imegundulika kuwa maeneo mengi ya kibiashara katika Mkoa wa
Mjini Magharibi hayajapimwa na hayalipiwi kodi ya Ardhi. Hali hii inakwenda
kinyume na matakwa ya mfumo bora wa kodi. Kwa mwaka wa fedha ujao, Serikali
kupitia Idara ya Ardhi kwa kushirikiana na taasisi za kodi, itaanza kuyapima
maeneo ya kibiashara ambayo hayajapimwa ili kuhami mapato yake na kuwa na mfumo
wa haki kwa walipakodi wote. Hatua hii inatarajiwa kuongeza mapato ya Serikali
ya jumla TZS 262 milioni.
2.
Bodi ya Kusimamia Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu.
47.
Mheshimiwa Spika, maeneo mengine ya kiutawala ni kutekeleza uanzishaji wa Bodi ya
kusimamia Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu nchini na kuanzisha matumizi ya
mashine maalum za kutolea risiti kwa njia ya elektroniki (Electronic Fiscal Devices
- EFDs). Matayarisho ya mambo haya tayari yamefikia hatua ya kuridhisha na
yanatarajiwa kuanza rasmi katika mwaka wa fedha 2015/16. Jumla ya TZS 6.0
bilioni zinatarajiwa kukusanywa kutokana na hatua hizo.
Mapato Yasiyokuwa ya Kodi
3.
Kufanya Mapitio ya Viwango vya Ada mbalimabli
zinazotozwa na Taasisi za Serikali.
48.
Mheshimiwa Spika, Imebainika kwamba mapato yanayokusanywa na taasisi mbalimbali za Serikali
bado yako chini sana, hali hii imekuwa ikisababishwa na viwango vya ada hizo
kuwa vya zamani na kutoendana na wakati. Serikali inakusudia kuvifanyia mapitio
viwango vya ada katika taasisi za Idara ya Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali; Wizara
ya Afya; Wizara ya Biashara, Viwanda na Masoko; na Ofisi ya Rais – Tawala za Mikoa na Idara
Maalum ili viendane na wakati bila ya kuathiri utoaji wa huduma hizo. Hatua hii
inatarajiwa kuongeza mapato ya jumla ya TZS 60 milioni.
Marekebisho ya Sheria za Kodi
4.
Kodi ya Miundombinu (Infrastructure Tax)
49.
Mheshimiwa Spika, Kwa sehemu kubwa uimarishaji wa miundombinu nchini umekuwa ukitegemea
mchango wa ruzuku kutoka Taasisi za fedha za kimataifa na Washirika wa Maendeleo.
Wakati bado kuna uhaba wa miundombinu muhimu, mwenendo wa Washirika wa Maendeleo
umekuwa hautabiriki na una muelekeo wa kupungua mwaka hadi mwaka. Serikali
inalazimika kubuni utaratibu maalum ili iweze kuwekeza zaidi katika eneo hili
muhimu. Kuanzia mwaka ujao wa Fedha, inapendekezwa kuanzisha Kodi maalum kwa ajili
ya miundombinu (Infrastructure Tax). Mapato yatakayopatikana kutokana na Kodi
hizo yatawekwa katika Mfuko maalum (Infrastructure Fund). Mapato hayo yatatokana
na mabadiliko ya kodi mbalimbali ambapo kwa mwaka wa fedha 2015/16, jumla ya TZS
25 bilioni zinatarajiwa kukusanywa. Asilimia 75 ya fedha zitakazopatikana
zitaelekezwa katika uimarishaji wa miundombinu muhimu na asilimia 25 iliyobakia
itatumika kwa ajili ya Mifuko mingine iliyoanzishwa chini ya Sheria mbali mbali.
Mgao wa fedha hizo za asilimia 25 kwa ajili ya Mifuko hiyo utaandaliwa
utaratibu maalum.
50.
Mheshimiwa Spika, kati ya TZS 25 bilioni, TZS 10 bilioni zinatarajiwa kukusanywa na TRA
kupitia Idara ya Forodha na TZS 15 bilioni zitakusanywa na ZRB kama kodi za
ndani. Kodi hiyo itatozwa chini ya Sheria ya Fedha ya mwaka 2015 na usimamizi
wake utafuata Sheria ya Usimamizi wa Kodi (TAPA) namba 7 ya mwaka 2009. Kodi
zinazopendekezwa kutozwa kwa madhumuni ya
Miundombinu ni kama ifuatavyo:
i.
Kutoza Dola moja
ya Kimarekani kwa siku kwa kila mgeni atakaelala katika hoteli za Zanzibar
ambapo itachangia TZS 3.2 bilioni;
ii.
Kutoza TZS 2,000
kwa kila abiria anaeondoka katika Bandari za Zanzibar kwenda Katika Bandari
nyengine za Tanzania nje ya Zanzibar na TZS 2,000 kwa kila abiria anaeondoka
katika Bandari za Zanzibar kwenda katika Bandari nyengine za Zanzibar. Jumla ya
TZS 1.9 bilioni zinatarajiwa kupatikana kutokana na hatua hii;
iii. Kutoza TZS 2,000
kwa kila abiria anaeondoka katika kiwanja cha ndege kilichopo Zanzibar na
kwenda kiwanja chengine ndani ya Tanzania. Jumla ya TZS 684 milioni
zinatarajiwa kukusanywa.
iv.
Kutoza asilimia
3 ya thamani za bidhaa zinazoingizwa nchini ambapo jumla ya TZS 10.0 bilioni
zinatarajiwa kukusanywa;
v.
Kutoza asilimia
2 kwa ununuzi wa umeme na kutarajiwa kuingiza TZS 0.9 bilioni
vi.
Kutoza TZS 100/=
ya ziada kwa lita ya Petroli au Dizeli inayoingizwa nchini. Hatua hii
inatarajiwa kuingiza jumla ya TZS 8.3 bilioni.
Kwa ujumla,
hatua zote hizo zinatarajiwa kuingiza jumla ya TZS 25.0 bilioni.
5. Ada ya viwanja vya ndege na
Bandari (Sheria ya Ada ya Bandari Namba 2 ya Mwaka 1999)
51.
Mheshimiwa Spika, Kampuni za Ndege zinazotoa huduma za usafiri hapa Zanzibar,
huwatangazia abiria wanaosafiri kwenda nje ya Tanzania Dola 9 kwa mujibu wa Sheria
ya Tanzania Bara kwa kila abiria kama ni Ada ya usalama wa uwanja wa ndege.
Kampuni hizo hukusanya ada hiyo na huwasilisha malipo ya Dola 8 kwa kila abiria
kwa mujibu wa Sheria ya Zanzibar. Ili kurekebisha kasoro hiyo inapendekezwa
kuongezwa ada hiyo kutoka Dola 8 hadi 9 ili kutambua rasmi ada hiyo inayotozwa
sasa.
52.
Mheshimiwa Spika, Kwa upande wa Bandari, Serikali inajukumu la kuimarisha huduma katika
Bandari zake, Unguja na Pemba. Hivyo, inapendekeza kuongeza tozo la mauzo ya
tiketi na usafirishaji wa mizigo baharini kutoka asilimia 5 ya sasa hadi
asilimia 8.
Hatua hizi zinatarajiwa kuingizia Serikali jumla ya
TZS 969 milioni.
6. Kuondoa misamaha ya kodi ya
mapato (Tax Holidays) na kuruhusu punguzo la Uchakavu kwa haraka Zaidi
(Accelerated Depreciation)
53.
Mheshimiwa Spika, Mfumo uliopo sasa wa kutoa misamaha kwa wawekezaji wa ndani na nje
katika kodi ya mapato itokanayo na faida (Corporate Income Tax Holiday)
umepitwa na wakati, na hauendani na mahitaji ya uwekezaji. Miongoni mwa
changamoto zinazokabili mfumo huu ni kama zifuatzo:-
i.
Kutokuwepo kwa
usawa katika utowaji wa misamaha kwa miradi ya wawekezaji ambapo miradi yenye
kurejesha gharama kwa haraka (higher rate of return) inapatiwa msamaha sawa na
ile inayorejesha taratibu (lower rate of return).
ii.
Kuwezesha uhamishaji
wa faida kutoka kampuni moja kwenda nyengine zinazomilikiwa na mtu mmoja
(domestic transfer pricing).
iii.
Unawezesha
mwekezaji kupatiwa msamaha wa kodi na baada ya kumalizika kwa muda wa msamaha
huo anafunga biashara/anauza mradi na hatimae kuja mwekezaji mwengine na kudai
tena msamaha.
iv.
Unavutia zaidi
miradi midogo midogo kuliko miradi mikubwa.
v.
Unapelekea kutokujulikana
kiwango sahihi cha misamaha ya kodi inayotolewa na Serikali.
54.
Mheshimiwa Spika, Ili kuondokana na changamoto hizo inapendekezwa kubadilisha mfumo wa
sasa na kwenda na mfumo wa “Accelerated Depreciation” ambao unaruhusu msamaha
kwa vifaa vilivyowekezwa na kutumika katika mradi. Marekebisho haya yatafanywa
chini ya Sheria ya kulinda Vitega Uchumi namba 11 ya mwaka 2004.
Hatua hii inatarajiwa kuongeza mapato jumla ya TZS 500 milioni kwa mwaka
2015/16. Mafanikio zaidi ya ukusanyaji yanatarajiwa miaka inayofuata baada ya
kumaliza kipindi cha msamaha kwa wawekezaji wenye msamaha huo kwa sasa hivi.
6. Sheria ya Usajili wa Kampuni
55.
Mheshimiwa Spika, kutokana na gharama kubwa za kusajili jina la biashara zinazowakabili
wawekezaji wa ndani na nje ya nchi, wawekezaji hao hupunguza kiwango cha mtaji
wanaposajili jina la biashara. Kuanzia mwaka wa fedha wa 2015/16 inapendekezwa
kupunguza gharama za kusajili jina la biashara na kuwa TZS 5,000 tu kutoka
asilimia moja ya mtaji.
7. Kupunguza Misamaha ya Kodi (Sheria
ya kodi ya Ongezeko la Thamani Namba 4 ya mwaka 1998)
56.
Mheshimiwa Spika, Ili kuimarisha mapato ya Serikali, katika mwaka unaoendelea wa fedha, Serikali
ilipunguza unafuu wa misamaha ya Ushuru na Kodi ya VAT kwa wawekezaji. Hatua
hii haikuhusisha Taasisi za kijamii (NGOs) na za kidini. Kwa mwaka wa fedha 2015/16
inapendekezwa kupunguza kiwango cha unafuu maalum kwa kodi ya VAT kwa taasisi
za kijamii na kidini hadi kufikia asilimia 75 kama inavyoonekana katika vifungu
vya (k), (i) na (m) vya jadweli ya 3 ya Sheria ya VAT. Kwa mabadiliko haya,
Taasisi hizo sasa zitapaswa kulipa asilimia 25 ya Kodi na kusamehewa asilimia
75 iliyobakia kwa vifaa vinavyostahiki msamaha. Lengo la hatua hii ni
kuwianisha viwango vya misamaha baina ya ile inayotolewa kwa wawekezaji ambao
tayari unafuu wao ni asilimia 75 na misamaha inayotolewa kwa Taasisi zisizo za
Kiserikali.
Hata hivyo, Serikali itaendelea kutoa msamaha wa asilimia 100 kwa
taasisi hizo za kijamii na kidini kwa ajili ya shughuli za misaada wakati wa
maafa na pia katika miradi inayotekelezwa pamoja na Serikali katika huduma za maji,
afya na elimu. Hatua hii haitarajiwi kuongeza sana mapato, bali inakusudia kuleta
uwiano wa misamaha baina ya wawekezaji na taasisi zisizo za kiserikali na hivyo
kurahisha usimamizi wa Kodi.
8. Ada ya Uingizaji wa Magari
57. Mheshimiwa
Spika, Serikali, kupitia Shirika la
Magari, ilikuwa ikitoza Ada ya TZS 100,000 kwa magari yote yanapoingia nchini.
Kufuatia kufungwa rasmi Shirika hilo, kwa sasa mapato haya yanakusanywa na TRA na
kuingizwa Mfuko Mkuu wa Serikali. Kwa mwaka wa fedha ujao, inapendekezwa kubadilisha
kiwango hicho na kuweka kiwango mbadala cha ama TZS 100,000 kwa gari au aslimia
3 ya thamani ya gari inayoingizwa kwa kufuata kiwango kinachotoa mapato zaidi.
Marekebisho haya yatafanywa kupitia Kanuni zilizo chini ya Sheria ya Biashara,
namba 14 ya mwaka 2013. Hatua hii itaongeza mapato ya Serikali kwa jumla ya TZS
800 milioni.
Hata hivyo, kutokana na
kuongezeka kwa gharama za matengenezo ya barabara kutokana na kupanuka kwa
mtandao wa barabara nchini, mapato yatakayopatikana kutokana na ada hii
yatapelekwa Mfuko wa Barabara ili kusaidia zaidi matengenezo ya barabara.
9. Msamaha wa Ushuru wa Forodha kwa Majiko (Stoves) yanayotumia Ethanol iliyosarifiwa
58. Mheshimiwa
Spika, Ripoti za tafiti mbalimbali
zinaonesha kuwa bado wananchi wengi wanatumia kuni na bidhaa za kuni kama vile
makaa kwa ajili ya nishati ya kupikia nyumbani. Hali hii inaendelea kuathiri
mazingira yetu na vyanzo vya maji kutokana na ukataji mkubwa wa misitu ya
asili. Katika miaka ya karibuni baadhi ya wananchi wameanza kutumia gesi ya
asili katika matumizi ya nyumbani. Hata hivyo, bado matumzi hayo hayajakuwa kwa
kiasi cha kutosha kupunguza matumizi ya kuni na makaa. Kwa kushirikiana na
Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo ya Viwanda, UNIDO, utafiti umefanywa
juu ya matumizi ya majiko yanayotumia spiriti ya aina ya ethanol.
59.
Mheshimiwa Spika, matokeo ya utafiti huo yameonesha matumaini makubwa kwa upande wa
unafuu wa gharama, nishati inayopatikana na ufanisi wake. Kwa kuwa jitihada za Serikali
za kufufua kiwanda cha Sukari cha Mahonda kupitia uwekezaji binafsi
zinaendelea, na inatarajiwa kuwa miongoni mwa bidhaa za ziada zitakazozalishwa
kiwandani hapo ni ethanol, kuna haja ya kuanza kushajiisha matumizi ya majiko
maalum yanayotumia aina hii ya nishati. Serikali inapendekeza kuondoa ushuru
kwa majiko hayo. Aidha, hadi hapo spiriti ya ethanol itakapotengenezwa ya kutosha
nchini, inapendekezwa pia kuondoa ushuru wa forodha kwa uingizaji wa ethanol iliyosarifiwa
maalumu kwa matumizi ya nishati.
Kwa kuwa kwa sasa majiko haya hayaingizwi, hatua hii haitarajiwi kuleta
athari ya mapato.
60.
Mheshimiwa Spika, Serikali itahakikisha kuwa kuna usimamizi mzuri wa ukusanyaji wa mapato
kwa taasisi zote ili kuhakikisha malengo waliyowekewa yanafikiwa. Usimamizi huo
utajumuisha kuzipitia mara kwa mara taasisi husika kwa kuzifanyia tathmini na
kuzikagua ili kujua changamoto zilizopo kwa lengo la kuimarisha vyanzo vya ukusanyaji
wa mapato. Aidha, Wakuu wa Taasisi wanatakiwa wawe makini katika kusimamia mapato
ya taasisi zao ili kufanikisha shabaha zilizowekwa.
H. MAKADIRIO YA MATUMIZI KWA MWAKA
2015/16
61.
Mheshimiwa Spika, kwa mwaka 2015/16 jumla ya TZS 830.4 bilioni zimekadiriwa kutumika kwa
kazi za kawaida na maendeleo. Kwa upande wa matumizi ya kazi za kawaida, Serikali
inatarajia kutumia jumla ya TZS 431.4 bilioni sawa na ongezeko la asilimia 26 ikilinganishwa
na TZS 343.4 bilioni zitakazotumika mwaka 2014/15. Kwa upande wa kazi za
maendeleo, jumla ya TZS 399.0 bilioni zinatarajiwa kutumia ikiwa ni ongezeko la
asilimia 122 kwa kulinganishwa na TZS 179.7 bilioni zinazotarajiwa kutumika
hadi Juni 2015. Ongezeko hilo kubwa linatarajiwa kutokana na upatikanaji wa
fedha kwa ajili ya ukamilishaji wa Mradi wa Ujenzi wa Jengo jipya la abiria
katika kiwanja cha ndege cha Abeid Amani Karume. Fedha hizo, zinatarajiwa
kuongeza pia mchango wa Washirika wa maendeleo kwa asilimia 171 kutoka TZS
127.9 bilioni zinazotarajiwa kutumika hadi Juni 2015 hadi kufikia TZS 347.1
bilioni kwa mwaka wa fedha 2015/16.
62.
Mheshimiwa Spika, Serikali inatarajiwa kuchangia jumla ya TZS 51.9 bilioni kama mchango
wake kwa kazi za Maendeleo sawa na matumizi ya TZS 51.8 bilioni ya mwaka
2014/15.
I.MAENEO MUHIMU YALIZONGATIWA KATIKA BAJETI YA MWAKA 2015/16
63.
Mheshimiwa Spika, Serikali ni ya Wananchi na siku zote huwa inafanyakazi kwa ajili yao.
Kwa kutambua ukweli huu, Bajeti ya Serikali itaendelea kuelekeza fedha katika
maeneo makubwa yanayowagusa wananchi. Kwa mwaka ujao wa Fedha, maeneo muhimu
yaliozingatiwa ni pamoja na haya yafuatayo:
1. Miundombinu
64.
Mheshimiwa Spika, nchi yetu bado ni miongoni mwa nchi maskini zaidi duniani na ni nchi
inayoendelea. Kwa kawaida, nchi zilizomo katika kundi hili huwa na uhaba wa
miundombinu mbalimbali muhimu ikiwemo ya nishati, barabara, viwanja vya ndege,
bandari, na maji. Kwa mwaka ujao wa
fedha, Serikali imetenga jumla ya TZS 212.4 bilioni kwa kazi za maendeleo
katika Sekta za Miundombinu na Mawasiliano na Maji na Nishati pekee. Kiasi
hicho ni sawa na asilimia 53.2 ya Bajeti yote ya Kazi za Maendeleo.
2. Huduma za Elimu
65. Mheshimiwa
Spika, kulingana na matokeo ya Sensa ya
Watu na Makaazi ya mwaka 2012, Zanzibar kwa sasa inakisiwa kuwa na watu wapatao
1,375,000. Asilimia 42.5 ya idadi yote ni watoto walio na umri wa chini ya
miaka 15. Aidha, asilimia 20.3 ya idadi yote ni watu walio na umri wa kati ya miaka
15 na 24. Takwimu pia zinaonesha kuwa kwa mwaka 2014, watoto wapatao 253,152
walikuwa katika skuli za msingi, kati yao 233,883 wakiwa katika skuli za Msingi
za Serikali, sawa na asilimia 92.4 ya wanafunzi wote wa Skuli za Msingi. Aidha,
takwimu pia zinaonesha kuwa kwa mwaka huo, tulikuwa na wanafunzi 81,621 katika
Skuli za Sekondari kuanzia kidato cha kwanza hadi cha sita. Kati yao, wanafunzi
74,968 sawa na asilimia 91.8 walikuwa katika Skuli za Serikali. Kwa upande wa
Elimu ya juu, takwimu zinaonesha kuwa kwa mwaka huo tulikuwa na zaidi ya
wanafunzi 11,000 katika vyuo mbalimbali vilivyopo Zanzibar pekee.
66.
Mheshimiwa Spika, takwimu hizi zinamaanisha kwamba kwa ujumla, jamii yetu kwa kiasi
kikubwa inaundwa na vijana, hasa watoto wa chini ya miaka 25 ambao kwa ujumla
wanafikia asilimia 62.8 ya watu wote wa Zanzibar. Kundi hili lina mahitaji
maalum. Kwa umri wa kuwa skuli, mahitaji muhimu zaidi ni elimu. Serikali
inatambua wajibu wake wa kutoa Elimu iliyo bora kwa watoto wetu wote. Kwa
sababu hii, jumla ya TZS 120.7 bilioni sawa na asilimia 14.5 ya Bajeti yote zimetengwa
kwa ajili ya Sekta ya Elimu. Sekta hii pia ndio inayoongoza kwa Bajeti ya Kazi
za kawaida kwa kutengewa TZS 96.8 bilioni, sawa na asilimia 22 ya Bajeti yote
ya kazi za kawaida.
67.
Mheshimiwa Spika, kutokana na matumizi hayo, na kwa kuzingatia Sera ya Elimu Bila ya
Malipo iliyotangazwa mara tu baada ya Mapinduzi matukufu ya mwaka 1964, na kama
ilivyoelezwa katika Mpango wa Maendeleo uliowasilishwa leo kuwa mojawapo ya
vipaumbele ni kutoa elimu iliyo bora, Serikali inakusudia kuchukua hatua
makhsusi zinazolenga kubeba zaidi jukumu la kutoa elimu kwa watoto wetu. Naomba
nitamke rasmi kuwa
kuanzia mwaka wa
fedha 2015/16, michango yote wanayotozwa wazazi kwa elimu ya watoto wa skuli za
msingi imefutwa. Hakuna mzazi atakaetozwa malipo yoyote kwa mtoto anaesoma
skuli ya Msingi ya Serikali. Serikali itabeba jukumu la kuwasomesha watoto
wote.
68.
Mheshimiwa Spika, Kwa upande wa Elimu ya Sekondari, Serikali inajipanga ili nako elimu
yote iweze kutolewa bila ya malipo. Kwa
kuanzia, kwa mwaka wa fedha 2015/16, Serikali inafuta rasmi malipo yote
yanayotozwa wazee kwa ajili ya mitihani ya Kidato cha pili, kidato cha nne na
kidato cha sita. Wazazi hawatatozwa tena malipo yoyote ya mitihani ya
sekondari kwa watoto wao. Serikali inabeba pia jukumu hili.
Kwa kutekeleza azma hiyo ya Serikali ya kuwaondoshea wazee michango ya
elimu ya Msingi na malipo kwa ajili ya mitihani ya Sekondari, Serikali imetenga
jumla ya TZS 8.0 bilioni kwa mwaka ujao wa fedha 2015/16. Aidha, jumla ya TZS
9.5 bilioni zimetengwa kwa ajili ya Ruzuku kwa Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu. Tokea
kuanzishwa kwa Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu mwaka 2011, Serikali imeshatowa
Zaidi ya TZS 26 bilioni kwa ajili ya Mikopo ya Elimu ya Juu.
3. Huduma za Afya
69.
Mheshimiwa Spika, sekta nyengine muhimu na inayomgusa takriban kila mwananchi ni sekta ya
Afya. Takwimu za Sensa ya Watu na Makaazi zinaonesha kuwa asilimia 15.6 ya
wakaazi wote wa Zanzibar ni watoto wa chini ya umri wa miaka mitano. Kwa
takwimu za sasa za idadi ya watu, watoto wa kundi hili wanafikia 214,500. Watoto
hawa wana mahitaji maalum ya afya, hususan chanjo dhidi ya maradhi mbalimbali.
70.
Mheshimiwa Spika, kwa upande mwengine, Utafiti wa Kijamii na Uchumi wa mwaka 2015 unaonesha
kuwa kwa mwaka 2014, jumla ya wagonjwa 440,201 walitibiwa katika hospitali za
Serikali. Hali hii inaonesha kupungua kwa wagonjwa kutoka wagonjwa 456,750
waliotibiwa mwaka 2013. Kama nilivyotamka awali kuwa moja ya malengo makuu
yaliomo katika falsafa ya Dira ya Maendeleo ni kujenga Taifa la watu wenye
siha, uimarishaji wa Sekta ya afya una umuhimu wa pekee. Kwa kuzingatia dhima
hii, Serikali imetenga jumla ya TZS 85.0 bilioni sawa na asilimia 10.2 ya
Bajeti ya Serikali ya mwaka 2015/16 kwa Sekta ya Afya na hivyo kuifanya kuwa
sekta ya tatu kifedha ikitanguliwa na Miundombinu na Elimu.
71.
Mheshimiwa Spika, miongoni mwa maeneo muhimu katika uimarishaji wa Afya ni upatikanaji wa
Dawa, vifaa vya tiba na nyenzo nyengine muhimu. Kwa miaka kadhaa sasa sehemu
kubwa ya dawa kwa ajili ya Hospitali zetu imekuwa ikipatikana kwa msaada wa
Washirika wa Maendeleo hususan Shirika la Maendeleo la Denmark, DANIDA. Hata
hivyo, Taarifa zilizopo sasa zinaashiria kuwa DANIDA imeanza kupunguza msaada
wake kwa Sekta ya Afya. Pamoja na hali
hiyo, kwa niaba ya Serikali na wananchi wote wa Zanzibar naomba nitumie fursa
hii kulishukuru kwa dhati kabisa Shirika la DANIDA kwa msaada wake katika
kipindi chote hicho, msaada ambao umenusuru maisha yetu na wananchi wenzetu.
Serikali kwa kutambua dhima yake katika upatikanaji wa dawa, vifaa vya tiba na
vifaa vyenginevyo, imefanya uamuzi wa kubeba jukumu hili kutoka kwa Washirika
wa Maendeleo. Kwa Bajeti ya mwaka 2015/16 jumla ya TZS 4.5 bilioni zimetengwa
kwa ajili ya ununuzi wa dawa na vifaa mbalimbali vya tiba.
72.
Mheshimiwa Spika, Serikali imekuwa ikipeleka nje ya nchi, hususan nchini India, wagonjwa
ambao matibabu yao yameshindikana hapa nchini. Pamoja na gharama za matibabu
nje ya nchi kuwa kubwa sana, bado utaratibu huu umesaidia sana ama kuokoa
maisha ya wananchi wenzetu au kuwaondoshea maradhi yalioshindikana hapa nchini.
Kwa bahati mbaya, fedha zilizokuwa zikitengwa kwa madhumuni haya ni kidogo
wakati mahitaji yake ni makubwa sana. Kwa mwaka ujao wa fedha, Serikali
imetenga jumla ya TZS 2.5 bilioni kwa madhumuni hayo hii ni zaidi ya asilimia 213
ya iliotengwa kwa ajili ya mwaka 2015/16. Hata hivyo, ni muhimu kutambua kwamba
utaratibu huu umewekwa kwa wenzetu ambao matibabu yao hayapatikani hapa nchini.
Jitihada za kudhibiti matumizi ya fursa hii zitaimarishwa ili kuhakikisha
unanufaisha wale tu wanaohitaji kweli matibabu nje ya nchi.
4. Huduma kwa Wazee
73.
Mheshimiwa Spika, kundi jengine muhimu kwa jamii yetu ni Wazee. Kundi hili pia lilipewa
umuhimu maalum tokea Mapinduzi yetu matukufu kwa kupatiwa makaazi na matunzo
maalum. Taarifa ya Sensa ya mwaka 2012 inaonesha kuwa Wazee waliofikia miaka 65
na zaidi ni asilimia 2.8 ya watu wote wa Zanzibar. Hawa ni wazee wetu ambao
wameshatoa mchango mkubwa katika maendeleo ya Taifa letu, ulezi wa vijana na
watoto na sasa wamefikia umri wa kusaidiwa. Takwimu zinaonesha kuwa idadi ya
wazee wanaohitaji msaada wa matunzo ya Serikali imekuwa ikipungua kutoka Wazee
223 mwaka 2010 hadi Wazee 148 mwaka 2015. Hali hii inamaanisha kuwa wengi wa
Wazee wetu wanatunzwa na jamii, hasa watoto na jamaa zao. Baadhi ya Wazee hawa
ni wale waliotumikia Serikali wakati wa ujana wao na kwa sasa ni Wastaafu na
wanategemea kipato cha Pencheni.
74.
Mheshimiwa Spika, kumekuwa na malalamiko ya udogo wa kiwango cha chini cha Pencheni
kinachotolewa sasa. Serikali iliahidi kukiangalia kiwango hicho kwa kadiri hali
itakavyoruhusu hasa kwa kuzingatia kuwa mara kadhaa kumekuwa na marekebisho ya
mishahara kwa Wafanyakazi wa Serikali ambayo hayakuhusisha pencheni.
Kwa mwaka wa fedha 2015/16, Serikali
inakusudia kupandisha kiwango cha chini cha pencheni kutoka TZS 40,000 kwa
mwezi za sasa hadi TZS 60,000.
Marekebisho haya yamelenga zaidi kwa wale
ambao wanapokea kiwango cha chini cha pencheni.
75.
Mheshimiwa Spika, baadhi ya nchi duniani zina utaratibu wa kulipa pencheni kwa wazee hata
kama sio wastaafu wa Serikalini. Katika nchi za jirani kama vile Mauritius ,
utaratibu huu umetumika kwa miaka kadhaa sasa. Serikali kwa kusaidiana na
Taasisi ya kuwasaidia Wazee ya "Help Age International" imefanya
utafiti na kuzingatia uzoefu wa nchi nyengine katika kutunza Wazee. Kwa sasa
Serikali inakamilisha taratibu za kuwatambua Wazee wote waliofikia miaka 70 na
zaidi kwa lengo la kuwapatia vitambulisho vyao pamoja na taratibu nyengine. Zoezi
hili litachukua sio zaidi ya miezi 10.
Nina
furaha kulitangazia Baraza lako tukufu kuwa kuanzia tarehe 1 April mwaka 2016,
Serikali itaanza kulipa pencheni kwa Wazee wote waliofikia umri wa miaka 70
(universal pension).
Pencheni hiyo itatolewa kwa Wazee waliofikisha umri
huo bila ya kujali kipato chake na italipwa kwa kiwango cha TZS 20,000 kwa
mwezi. Jumla ya TZS 1.65 bilioni zinatarajiwa kutumika kwa ajili hiyo.
5. Makundi Maalum
76.
Mheshimiwa Spika, makundi haya yanajumuisha makundi yenye mahitaji maalumu kama vile watu
wenye ulemavu, watu wanaoishi na UKIMWI na VVU, watumiaji wa dawa za kulevya na
kadhalika. Kupitia Sheria mbalimbali, Serikali itaanzisha Mifuko maalum ili
kukidhi mahitaji ya fedha kwa makundi hayo na sehemu ya fedha za mfuko
zitatolewa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
77.
Mheshimiwa Spika, nimetumia muda mwingi kueleza mambo haya ili Wananchi wenyewe waone
vipi fedha zao wanazolipa kupitia kodi mbalimbali zinavyotumika. Aidha, imekuwa
ni muhimu kueleza haya ili waweze kuelewa hatua zinazochukuliwa na Serikali yao
katika kutumia fedha chache zilizopo kutatua matatizo mbalimbali
yanayowakabili. Nikizungumzia uchache wa fedha, naomba sasa nitoe uchambuzi wa
Bajeti ya mwaka 2015/16.
J. UCHAMBUZI WA BAJETI 2015/16
78.
Mheshimiwa Spika, Kama nilivyotangulia kusema, matarajio ya mapato ya ndani hadi kufikia
mwezi Juni 2015 ni kufikia TZS 360.4 bilioni. Hatua za kuimarisha usimamizi wa
mapato pamoja na hatua mpya zinazopendekezwa kwa mwaka wa fedha 2015/16 zinatarajiwa kuongeza
jumla ya TZS 90.1 bilioni na hivyo kufanya mapato ya ndani kufikia TZS 450.5
bilioni.
79.
Mheshimiwa Spika, Katika mwaka wa fedha 2015/16, matumizi ya lazima (mandatory
expenditure) yatagharimu Serikali jumla ya TZS 346.0 bilioni. Matumizi haya ni
pamoja na haya yafuatayo:
a)
Mishahara ya
Wizara na Taasisi zote zinazopokea ruzuku itafikia TZS 223.7 bilioni
b)
Matumizi ya
kisheria ya Mfuko Mkuu wa Serikali (CFS) yamefikia TZS 53.4 bilioni ikijumuisha
Pencheni TZS 11.0 bilioni, Mishahara ya Mfuko Mkuu TZS 1.3 bilioni, Malipo ya
mikopo na riba TZS 20.95 bilioni na Malipo ya viinua mgongo TZS 11.0 bilioni
pamoja na Malipo ya Mafao ya Wajumbe Wastaafu wa Baraza la Wawakilishi na
Wanasiasa wengine ni TZS 8.5 bilioni
c)
Gharama za
miradi yanye dhima (Commited Projects) TZS 39.1 bilioni , ikijumuisha kupandisha hadhi hospitali ya mnazi mmoja TZS
4.0 bilioni, Ujenzi wa barabara Unguja
na Pemba TZS 6.6 bilioni, Ujenzi wa
Jengo Jipya la Abiria TZS 3.0 bilioni na uwekaji wa kamera na vifaa vya ulinzi
TZS 10.0 bilioni
d)
Gharama za
chakula cha wagonjwa ni TZS 0.3 bilioni
e)
Ruzuku za
kisheria za TZS 29.5 bilioni ikiwemo, ZRB TZS 11.3 bilioni, Mfuko wa Barabara
TZS 10.2 bilioni, SDL TZS 6.2 bilioni pamoja na ununuzi wa madeski TZS 1.8
bilioni.
Matumizi haya ya lazima yatabakisha
TZS 104.5 bilioni tu ya mapato ya ndani.
80.
Mheshimiwa Spika, Pamoja na gharama hizo za lazima, Serikali inakabiliwa na ongezeko la
gharama mbali mbali zisizoepukika (Committed Expenditure). Matumizi hayo
yasiyoepukika kwa mwaka huu, yataigharimu Serikali jumla ya TZS 42.5 bilioni.
Matumizi hayo ni pamoja na haya yafuatayo:
a)
Gharama za
Uchaguzi mkuu TZS 7.5 bilioni
b)
Gharama
zinazoambatana na awamu mpya ya Serikali na Baraza la Wawakilishi TZS 1.8
bilioni
c)
TZS 1.65
bilioni zitatumika kwa ajili ya kulipia pencheni kwa wazee wote walio na umri
kuanzia miaka sabini.
d)
Gharama za
Huduma za afya ikiwemo Ununuzi wa Dawa na matibabu nje TZS 7.0 bilioni
e)
Uimarishaji
wa Huduma za Elimu ikiwemo uamuzi wa Serikali wa kutoa huduma zote za Elimu ya
msingi na mitihani ya elimu ya Sekondari bila ya Malipo TZS 8.0 bilioni
f)
Ziada ya
Ruzuku ya Pembejeo za Kilimo ya TZS 500 milioni
g)
Malipo ya
Bili za Umeme kwenye visima vya maji ni TZS 4.5 bilioni
h)
Baraza la
mitihani TZS 2.0 bilioni
i)
Mkopo wa
Elimu ya juu TZS 9.5 bilioni
81.
Mheshimiwa Spika, Matumizi haya yatabakisha jumla ya TZS 62.0 bilioni. Hali hii, ikizingatiwa pia na kutokuwepo kwa
misaada ya kibajeti (GBS) iliokuwa ikifikia wastani wa TZS 40 bilioni,
itapelekea kupungua sana kwa bajeti ya matumizi ya kawaida kwa Wizara na
Taasisi zote za Serikali pamoja Miradi ya maendeleo. Hata hivyo TZS 2.8 bilioni
zinatarajiwa kupatikana kutokana na msamaha wa madeni pamoja na Mfuko wa
Wafadhili na kupelekea jumla ya bakaa ya TZS 64.9 bilioni. Miradi iliyobakia ya
maendeleo inatarajiwa kutumia jumla ya TZS 12.8 bilioni ambayo itapunguza bakaa
hadi kufikia TZS 52.0 bilioni. Gharama za matumizi ya kawaida (TZS 65.7
bilioni) na matumizi mengineyo ya Mfuko mkuu wa Serikali (16.3 bilioni) yanatarajiwa
kufikia jumla ya TZS 82.0 bilioni, na kupelekea nakisi ya TZS 30 bilioni.
Inapendekezwa kukopa ndani ya nchi kiasi hicho cha TZS 30.0 bilioni na hivyo
kuziba nakisi yote ya Bajeti.
82.
Mheshimiwa Spika, Serikali imeandaa utaratibu madhubuti utakaohakikisha matumizi mazuri
ya fedha za umma kwa taasisi zake. Utaratibu huu ni pamoja na matumizi ya mfumo
mpya wa bajeti unaozingatia matokeo (PBB). Uwazi wa mfumo huo, utawawezesha
Wajumbe wa Bazara lako tukufu kuhoji matokeo ya huduma mbali mbali zinazotolewa
na programu kwa kuangalia viashiria vya huduma hizo.
K. SURA YA BAJETI KWA MWAKA 2015/16
83.
Mheshimiwa Spika, kutokana na maelezo ya hapo juu, Bajeti ya mwaka 2015/16 inatarajiwa
kuwa na mwelekeo ufuatao:
Mapato:
84.
Mheshimiwa Spika, Bajeti ya mwaka 2015/16, inatarajiwa kuwa na mapato ya jumla ya TZS
830.4 bilioni zikihusisha mapato ya ndani ya TZS 450.5 bilioni na mikopo ya
ndani ya TZS 30 bilioni. Fedha kutoka
kwa Washirika wa Maendeleo kwa ajili ya Programu na Miradi ya Maendeleo ambazo
ni TZS 347.1 bilioni na TZS 2.8 bilioni za Msamaha wa madeni na Mfuko wa
Wafadhili. Kwa upande wa matumizi, kati ya TZS 830.4 bilioni zinazotarajiwa,
matumizi kwa Kazi za Kawaida yanatarajiwa kufikia TZS 431.4 bilioni na yale ya
kutekeleza Mpango wa Maendeleo ni TZS 399.0 bilioni.
85.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa mchango wa maendeleo ni TZS 98.2 bilioni tu zinazotarajiwa
kupokelewa kama Ruzuku, kwa kiasi kikubwa Bajeti ya mwaka 2015/16 inategemewa
itokane na fedha zetu wenyewe, ama za makusanyo ya ndani au mikopo itakayolipwa
baadae. Kutokana na hali hiyo, kiwango
cha utegemezi kinatarajiwa kushuka hadi kufikia asilimia 12.2 tu. Kwa sababu
hii, na kwa sababu ya fedha nyingi zilizoelekezwa katika huduma mbalimbali
zinazolenga masuala muhimu ya kijamii, nathubutu kutamka kuwa Bajeti
ya mwaka 2015/16 ni Bajeti ya Jamii na Kujitegemea.
86.
Mheshimiwa Spika, Mfumo wa bajeti ya Serikali kwa mwaka 2015/16 utakuwa kama
unavyoonekana katika Jadweli hapa chini.

Chanzo: Wizara ya Fedha
L. SHUKRANI
87.
Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema awali, kikao hichi cha Bajeti kinahitimisha miaka
mitano ya uongozi wa awamu hii. Mosi, naomba nitumie fursa hii kuwashukuru sana
Wananchi wote wa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla. Nawashukuru kwa kutuamini na
kuturuhusu kuwatumikia kwa kipindi chote cha miaka mitano, nawashukuru kwa
imani yao muda wote wa kipindi hicho, na nawashukuru kwa utulivu wao mkubwa
waliouonesha ambao umetusaidia sana katika kuwatumikia vyema.
88.
Mheshimiwa Spika, Pili, naomba pia kwa niaba ya Serikali kukushukuru sana wewe binafsi
Mheshimiwa Spika na Mheshimiwa Omar Othman Makungu, Jaji Mkuu wa Zanzibar kwa
uongozi wenu katika mihimili ya Baraza la Wawakilishi na Mahakama uliokuwa na
mashirikiano makubwa na Mhimili wa Utawala wa Serikali. Bila ya shaka, kupitia
kwako Mheshimiwa Spika, nawashukuru sana Mheshimiwa Ali Abdulla Ali, Naibu
Spika, na wenyeviti wote wa Baraza ambao wamekuwa wakikusaidia wewe
unapodharurika. Mashirikiano yenu yametusaidia sote kuwa na utulivu wa
kutekeleza majukumu yetu na kuwatumikia wananchi wenzetu.
89.
Mheshimiwa
Spika, tatu naomba kuwashukuru sana Waheshimiwa wajumbe wote wa Baraza hili
kwa mashirikiano makubwa kwa kipindi chote cha utendaji wetu wa pamoja. Kwa
namna maalum naomba pia kumshukuru Mwenyekiti wa Kamati ya wenyeviti wa Kamati
za Kudumu za Baraza la wawakilishi, Mheshimiwa Hamza Hassan Juma, na wajumbe
wake ambao ni, Mwenyekiti wa Kamati ya Kuchunguza Hesabu za Serikali (PAC),
Mheshimiwa Omar Ali Shehe Mwenyekiti wa Kamati ya Fedha, Biashara na Kilimo, Mheshimiwa
Hija Hassan Hija, Mwenyekiti wa Kamati ya Mawasiliano Mheshimiwa Mahmoud Mohammed
Mussa, Mwenyekiti wa Kamati ya Ustawi wa Jamii Mheshimiwa Mgeni Hassan Juma na
Mwenyekiti wa Kamati ya Mifugo, Utalii, Uwezeshaji na Habari Mheshimiwa Mlinde
Mabrouk Juma. Kwa nafasi yangu pia nimefanya kazi na kwa karibu zaidi na Kamati
tatu; ya Wenyeviti wa Kamati za Kudumu, Kamati ya Kuchunguza Hesabu za Serikali
na Kati ya Fedha, Biashara na Kilimo. Najihisi nina deni kubwa la kuwashukuru
Wenyeviti na Wajumbe wote wa Kamati hizi kwa mashirikiano yao kwangu. Nasema Ahsanteni
sana nyote.
90. Mheshimiwa
Spika, nne, napenda kutoa shukrani zangu za dhati kwa Kamati ya Makatibu
Wakuu chini ya uongozi wa Dk. Abdulhamid Yahya Mzee, Katibu wa Baraza la
Mapinduzi na Katibu Kiongozi, kwa ushauri wao ambao umekuwa chachu ya utendaji
mzuri wa Serikali yetu. Bila ya shaka, shukurani hizi zinawahusu pia Watendaji
Wakuu na wafanyakazi wa Wizara mbali mbali, Idara zinazojitegemea, Mikoa,
Wilaya, Baraza la Manispaa, Halmashauri za Wilaya, Mabaraza ya Miji, Asasi
zisizo za Kiserikali pamoja na Sekta Binafsi. Wote hawa tumefanya nao kazi kwa
karibu sana na tumenufaika sana na michango na kujitolea kwao kiutaalamu,
kihali na mali.
91. Mheshimiwa
Spika, kazi yangu ya uwaziri imesaidiwa sana na utendaji makini wa
wasaidizi wangu mahiri. Naomba niwashukuru kwa namna ya pekee kabisa ndugu
yangu Khamis Mussa Omar, Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Bi. Amina Khamis
Shaaban, Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango ambae awali ilikuwa sehemu ya
iliyokuwa Ofisi ya Rais – Fedha, Uchumi na Mipango ya Maendeleo niliyokuwa
nikiongoza hadi mwezi Agosti mwaka 2013 ambapo kazi za Mipango zilitenganishwa
kimuundo na zile za Fedha. Namshukuru pia ndugu Juma Ameir Hafidh, Naibu Katibu
Mkuu, Ndugu Omar Hassan Omar, Mhasibu Mkuu wa Serikali, Ndugu Mwita Mgeni
Mwita, Kamishna wa Bajeti, Makamishna, Wakurugenzi na watendaji wote wa Wizara
ya Fedha na Taasisi zake kwa utendaji wao katika kipindi chote cha miaka mitano
inayokaribia kukamilika mwaka huu.
92.
Mheshimiwa
Spika, kipindi cha miaka hiyo mitano tumefanya kazi kwa karibu na kunufaika
na msaada na mashirikiano na nchi rafiki na Mashirika ya kimataifa. Kwa niaba
ya Serikali, kwa niaba yangu binafsi na kwa niaba ya Wananchi wote wa Zanzibar,
naomba kuthamini na kushukuru sana mashirikiano na msaada wa nchi za Canada, China,
Cuba, Denmark, Falme za Kiarabu, Finland, India, Ireland, Japani, Korea ya
Kusini, Kuwait, Marekani, Misri, Norway, Oman, Saudi Arabia, Sweden, Ubelgiji,
Uholanzi, Uingereza, Ujerumani na Uturuki.
93.
Mheshimiwa
Spika, kwa upande wa mashirika ya kimataifa, naomba nishukuru misaada ya:
ACBF, ACCRA, AfDB, AGRA, BADEA, CARE INTERNATIONAL, CDC, CHAI, CIDA, DANIDA,
DFID, EGH, EU, EXIM Bank ya China, EXIM Bank ya Korea, FAO, FHI, GAVI, GEF,
GLOBAL FUND, IAEA, ICAP, IDB, IFAD, ILO, IMF, IPEC, JICA, JSDF, KOICA, MCC, NORAD,
OFID, ORIO-Netherlands, PRAP, SAUDI FUND, Save the Children, SIDA, UN AIDS, UN,
UNDP, UNESCO, UNFPA, UN-HABITAT, UNICEF, UNIDO, USAID, WB, WHO na WSPA.
M. HITIMISHO
94.
Mheshimiwa
Spika, kwa kuwa tumekabiliwa na mchakato wa kidemokrasia unaowataka
Wananchi kuchagua Viongozi wao wa kuwaongoza kwa kipindi cha miaka mitano
ijayo, naomba nihitimishe kwa kuwaomba sana Viongozi wa vyama vya siasa,
wanachama wao na wananchi kwa ujumla kuhakikisha kuwa tunatumia fursa yetu hiyo
ya kuchagua viongozi wetu kwa amani, udugu na upendo mkubwa. Tunaweza
kuchaguana bila ya kuumizana. Tunaweza kuchaguana bila ya kupigana. Tunaweza
kuchaguana bila ya kuhasimiana. Kila mmoja wetu ana dhima ya kuhakikisha
uchaguzi Mkuu wa mwaka huu unakuwa wa mfano kwa utulivu na mafanikio. Kila
mmoja wetu autimize wajibu huo. Niitumie pia fursa hii kuwatakia kheri
Waheshimiwa Wawakilishi wote wanaokusudia kuomba tena ridhaa ya Wananchi
kuwaongoza tena katika Majimbo yao. Tuelewe tu kuwa Wananchi ndio waamuzi,
watakapochagua itakuwa ndio wamesema. Tuheshimu kauli yao na kuikubali bila ya
kinyongo kwani sote ni Wazanzibari na Watanzania. Katika kutafuta ridhaa za wananchi
lugha zetu zina nafasi sana. Wakati wa kampeni tutumie lugha ambazo zitajenga
umoja wetu na kuifanya Zanzibar yetu iwe na Amani; bila ya Amani ule msemo wa “
Zanzibar ni njema atakae aje” utakuwa hauna maana.
95.
Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo hayo, sasa kwa heshima na taadhima naliomba Baraza
lako tukufu lipokee, lijadili na hatimae kwa kauli moja liidhinishe Makadirio
ya mapato ya Shilingi mia nane na
thelathini bilioni na mia nne milioni (TZS 830.4 bilioni) na matumizi ya
kiasi hicho cha fedha kwa ajili ya kugharamia kazi za kawaida za Shilingi mia nne na thelathini na moja bilioni na milioni
mia nne (TZS 431.4 bilioni) na kwa upande wa Mpango wa Maendeleo kutumia Shilingi
mia tatu na tisini na tisa bilioni (TZS
399.0 bilioni) kwa mwaka wa fedha 2015/16.
96. Mheshimiwa Spika, Nashukuru kwa kunisikiliza na sasa naomba kutoa hoja.
Omar Y. Mzee
WAZIRI WA FEDHA,
ZANZIBAR.
13
Mei, 2015
Siku njema Mimi ni Mheshimiwa Alimin Muhammad muslin mkopo Taasisi, mimi ni
ReplyDeleteMkurugenzi Mtendaji wa ALIMIN MUHAMMAD MKOPO KAMPUNI sisi kutoa mikopo binafsi na biashara kwa wale ambao mahitaji mkopo salama na hakuna kuchelewa
Yetu ni 100% kuhakikisha matatizo ya bure katika kiwango cha riba ya 3% wasiliana nasi kupitia aliminmuhammadloancompany@gmail.com
Na kupata mkopo wako leo bila matatizo yoyote
wasiliana nasi leo saa
aliminmuhammadloancompany@gmail.com
Siku njema Mimi ni Mheshimiwa Alimin Muhammad muslin mkopo Taasisi, mimi ni
ReplyDeleteMkurugenzi Mtendaji wa ALIMIN MUHAMMAD MKOPO KAMPUNI sisi kutoa mikopo binafsi na biashara kwa wale ambao mahitaji mkopo salama na hakuna kuchelewa
Yetu ni 100% kuhakikisha matatizo ya bure katika kiwango cha riba ya 3% wasiliana nasi kupitia aliminmuhammadloancompany@gmail.com
Na kupata mkopo wako leo bila matatizo yoyote
wasiliana nasi leo saa
aliminmuhammadloancompany@gmail.com