Habari za Punde

Itikadi za vyama zisitumika katika kuwapatia wanafunzi elimu.

Hassan Khamis, Pemba
MBUNGE wa viti maalum wa chama cha Mapinduzi ‘CCM’ na Mjumbe wa Kamati Kuu na halmashauri kuu taifa Mhe: Dokta Maua Abeid Daftari amewataka waalimu mkoa wa kaskazini Pemba, kuondoa itikadi za vyama katika kuwapatia wanafunzi elimu.
Hayo aliyasema jana alipokua akikabidhi msaada wa vitabu vya kusomea vyenye thamani ya shilingi milioni 10 kwa skuli 11 za Msingi na Sekondari zilizomo katika Mkoa wa Kaskazini Pemba.
Alisema suala la kuwapatia haki ya elimu watoto halipaswi kuhusishwa na itikadi za kichama, na nivyema waalimu wakafanya juhudi ili kuhakikisha wanawasomesha kwa kina.
Aidha Mbunge huyo alieleza kuwa pamoja na changamoto kubwa inayowakabili waalimu hao, ni vyema wakapanga mikakati na mbinu za kudumu ili kuona wanafunzi wanapata elimu ambayo inaweza kuwakomboa hapo baadae.
“Nitakua nikigawa vitabu kila hali ikiruhusu na nitasadia katika nyanja za elimu, afya na ujasiriamali, hivyo nakuombeni walimu muhakikishe vitabu hivi vinatumika kwa lengo lililokusudiwa”,aliesema.

Katika hatua nyengine aliwataka walimu hao kutokubali kurubuniwa na wanasiasa amabao hawaitakii mema nchi hii, na kuwataka wafahamu kuwa muelekeo wa nchi kwa sasa ni kujenga taifa imara litakalosaidia vijana wa sasa na wabaadae kwa kuzingatia elimu waliyoipata.
Skuli zilizofaidika na misaada hiyo ni Chasasa, Kizimbani, Jadida, Pandani, Kangagani, Utaani, Mchanga mdogo, Bopwe, Miti Ulaya, Michewewni na Limbani.
Wakipokea msaada huo walimu wakuu wa skuli hizo wamesifu juhudi zinazofanywa na Mbunge huyo kwa kujitolea katika kusaidia jamii bila ya kujali itikadi za kisiasa.
Walisema yeye ni mtu jasiri anaejali utu katika kutekeleza majukumu yake kwani muendelezo wa juhudi zake unaonekana kila uchao na kupitia juhudi hizo jamii inafaidika na misaada mbalimbali ambayo amekuwa akiitoa kwa jamii.

Nae Aisha Yahya ambae ni mwanafunzi wa skuli ya Miti Ulaya amewaomba watu wengine wenye uwezo kutoa misaada kama hiyo na hata kwa vifaa vyengine vya skuli, kwani wapo wanafunzi wengi wenye moyo wa kusoma lakini wamekua wakishindwa kutokana hali zao za kimaisha kuwa duni.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.