Habari za Punde

Mabalozi wakutana na Rais Dk Shein Ikulu leo

 Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein akisalimiana  na Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania  nchini Japan Batilda Burian aliyeteuliwa hivi karibuni na kufika Ikulu Mjini Zanzibar leo 
kujitambulisha,[Picha na Ikulu.]

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein akizungumza  na Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania  nchini Japan Batilda Burian aliyeteuliwa hivi karibuni na kufika Ikulu Mjini Zanzibar leo kujitambulisha,[Picha na Ikulu.]
 Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein akizungumza na  Balozi wa Malawi katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania  Hawa O.Ndilowe alipofika Ikulu Mjini Zanzibar leo kujitambulisha kwa Rais,[Picha na Ikulu.]
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein akiagana na  Balozi wa Malawi katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania  Hawa O.Ndilowe baada ya mazungumzo yao leo  alipofika Ikulu Mjini Zanzibar kujitambulisha,[Picha na Ikulu.]


  
STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
  Zanzibar                                                                            6.5.2015
---
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesisistiza haja ya kuimarisha zaidi uhusiano na ushirikiano uliopo kati ya Tanzania na Japan hasa kwa kutambua hatua za nchi hiyo za kuendelea kuiiunga mkono Tanzania katika kuimarisha miradi mbali mbali ya maendeleo hapa nchini.

Dk. Shein aliyasema hayo leo huko Ikulu mjini Zanzibar, wakati alipofanya mazungumzo na Balozi Mteule wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Japan Mhe. Batilda Buriani.

Katika mazungumzo hayo Dk. Shein alimueleza Balozi huyo Mteule kuwa Tanzania ikiwemo Zanzibar inajivunia uhusiano na ushirikiano sambamba na hatua za Japan za kuendelea kuiunga mkono Tanzania katika kuimarisha miradi kadhaa hapa nchini.

Dk. Shein alisema kuwa kwa upande wa Zanzibar, Japan imekuwa mshirika mkubwa katika kuunga mkono uimarishaji wa miradi ya maendeleo ikiwa ni pamoja na kusaidia mradi mkubwa wa maji ambao hivi sasa upo katika awamu ya pili sambamba na usambazaji wa huduma za umeme pamoja na miradi mengineyo.


Aidha, Dk. Shein alisema kuwa mbali na juhudi hizo za nchi ya Japan kwa Tanzania kwa vile Zanzibar imekuwa ni miongoni mwa visiwa maarufu kiutalii duniani ipo haja ya kuendelea kuitangaza Zanzibar nchini humo ili wataalii wa Japan waje kuitembea Zanzibar kwa wingi.

Pamoja na hayo, Dk. Shein alitumia fursa hiyo kumueleza Balozi Burian azma ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuimarisha sekta ya uvuvi hapa nchini.

Dk. Shein pia, alimueleza Balozi huyo haja ya kuikuza na kuiimarisha lugha ya Kiswahili kwa kutambua kuwa hivi sasa lugha hiyo imekuwa na nafasi kubwa duniani  ikiwa ni pamoja na kuwepo kwa redio ya kiswahili nchini humo.

Kutokana na hatua hiyo Dk. Shein alisema kuwa ipo haja ya kuikuza lugha hiyo kwa kukitangaza Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar SUZA nchini Japan, ambacho kimekuwa na Kada ya Kiswahili kinachofundishwa kwa wageni.

Nae Balozi huyo Mteule wa Tanzania nchini Japan Mhe. Batilda Burian alitoa pongezi kwa Dk. Shein pamoja na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete kwa kupata uteuzi huo mpya ambapo kabla ya uteuzi huo alikuwa Balozi wa Tanzania nchini Kenya.

Balozi Burian alimuhakikikishia Dk. Shein kuwa katika wadhifa wake huo mpya juhudi za makusudi atazichukua katika kuhakikisha uhusiano na ushirikiano uliopo kati ya Japan na Tanzania unaimarishwa zaidi.

Wakati huo huo, Dk. Shein alifanya mazungumzo na Balozi wa Malawi nchini Tanzania Mhe. Hawa Ndilowe  na kumueleza kuwa Zanzibar ina historia kubwa ya uhusiano na ushirikiano kati yake na Malawi na kusisitiza haja ya kuimarishwa.

Katika mazungumzo hayo, Dk. Shein limueleza Balozi huyo kuwa hivi sasa Zanzibar kutokana na kukua kwa sekta ya elimu ikiwa ni pamoja na kuimarika kwa vyuo vikuu hapa nchini wananchi kutoka Malawi wamekuwa wakipata fursa ya kusoma katika vyuo vikuu vya Zanzibar.

Aidha, Dk. Shein alimueleza Balozi huyo azma ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kukuza sekta zake za maendeleo ikiwemo sekta ya kilimo ambayo alisema ushirikiano wa kitaalamu unahitajika katika sekta hiyo kwa pande mbili hizo.

Kwa upande wa sekta ya biashara, Dk. Shein alisema kuwa wafanyabiashara wengi wa Malawi wamekuwa wakifanya biashara zao nchi Tanzania na kusisitiza haja ya wafanyabiashara hao kuja Zanzibar kwa ajili ya kufanya biashara ya viungo ambavyo itakuwa ni kivutio kikubwa kwa watalii kutoka nchini humo.

Mbali na ushirikiano katika sekta za maendeleo pia, Dk. Shein alieleza kuwa kutokana na wananchi wa pande mbili hizo kushabihiana kiutamaduni kuna haja ya kushirikiana katika kukuza sekta hiyo.

Nae Balozi Hawa, alimpongeza Dk. Shein pamoja na Serikali anayoiongoza kwa mafanikio makubwa yaliopatikana hapa Zanzibar na kumueleza kuwa Malawi ina mambo mengi ya kujifunza kutoka kwa ndugu zao wa Zanzibar.

Balozi Hawa alieleza kuwa Malawi inathamini uhusiano na ushirikiano wa kihistoria kati ya nchi hiyo na Zanzibar tokea wakati wa Waasisi wa pande mbili hizo na kuahidi kuwa hatua hiyo itaimarishwa na kuendelezwa.

Pamoja na hayo, Balozi Hawa alimueleza Dk. Shein kuwa mbali ya azma ya nchi yake ya kuendeleza uhusiano na ushirikiano katika sekta za maendeleo ikiwemo kilimo, elimu, biashara, utamaduni na nyenginezo pia, Malawi itapata fursa ya kupanua wigo kwenye sekta ya utalii ambayo kwa Zanzibar tayari imeshapiga hatua.
Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 
 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.