Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein akisalimiana na Balozi Mteule wa wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Burundi Mhe,Rajab Gamala alipofika Ikulu Mjini Zanzibar kujitambulisha jana,[Picha na Ikulu.]
STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar
12.6.2015

RAIS wa
Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesema
kuwa Zanzibar imekuwa na uhusiano na mashirikiano mazuri na nchi za Maziwa Makuu hivyo ipo haja ya kuimarisha
hatua hiyo kwa kuendelea kuutangaza utalii wa Zanzibar katika nchi hizo.
Dk. Shein
aliyasema hayo leo, huko Ikulu mjini Zanzibar wakati alipofanya mazungumzo na
Balozi Mteule wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Burundi Mhe. Rajab Hassan
Gamaha ambaye alifika Ikulu kwa ajili ya kuaga na kupata baraka za Rais.
Katika mazungumzo
hayo, Dk. Shein alimueleza Balozi huyo kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
imechukua juhudi kubwa za kuiimarisha sekta ya utalii hapa nchini sambamba na
kuimarisha vivutio vyake kwa wageni kutoka nchi mbali mbali duniani zikiwemo nchi za Maziwa Makuu kama vile
Burundi.
Dk. Shein alieleza
kuwa ni imani yake kubwa kuwa migogoro iliyopo nchini humo hivi sasa itamalizika
kwa msaada mkubwa wa viongozi wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki ambao
wamekuwa wakichuku juhudi za makusudi za kuhakikisha migogoro iliyopo nchini
humo inamalizika.
Alisema kuwa
kuteuliwa kwa Balozi huyo kuiwakilisha Tanzania nchini humo ni hatua moja wapo
ya Tanzania kuendelea kuimarisha uhusiano na ushirikiano wa kidugu, kidamu na
kimipaka na Burundi.
Dk. Shein alisema
kuwa hivi sasa wananchi walio wengi wa Burundi wameanza kujifunza lugha ya
Kiswahili na Zanzibar ni sehemu yenye asili ya lugha hiyo, hivyo ipo haja ya
kuwashajiisha wananchi wa Burundi kuja Zanzibar kujifunza lugha hiyo kwenye
Chuo chake Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA).
Katika maelezo
yake Dk. Shein alisema kuwa heshima ya Tanzania nchini Burundi ni kubwa
sana hivyo ipo haja ya kuendeleza
uhusiano na ushirikiano wa muda mrefu uliopo kati ya pande mbili hizo.
Kutokana na hatua
hiyo, Dk. Shein alisisitiza kuwa kuna kila sababu za kuimarisha uhusiano na
kiuchumi hasa katika uwekezaji kati ya Tanzania na Burundi kwa kuangalia zaidi
fursa ziliopo nchini hasa kwa upande wa Zanzibar katika sekta ya utalii na hata
sekta ya biashara.
Aidha, Dk. Shein
alitumia fursa hiyo kumueleza Balozi Gamaha kuwa wakati ukifika Zanzibar
itafanya uchaguzi wake ulio huru na haki huku akieleza matumaini yake kuwa
viongozi wa vyama vya siasa watafuata matakwa ya Serikali katika kusimamia
amani na utulivu.
Nae Mhe. Rajab Hassan Gamaha, Balozi Mteule wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Burundi alieleza kuwa katika utendaji
wake wa kazi nchini humo atahakikisha uhusiano na ushirikiabno kati ya Tanzania
na Burundi unaumarika zaidi.
Balozi huyo nae
alieleza matumaini yake kuwa nchi hiyo itafika siku itarejea katika hali yake
ya amani na utulifu kutokana na juuhudi zinazochukuliwa na viongozi wa Afrika
Mashariki katika kutatua migogoro nchini humo.
Balozi Gamaha,
alisema kuwa wananchi wa Barundi na Tanzania wamekuwa na uhusiano na
ushirikiano wa muda mrefu kwani tayari wapo baadhi ya Watanzania ambao
wameekeza nchini Burundi pamoja na wengine wanaofanya biashara nchini humo.
Sambamba na hayo,
Balozi huyo Mteule alimuhakikishia Dk. Shein kuwa atahakikisha anafanya kazi
zake kwa uaminifu na bidii kubwa huku akiiombea Tanzania na Zanzibar kwa jumla
kufanya uchaguzi mkuu ujao kwa amani na utulivu.
Aidha, Balozi
Gamaha alieleza kuwa Sekta ya Utalii aghalabu huendana na sekta ya biashara
hivyo kuimarika kwa sekta ya biashara kati ya Burundi na Tanzania ikiwemo
Zanzibar kutasaidia kwa kiasi kikubwa kupanua soko la utalii la Zanzibar.
Alieleza
matumaini yake kuwa sekta ya utalii inaweza kuimarika zaidi hapa Zanzibar
kutokana na soko la nchi za Maziwa Makuu ikiwemo Burundi.
Balozi Rajab
Gamaha ameshawahi kuwa Balozi wa Tanzania nchini Uganda kabla ya kuwa Naibu
Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Gamaha anachukua
nafasi ya Balozi Dk. Mwasi Nzagi ambaye amestaafu kwa mujibu wa Sheria.
Rajab Mkasaba, Ikulu
Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024
2231822
E-mail:
rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment