Na Maryam Kidiko – Maelezo Zanzibar.
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeamua kutengeneza Meli mpya ya Abiria MV Mapinduzi 11 pamoja na mizigo Nchini Korea ili kuwapatia usafiri wa uhakika wa Baharini kwa Wananchi wa Visiwa vya Unguja na Pemba.
Hayo yameeleza leo na Naibu wa Miundombinu na Mawasiliano Issa Haji Ussi huko Baraza la Wawakilishi linaloendelea Chukwani Nje kidogo wa Mji wa Zanzibar wakati akijibu suala la Muwakilishi Salim Abdallah Hamadi wa Jimbo la Mtabwe aliyetaka kujua Meli hiyo inatarajiwa kugharimu kiasi gani.
Amesema mradi wa ujenzi wa Meli ya Serikali itagharimu jumla ya Dola za Kimarekani USD 30,825,000 ikiwemo malipo ya Msimamizi wa Ujenzi wa Meli hiyo.
Aidha amefahamisha kuwa jumla ya USD 37,000 zitatumika katika gharama ya safari ya Viongozi wa Serikali pamoja na wanasiasa waliopata fursa ya kusafiri Nchini Korea ya kusini .
Hata hivyo ameeleza kuwa safari za Viongozi hao wa Serikali,Wanasiasa na Watendaji wa Serikali zimegharamia kupitia Bajeti za Wizara na Taasisi zenye dhamana ya utekelezaji wa mradi huo.
Vilevile amefahamisha kuwa kulifanyika vikao vya maendeleo ya mradi (Progress Meetings) ambapo mambo mbali mbali yanayohusu utekelezaji wa mradi yamejadiliwa na kuzipatia ufumbuzi changamoto zilizojitokeza katika utekelezaji wa mradi kabla ya kuruhusu kazi nyengine za mradi huo kuendelea.
Naibu huyo amesema kwa mujibu wa ratiba ya ujenzi wa Meli hiyo tukio linalofuata la majaribio la Meli Baharini linawahusu Mabahari wanaopatiwa mafunzo ya uwendeshaji wa Meli hiyo na kuileta Nchini.
No comments:
Post a Comment