Habari za Punde

Mwenyekiti wa AFP Said Soud Alaani Kitendo cha CUF Kutoka katika Kikao cha Bajeti

Na Maryam Kidiko / Mwashungi Tahir-Maelezo Zanzibar           .

Chama cha  Wakulima ( A.F.P.) wamesikitishwa na kitendo cha wawakilishi wa Chama cha Wananchi (CUF) kutoka nje  ya kikao cha Baraza la Wawakilishi  ambacho kilikuwa  kikijadili mswada wa kupitisha matumizi ya Serikali kwa mwaka 2015/2016.

Akizungumza na Waandishi wa habari katika Ukumbi wa Habari Maelezo Zanzibar Mwenyekiti wa chama hicho Said Soud Said amesema Chama cha CUF ni sehemu ya Serikali hivyo hawapaswi kufanya kitendo hicho.

Amesema chama hicho  kimelaani vibaya kitendo hicho kwa chama cha CUF kwani kimeweza  kuonesha picha mbaya   katika Baraza la Wawakilishi kwakuwa wao ni Viongozi wakuu katika Serikali ya Mapinduzi hawakupaswa kuchukua hatua hiyo ambayo imewaacha jamii katika hali ngumu.

Aidha amesema  kitendo hicho kimelaaniwa na kila  mwananchi mpenda maendeleo  na ambae  anaumwa na nchi hii  na pia inaonyesha dhahiri kuwa CUF hawawezi kuongoza pindi wakipata madaraka.

“Wazanzibar hawajazowea fujo kwani wamezowea kuwa nchi hii kuwa na amani na utulivu ambayo ni thamani yetu tunojivunia hapa nchini” alisema mwenyekiti huyo.

Pia aliitaka Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kujenga Viwanda mbalimbali ili Vijana ambao waliomaliza elimu wapate ajira katika Viwanda hivyo.

Vile vile alimuomba Rais wa Zanzibar atumie busara na hekma ili uvunjifu wa amani usijetokea katika nchi hii ya Zanzibar na kwa wale ambao wanaotaka kuharibu amani ya Nchi wachukuliwe hatuwa za kisheria mara moja.

Sambamba na hayo amesema Wananchi wapatiwe elimu ya uraia ili waepuke tabia ya kuendeshwa na watu wasiotaka maendeleo ya Nchi.

                                        MWISHO.
                       IMETOLEWA NA MAELEZO ZANZIBAR.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.