Na Haji Nassor, Pemba
BAADA ya gazeti hili, kuchapisha
habari juu ya wahamiaji wasio rasmi kuzitumia bandari bubu kuingia na kutoka nchini,
sasa Idara ya Uhamiaji Zanzibar, imeibuka na kutaka kudhibiti bandari hizo kwa
kushirikiana na vikosi vya ulinzi na usalama.
Wakati
hayo yakijiri kwa upande wao wananchi wanaoishi ukanda wa bahari ya hindi
Kisiwani Pemba, wameahidi kushirikiana na Idara ya uhamiaji juu ya wazo lake la
kuimarisha ulinzi katika bandari hizo.
Walisema kwa muda mrefu Idara hiyo imekuwa
imesahau wajibu wake wa kushisirikia vikosi mbali mbali vikiwemo vya SMZ na
wananchi husika, jambo ambalo lililosababisha uingiaji wa wageni kwa wingi
kupitia bandari hizo.
Wakizungumza
na mwandishi wa habari hizi kwa nyakati tofauti, wananchi hao walisema, suala
la kudhibiti wahamiaji wasio rasmi, linapaswa kwa idara tofauti kushirikiani
ikiwemo ya Uhamiaji, KMKM, masheha na wananchi husika wakiwemo wavuvi.
Walisema
kama sasa Idara ya uhamiaji imeshajipanga na hilo, wao kama wananchi wako tayari
maana athari ya wageni kutumia bandari bubu kuingia na kutoka ndani ya visiwa
vya Unguja na Pemba humpata kila mmoja.
Mmoja
wa wananchi hao Ali Khamis Haji wa shehia ya Ziwani Chake chake, alisema ni
vyema kwa Idara hiyo kwanza kukaa na wananchi kwa kuwapa mbinu mwafaka ili
kutoa taarifa pale wanapowashuhudia.
“Unajua
sisi kama wananchi hatupendi kuona wageni, lakini hatuna elimu ya kujua
tuzifikishe wapi taarifa husika, ambapo watachukua hatua thabiti’’,alisema.
Nae
Hamad Kombo Mjaka wa shehia ya Gando alisema, wakati umefika kwa Idara ya
uhamiaji kuziacha ofisi na kufika kwa wananchi hasa wanaoishi karibu na bandari
bubu, ili kukaa nao na kuwapa maelekezo ya kitalaamu.
Kwa
upande wake Hassan Juma Hassan wa Kangani Mkoani, alisema kutokana na uwingi wa
bandari bubu uliopo Zanzibar, ni vyema kwa Idara hiyo sasa kuwa karibu na KMKM
pamoja na wananchi wengine.
“Mbona
magendo ya karafuu yamepungua sana na yalikuwa sugu, sasa hata wageni
wanaoingia kwa kutumia bandari bubu wanaweza kukoma kama Idara hiyo
ikishirikiana na wananchi’’,alifafanua.
Hivi
karibuni afisa uhusiano wa Idara ya uhamiaji Zanzibar Muhsin Abdalla
alinukuliwa na vyombo vya habari, kwamba wanatarajia kushirikiana na vyombo
vyengine vya ulinzi, pamoja na masheha ili kuweka ulinzi maalumu kwenye bandari
bubu ili kudhibiti wahamiaji wasio rasmi.
Uhamiaji
ilisema kuelekea uchaguzi mkuu, na hata badae ni vyema nchi ikawa shuwari na
hasa baada ya kuwepo taarifa kwamba bandari bubu zinatumiwa na wageni kwa lengo
la kujiandikisha na kwa ajili ya uchaguzi mkuu.
Kwa
upande wake afisa uhamiaji wilaya ya Mkoani Pemba Abdalla Shehe alisema suala
la bandari bubu limezagaa na wakati umefika kwa jamii kushirikiana na taasisi
husika.
“Hata
wilaya yangu ya Mkoani, bandari bubu zipo na zimekuwa zikitumika vibaya kwa
kupitia wahalifu na hata kutoroshea mazao ya taifa’’,alifafanua.
Mei
15 na 16 mwaka huu, gazeti hili lilitoa habari juu ya uwepo kwa bandari bubu
zaidi ya 500 kisiwani Pemba, ambapo wahamiaji wasio rasmi huzitumia na wahalifu
kutoka au kuingia kukimbia mkono wa sheria.
Katika
habari hizo, zileleza kuwa ukosefu wa walinzi wa kutosha, kutokuwepo kwa
ushirikiano baina ya vikosi vya ulinzi na wananchi kukosa uzalendo ndio sababu
za bandari hizo kutumika kiholela.
Bandari
bubu hapa visiwani zimekuwa zikitumiwa kama kawaida na baadhi ya wavuvi na
wasafiriahaji magendo kama ya karafuu na kubainika kuwa pia wakati mwengine
kuwatorosha wahalifu au kuwaingiza.
No comments:
Post a Comment