Habari za Punde

Balozi Seif afutari na watoto yatima Dodoma

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akitoa sadaka kwa Watoto Yatima wa kiumewa Kituo cha Kulelea Watoto Yatima cha Rahman kiliopo Chang’ombe Mjini Dodoma hapo kwenye makazi yake Mtaa wa Farahani Mjini Dodoma. Kulia ya Balozi Seif Ali Iddi ni Mkewe Mama Asha Suleiman Iddi.
Balozi Seif Ali Iddi akitoa sadaka kwa Watoto Yatima wa Kike wa Kituo cha Kulelea Watoto Yatima cha Rahman kiliopo Chang’ombe Mjini Dodoma baada ya kufutari nao pamoja.
Baadhi ya Watoto Yatima wa Kituo cha Kulelea watoto Yatima cha Rahman kiliopo Chang’ombe Mjini Dodoma wakipata futari ya pamoja iliyoandaliwa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif katika Makaazi yake yaliyopo Mtaa wa Farahani Mjini Dodoma.Picha na – OMR – ZNZ.


Na Othman Khamis Ame, OMPR
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amesisitiza umuhimu wa Waumini wa Dini ya Kiislamu kuendelea kujenga utamaduni wa kufutari pamoja ili kudumisha utaratibu uliotiliwa nguvu na Kiongozi wa Dini hiyo Mtume Muhammad { SAW } na kuendelezwa na maswahaba waliomfuata.

 Balozi Seif ametoa sisitizo hilo kwenye hafla ya Futari ya pamoja aliyowaandalia Watoto Yatima wanaolelewa katika Kituo cha malezi ya Watoto yatima cha Kiislamu cha Rahman Kiliopo Chang’ombe Mjini Dodoma.


Futari hiyo ambayo pia ilihudhuriwa na baadhi ya viongozi wa Dini ya Kiislamu wa Mji wa Dodoma wakiambatana na baadhi ya Viongozi wa Serikali na Kisiasa ilifanyika katika Makazi yake yaliyopo Mtaa wa Farahani Mjini Dodoma.


Balozi Seif alisema mijumuiko hiyo ya waislamu mara kadhaa husaidia kuongeza upendo, ushirikiano na mahaba baina yao jambo ambalo huongeza nguvu za pamoja katika jitihada zao za kusimamisha Dini ya Mwenyezi

Muungu.


Akiwapatia  sadaka katika kujiandaa  kusherehekea siku kuu ya Iddi El - Fitri wanafunzi hao wa Chuo cha Malezi ya Kiislamu ya watoto Yatima cha Rahman Balozi Seif aliwaombea kusherehekea siku kuu hiyo kwa
amani,salama na upendo.



Akitoa shukrani kwa niaba ya waalikwa wa futari hiyo Sheikh Shaaban Kitila wa Masjid Nunge alimpongeza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif kwa ukarimu wake wa kuwakusanya wauminbi wenzake kwenye futari ya pamoja.



Sheikh Kitile alisema kufutarisha ni jambo la sunna lililosisitizwa na Mtume Muhammad { SAW } linalotoa nafasi kwa waumini wa dini ya Kiislamu wasio na uwezo kupata futari inayoleta faraja kwao. Kituo cha Kulelea Watoto Yatima cha Rahman kinachosimamiwa na Ustaadhat Rukia Khamis { Maarufu Mama Abdullah } kimeanzishwa mwaka
2007 kikiwa na wanafunzi 20 ambapo hivi sasa kinahudumia watoto yatima wapatao 70.



Balozi Seif amejiwekea utaratibu wa kufutari pamoja na Watoto hao wa Kituo cha kulelea Watoto yatima Mjini Dodoma napokuwa katika shughuli zake za kikazi akiwa Mjini Humo ndani ya Mfungo wa mwezi mtukufu wa
Ramadhani.

Wakati Kumi la Pili ya Maghfira likimalizika na kuingia kumi la Mwisho la Kuachwa huru na Moto ndani ya Mfungo wa mwezi Mtukufu wa Radhani waumini wa Dini ya Kiislamu wamekuwa wakiendelea kujumuika katika

futari ya pamoja katika maeneo mbali mbali hapa Nchini.

2 comments:

  1. Wewe kiongozi wa ngazi za juu, tena ni Balozi wa siku nyingi, kwa nini unawapa cash watoto kwenye vijibahasha? Huoni kama unawazoesha tabia mbaya hao watoto? Tunajua hizo pesa hazina thamani kwako, kwa vile zimejujaa bwerere.

    Kwa nini hizo pesa usiwape kwa kupitia kwenye mfuko wa kituo chao. Kwa kweli sielewi kwa nini uwape kama mtindo wa zawadi vile? Huo sio uandilifu na wala sio dini, bali ni kinyume chake. Hio kiislamu inaitwa Ria, au kujionyesha, kitu ambacho ni kiovu katika Uislaam. Inakera

    ReplyDelete
  2. Ndugu yangu, acha kuchanganya dini na siasa!

    "Inna mal aghmaly, bin- nniyyah"

    Wakati waumini wa kawaida huftarisha na kutoa sadaka kwa kutafuta fadhila za ramadhani, wanasiasa ni tofauit, zaidi wao hutafuta umaarufu wa kisiasa, sasa kuna ubaya gani kwa Balozi kufanya hivyo?

    Ndio maana baadhi ya watu hufikia hata kusema kua siasa yenyewe ni Dini ambayo ni tofauti na Uislamu unao ujua wewe, na ndio maana si ajabu leo hii, UNAWEZA KUKUTA MWANASIASA ANAAMRISHA WATU KUPIGWA Mchana wa Ramadhani, halafu usiku anaftarisha!

    ReplyDelete

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.