Habari za Punde

Tamko la Mikoa Minne ya CCM Unguja Dhidi ya Waziri Mkuu Mstaaf Mhe Edward Lowassa.

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
(PRESS RELEASE)

Katibu wa CCM Wilaya ya Mjini Ndg Mohammed Omar Nyawanga akisoma Tamko la Mikoa Mnne ya CCM Unguja kuhusuana na Mhe Edward Lowassa. kwa Waandishi wa habari na Makada wa CCM Afisi Kuu ya CCM Zanzibar leo. 

NDUGU WANAHABARI!
WANACHAMA NA MAKADA WENZANGU WA CCM!
ASALAM ALEYKUM!
Awali ya yote, kwa niaba ya Wanachama na Makada wenzangu tuliokusanyika hapa leo, ninapenda kuchukua fursa hii kumshukuru Molla wetu mtukufu mwingi wa rehemu kwa ukarimu wake na kutujaalia afya njema na uwezo wa kukutana nanyi hapa leo.  Pili ninapenda kuwashukuru kwa dhati Wahariri na Wanahabari kutoka Vyombo mbali mbali vya Habari vya hapa Zanzibar, kwa kukubali kuitika wito wetu huu maalumu.
Sisi tuliowaita hapa ni Wanachama na Makada wa CCM.  Baadhi yetu ni viongozi wa CCM wa ngazi mbali mbali za Chama, wakiwemo Wajumbe wa Halmashauri Kuu za CCM za Wilaya, Mikoa na Taifa. Kwa kuzingatia nasabu yetu hio, ndio maana mkutano huu tumeamua kuufanyia katika jengo letu hili la Afisi Kuu ya CCM Zanzibar.
Lengo kubwa la kuwaiteni hapa leo, ni kuwaelezea hisia na msimamo wetu kama wanachama na viongozi wa CCM ambao kwa kuzingatia wajibu na majukumu tuliyonayo katika Chama, sisi ndio wasimamizi wakuu wa Siasa, Sera na Itikadi ya CCM hapa Zanzibar.
Hivyo basi, kwa kuzingatia hali ya Kisiasa iliyojiri hapa nchini, tangu kumalizika kwa Mkutano Mkuu Maalumuwa CCM wa Taifa uliofanyika tarehe 12 na 13/7/2015 mjini Dodoma, na kumchagua Mhe. Dk. John Pombe Joseph Magufuli kuwa mgombea wa CCM wa Kiti cha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kumthibitisha Mhe. Samia Suluhu Hassan kuwa mgombea mwenza na uhusika wetu katika maamuzi hayo ya Chama, tumeona ipo haja na umuhimu mkubwa wa kuitisha mkutano huu na kupitia kwenu kuwaeleza wanachama wenzetu wa CCM na Watanzania kwa jumla, hisia na muono wetu juu ya mustakabali wa Chama chetu na hatima ya Taifa letu.
Kama tunavyofahamu mapema mwezi Mei 2015, Chama chetu kilitangaza ratiba ya mchakato wa uteuzi wa wagombea wa CCM katika chaguzi za Vyombo vya Dola.  Ratiba hio ilihusu uteuzi wa mgombea wa kiti cha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Wabunge, Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar pamoja na Madiwani.
Mchakato wa uteuzi wa wagombea wa CCM wa Kiti cha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Rais wa Zanzibar, ulianza tarehe 3/6/2015 hadi 2/7/2015, kwa wanachama kuchukua na kuresha fomu za maombi.  Baada ya hapo vikao vya uchujaji vilianza kuanzia tarehe 4/7/2015 na kumalizika tarehe 13/7/2015.  Jumla ya Wanachama wa CCM 42 walijitokeza kuchukua fomu za maombi na kati yao 38 walifanikiwa kukamilisha masharti yaliyotakiwa na kurejesha.  Miongoni mwao walikuwemo Makamu wa Rais, Waziri Mkuu, Mawaziri Wakuu Wastaafu, Mawaziri, Majaji Wakuu Wastaafu, Mabalozi,  Mawaziri na hata wanachama wa CCM wa kawaida tu (wakulima, wafugaji n.k).
Kwa kuzingatia Katiba na Kanuni za Chama chetu, kikao cha kwanza kabisa cha uchujaji wa wagombea ni Kamati ya Usalama na Maadili ya ngazi husika.  Hivyo, kwa wagombea wa Kiti cha Rais, Kamati ya Usalama na Maadili ya Taifa ndicho chombo cha kwanza kabisa chenye wajibu wa kuchambua kwa makini ubora wa wanachama wanaoomba Uongozi, ama viongozi wanaoteuliwa katika ngazi mbali mbali za Chama, kabla vikao vinavyohusika havijatoa idhini ya kuwaruhusu wateuliwe kugombea uongozi huo ama kushika nafasi zilizo kusudiwa.
Kikao cha pili ni Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM ya Taifa, ambayo chini ya ibara ya 119(6)(b) ya Katiba ya CCM ya mwaka 1977, Toleo la 2012, imepewa jukumu la kufikiria na kutoa mapendekezo yake kwa Halmashauri Kuu ya CCM ya Taifa juu ya majina ya wanachama wasiozidi watano wanaoomba kugombea kiti cha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Ndugu Wanahabari!
          Tumelazimika kuvinukuu vifungu hivyo vya Katiba na Kanuni ya Uongozi na Maadili ya CCM, kwa sababu huo ndio msingi uliofuatwa na Chama chetu katika uteuzi wa Wagombea wa Kiti cha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kinyume na maelezo ya baadhi ya watu wasioitakia mema CCM na kwa kuzingatia maslahi yao binafsi wanataka kuwaaminisha Watanzania kwamba, mchakato huo uligubikwa na mizengwe, chuki na kila aina ya ubabaishaji, jambo ambalo sio la kweli.
          Tunayasema haya sio kwa ushabiki wala kushawishiwa na mtu au kiongozi yeyote wa CCM.  Bali ukweli ni kwamba sisi wenyewe tulikua sehemu ya mchakato huo na tulishiriki katika kila hatua ya utekelezaji.  Na kama ni kushawishiwa basi baadhi yetu tulishawishiwa kumuunga mkono huyo ambaye leo analalamika kuwa, CCM haikumtendea haki.  Sio siri, baadhi yetu tulikubali kumsaidia na kufanya kampeni kubwa ya kuwaomba wanachama wenzetu wa CCM wakubali kumdhamini katika Mikoa mbali mbali ya nchi yetu.  Tulifanya hivyo tukifahamu vyema matakwa ya Katiba na Kanuni za Chama chetu  kwamba, mwisho wa siku vikao halali vya Chama ndio vyenye wajibu na mamlaka ya kufanya maamuzi kwa kuzingatia Katiba na Kanuni za Chama chetu.
Hata hivyo, wengi hapa hatujashangazwa hata kidogo na kwa kweli tulitegemea kuona kile kilichotokea tarehe 28/7/2015  kwa ndugu yetu Waziri Mkuu wa zamani, Kada na Kiongozi wa muda mrefu wa CCM Edward Ngoyai Lowassa, kujitoa katika CCM na kujiunga na Chama cha upinzani cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kwa madai kwamba, CCM imeuonea na haikumtendea haki! 
Tunasema hivyo kwa sababu tulianza kupata mashaka pale tuliposikia kauli zake wakati akijibu maswali ya baadhi ya Waandishi wa habari kwamba, katika mchakato wa uteuzi wa mgombea wa CCM wa Kiti cha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ndani ya Chama, kwa upande wake hakuna kushindwa wala kikao chenye uwezo wa kukata jina lake.  Kimsingi, kauli hio sio tu ni ya kukidhalilisha Chama chetu bali vile vile ni uasi!  Kwani ndugu Lowassa anafahamu vyema wajibu wa mwanaCCM na mamlaka ya kila kikao ndani ya Chama.  Iweje leo atamke tena hadharani kwamba, CCM ni lazima imteue yeye kuwa mgombea wake na hakuna mwanachama mwengine ye yotemwenye  sifawala uwezo wa kumudu kuliongoza Taifa letu zaidi ya yeye tu peke yake!
Aidha, ni jambo la ajabu sana kuona kuwa, wale waliokua maadui zake wakubwa kisiasa,wakiwemo Viongozi Wakuu wa Vyama vya upinzani ambao walizunguka ndani na nje ya nchi kulichafua jina lake na CCM, leo hii bila haya wala soni ndio wanaosimama mbele ya Vyombo vya Habari na kupaza sauti zao eti CCM imemuonea na kumdhalilisha Lowassa!  Kama hio haitoshi, wapo wale wanaodiriki kututisha, eti nyuma yake lipo kundi kubwa la wanaCCM ambao wapo tayari kumfuata popote pale aendapo.
Ili kujibu madai hayo, na kwa kupitia kwenu Waandishi wa Habari, tunapenda kutumia fursa hii kumueleza ndugu Edward Ngonyai  Lowassa pamoja na wote wanaomuunga mkono hususan Viongozi na wanachama wa UKAWA, kwamba:-
a)    Sisi wote tuliyopo hapa leo na maelfu ya wanaCCM waliyo nyuma yetu hususan katika Mikoa yote ya Zanzibar, tulimuunga mkono Lowassa katika azma yake ya kuomba kuteuliwa na CCM kuwa mgombea wake wa Kiti cha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, sio kwa sababu ya uzuri wa suara yake au utajiri alionao hapana! Bali ni kwa sababu ya Siasa, Sera na Ilani ya Chama alichokiamini na kukipigania, yaani CCM.  Hivyo, kwa kuwa sasa ameamua kujitenga na CCM, basi nasi tumeamua kujitenga naye na kamwe hatuko pamoja naye.
b)    CCM ni muumini wa Haki za Binadamu, usawa na utawala wa sheria.  Hivyo, kujiondoa kwa Lowassa katika CCM ni sawa na ilivyokua wakati wa kujiunga kwake.  Ni suala la hiari yake na wala hatuna ugomvi naye.  Ila tunamkumbusha tu kwamba, inawezekana kabisa umaarufu alionao sasa umejengwa kutokana na CCM, lakini haiwezekani kabisa kuwa, umaarufu wa CCM umejengwa au kutokana na yeye.  Ndio maana tunasema, Chama kwanza mtu baadae”.
c)     CCM ni Chama chenye mamilioni ya wanachama na maelfu ya viongozi, wenye hekima, busara, mapenzi na uadilifu mkubwa kwa wananchi.  Bado kinaamiwa  na kukubalika miongoni mwa wananchi wengi wa Tanzania.  Wingi huo wa wanachama wake haitokani na wala haujaletwa na utajiri wa Viongozi wake.  Bali unatokana na uimara wa Siasa, Sera na Itikadi yake.,  Hivyo, hasara ya kweli kwa CCM sio kumpoteza tajiri mmoja anaetaka kubadili Sera na Itikadi ya CCM kwa maslahi yake binafsi na marafiki zake, bali ni kuwapoteza mamilioni ya wanachama wake ambao wanachoshwa na viongozi walafi na wanafiki ndani ya CCM!
d)    Kwa kuzingatia ukweli huo ni wazi kwamba, uamuzi wa Lowassa kujiondoa ndani ya CCM sio jambo la kukishtua Chama chetu, viongozi wala wanachama wake.  CCM kamwe haiwezi kudhoofika wala kupasuka.  Aidha, hii sio mara ya kwanza kwa CCM kuondokewa na Kiongozi Mwandamizi na kujiunga upinzani.  Mwaka 1989, CCM iliwafukuza uanachama jumla ya viongozi waandamizi 11 akiwemo Waziri Kiongozi Mstaafu wa Zanzibar, Seif Shariff Hamad.  Akafuatia Agostino Lyatonga Mrema, ambaye alijiunga  na NCCR-Mageuzi. Mwaka jana 2014, CCM ilimfukuza uanachama aliyekua Mwakilishi wa Jimbo la Kiembesamaki kwa tiketi ya CCM Mansoor Yussuf Himid.  Hivyo, kama wahenga walivyonena tunamuambia Lowassa, “Kama mvuvi wa pweza tukutane mwambani” !
e)    Tunawashangaa sana Viongozi wa baadhi ya Vyama vya Upinzani hasa vile vinavyounda umoja wa UKAWA na hususan Viongozi na Wanachama wa CHADEMA kwa namna wanavyoendelea kuendesha Siasa za ubabaishaji na ulaghai kwa Watanzania.  Kwa hakika ni jambo la aibu na kufedhehesha sana kuona kwamba, hata baada kufikisha umri wa miaka 23, tangu kuanzishwa rasmi kwa Vyama vya Upinzani hapa nchini (1992), bado Vyama hivyo hadi leo hii vimeshindwa kuandaa wagombea wenye uwezo wa kuwaongoza Watanzania na kuishia kudaka mapumba yanayotoka CCM?Mara nyingi tumewasikia wakijitoa kimasomaso kwakukariri nusu nusu kauli ya Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius K. Nyerere kwamba, “Watanzania wanahitaji mabadiliko na wasipoyapata ndani ya CCM watayafuata nje ya CCM”.  Kwa bahati mbaya sana wasia huo wa Baba wa Taifa unakaririwa nusu nusu.Naomba  kuwakumbushaViongozi wa UKAWA kwamba, Wasia huo wa Baba wa Taifa kwa Watanzania unaendelea kwa kutamka kwamba “Rais wa Tanzania anaweza kutoka Chama cho chote kile, lakini Rais bora wa nchi yetu atatoka CCM!

Mwisho kabisa, ninapenda nimalizie kwa kumpongeza sana Mhe. Dk. John Pombe Joseph Magufuli kwa kuteuliwa kuwa mgombea wa CCM wa kiti cha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kuteuliwa kuwa mgombea mwenza, pamoja na wanachama wengine wote waliojitokeza kutangaza nia hatimaye kuchukua fomu za kuomba kuteuliwa kugombea nafasi ya kiti cha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa heshima kubwa waliyoipatia CCM na kubwa zaidi kwa kukubali kupokea bila kinyongo maamuzi ya Chama na kudumisha umoja na mshikamano miongoni mwa wanaCCM.


                   KIDUMU CHAMA CHA MAPINDUZI !

5 comments:

  1. Tunaheshimu sana maoni na mitazamo yenu wana-ccm na watanzania wenzetu kutoka unguja lakini hata hivyo, mnapaswa kuelewa mambo yafuatayo:

    1) Pamoja na kwamba ccm ni moja na itikadi ya chama chetu ni moja lakni bado kuna tofauti nyingi za mitazamo kati ya ccm visiwani na huku bara.

    Nguvu ndogo ya ccm visiwani pamoja na upinzani unaowakabili hamuwezi kuhoji hata kama demokrasia haikutendeka katika chama...ianabidi mkubali tu!

    Jengine ni hali ya kiuchumi ya visiwani namna ilivyo ni ngumu kuishi bila kuwa mw'chama ccm au kufanyakazi serikalini ila huku ni tofauti!

    Ukweli ni kwamba ccm haikumtendea haki mhe Lowassa na uwamuzi wake wa kuhama chama ni sahihi hata kama hatashinda urais lakini itasidia kupanua demokrasia ya nchi yetu.

    Naamini ccm-bara ni tofauti na huko visiwani lazima wataungalia upya utaratibu wa kuchagua wagombea ktk chama siku za mbele ili kuhofia madhara kama itayosababisha lowassa mwaka huu!

    ReplyDelete
  2. hivi hiyo haki ya lowasa peke yake ni haki ipi iyo?na huko ikulu anakolazimisha kwenda anabiashara gani huko?

    ReplyDelete
    Replies
    1. waacheni hao,wanajuwana kinagaubaga,mengi mno tusiyoelewa kiuongozi yanaendelea.Swali la kujiuliza itakuwa mpaka lini????

      Delete
  3. Ccm mmeishiea sera mnatapata baharini, mmeshazama kabisa

    ReplyDelete
  4. Ccm imejichimbia kaburi

    ReplyDelete

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.