MENEJA wa Kilimo katika shirika la kuimarisha maisha kupitia maendeleo ya kilimo na mifugo BRAC Tanzania Joseph Mabula, akitoa mada katika warsha ya uwezeshaji mnyororo wa thamani wa zao la mahindi kwa wadau wa zao hilo Zanzibar, iliyofanyika katika ukumbi wa Wizara ya Afya Mombasa gereji Unguja.
Maelezo, Zanzibar
SHIRIKA la BRAC Maendeleo Tanzania linaloendesha mradi wa kuwaendeleza wadau wa zao la mahindi na ufugaji kuku, limewataka wadau hao kuunda mtandao utakaowawezesha kuongeza thamani ya zao hilo na kuwaletea tija zaidi.
Akitoa mafunzo katika warsha ya uwezeshaji mnyororo wa thamani wa zao la mahindi iliyofanyika katika ukumbi wa Wizara ya Afya Mombasa gereji, Meneja wa kilimo katika shirika la kuimarisha maisha kupitia maendeleo ya kilimo na mifugo (BRAC) Joseph Mabula, alisema zao la mahindi lina nafasi kubwa ya kuinua kipato cha wadau.
Hata hivyo alisema hilo litawezekana endapo wadau wa zao hilo kuanzia wakulima, wasagishaji, wasambazaji na wauzaji mahindi makavu na mabichi, watazingatia utaalamu na kushirikiana katika kuliendeleza zao hilo.
Alieleza kuwa, shirika la BRAC kupitia mradi wa 'LEAD' wa miaka minne, unaodhaminiwa na shirika la maendeleo la serikali ya Uingereza (UK AID), linalenga kuwainua wakulima wadogo wadogo wa mahindi na wafugaji wa kuku waishio vijijini.
Aidha alitaja lengo jengine la mradi huo ni kuwaongezea wakulima wa mahindi uwezo wa uzalishaji wenye tija na faida ili kuongeza kipato cha familia na ajira vijijini.
Alieleza kuwa, katika nchi ya Bangladesh ambako shirika hilo lilanzishwa, BRAC ipo kwenye wilaya zote 64 za nchi hiyo ikiwa na zaidi ya vikundi milioni tano vya wanajumuiya wa mikopo midogo midogo.
Aidha alisema huko Bangladesh, shirika lina skuli za msingi na maandalizi zisizo rasmi zaidi ya 370,000, maofisa wa afya wa kujitolea zaidi ya 70,000 na idadi ya wafanyakazi zaidi ya 120,000, wengi wao wakiwa wanawake.
Mabula alizitaja fursa ambazo wajasiriamali wanaweza kunufaika nazo kupitia mradi huo, kuwa ni mfumo wa kilimo na ufugaji kuku unaosimamiwa kitaalamu, mfuko wa uwekezaji, upatikanaji huduma za fedha pamoja na soko.
Mapema, Meneja Masoko wa mradi wa LEAD Stephano Mahenge, alisema tathmini ya zao la mahindi na uendelezaji wake uliofanywa kuanzia Mei 22 hadi Juni 20 katika masoko ya Mwanakwerekwe na Mombasa Unguja, umeonesha kuwa jitihada kubwa zinazochukuliwa kuimarisha zao hilo, zinakabiliwa na changamoto mbalimbali.
Miongoni mwa changamoto hizo, alisema ni pamoja na kutokuwepo mtandao unaowaunganisha wafanyabiashara wa pembejeo na wakulima ili kujua namna mbegu wanazowauzia zinasaidia kwa kiwango gani kuleta uzalishaji wenye tija.
"Lazima mjenge ushirikiano kwa kuulizana na kupeana maarifa juu ya njia bora za kuimarisha zao la mahindi ambalo soko lake nchini na nje ni kubwa. Wale waliofanikiwa wasifiche siri za mafanikio yao," alisisitiza Meneja huyo wa masoko.
Washiriki wa mafunzo hayo kutoka maeneo mbalimbali ya Unguja, walieleza kufarijika kwao na elimu waliyoipata katika warsha hiyo ya siku mbili iliyofungwa Agosti 13 na waliyopata kabla ya hapo, imewasaidia kukuza mitaji yao na kutanua wigo wa biashara na kilimo cha mahindi.
Walilishuuru shirika la BRAC kwa uamuzi wake wa kusambaza elimu hiyo wa wakulima wa Zanzibar, na kulitaka liendelee kuangalia maeneo mengine ili kuinua hali za maisha ya wakulima.
Mradi huo unaofanyika katika matawi 40 kwenye mikoa 15 ya Tanzania ikiwemo Zanzibar, umepania kuimarisha kipato cha familia maskini zinazoishi vijijini ambazo ni wakulima na wafugaji wadogo wadogo, ambapo asilimia 65 ni wanawake.
No comments:
Post a Comment