STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar 06 Agosti, 2015
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein ametoa wito kwa wanawake nchini kuchangamkia fursa za mafunzo yanayotolewa katika kituo cha kuwafunza wanawake utengenezaji wa vifaa vya umeme wa jua na ujasiriamali alichokifungua leo huko katika kijiji cha Kibokwa, Wilaya ya Kasazini ‘A’, Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Akizungumza na wananchi katika hafla ya ufunguzi wa kituo hicho, Dk. Shein amesema kuzinduliwa kwa kituo hicho ambacho kinapokea na kutoa mafunzo hata kwa wale kinamama ambao hawakubahatika kwenda skuli wakati wa utotoni au walikwenda skuli lakini hawakupata elimu inayotambulika rasmi ni hatua muhimu katika utekelezaji wa mipango ya serikali ya kuwawezesha kinamama na kuimarisha shughuli za ujasiriamali katika stadi mbali mbali.
Aliwataka wakufunzi wa kituo hicho ambao ni miongoni mwa kinamama waliobahatikia kupata mafunzo yao nchini India katika chuo kama hicho cha Barefoot ambacho Mheshimiwa Rais alikitembelea wakati wa ziara yake nchini India mwaka jana kutumia vipaji vyao kikamilifu kukiendesha kituo hicho kwa mafanikio makubwa.
“Ni matumaini yangu kuwa kituo hiki kinatoa hamasa kwa kinamama kukabiliana na changamoto wanazokabiliana nazo katika maisha yao ya kila siku na hatimae kuzishinda changamoto hizo na kuimarisha ustawi wa wanawake na jamii kwa ujumla” Dk. Shein alieleza.
Mbali ya kujifunza utengenezaji wa vifaa vya umeme wa jua wanawake wataokajiunga kituoni hapo watapata mafunzo mbalimbali ya amali ambayo yatasaidia kupambana na umasikini kwa kujiongezea kipato.
“Ni habari njema kuona kuwa katika kituo hiki kinamama watapata fursa za kujifunza mbinu na mitindo ya ushoni wa nguo za kike na za kiume, ufugaji wa nyuki na ukamuaji asali kwa biashara, utengenezaji chaki na mengine mengi ambapo shughuli zote hizi zinalenga katika kuwapatia ujuzi na hatimae waweze kujiongezea kipato na kujikimu kimaisha”Dk. Shein alibainisha.
Alisifu mwamko wa ujasiriamali walionao vijana na wanawake katika mkoa wa Kaskazini Unguja ambapo wanafanya shughuli mbalimbali za kijasiriamali mfano shughuli za uvuvi na biashara ya dagaa ambayo sasa imekuwa maarufu kwa wananchi wa mkoa pamoja na shughuli za kazi za mikono za kinamama.
Aidha, Dk. Shein alibainisha kuwa katika miaka mitano ya Serikali ya Awamu ya Saba wananchi wana kila sababu ya kujivunia mafanikio makubwa yaliyopatikana ya kuimarisha shughuli za ujasiriamali nchini pamoja na kuimarisha hali ya wanawake.
“Katika hili hata watoto wa kike wanafanya vizuri sana katika elimu hadi ngazi ya elimu ya juu ambapo hivi sasa mbali ya matokeo mazuri lakini hata idadi ya watoto wa kike ni kubwa kuliko wanaume katika taasisi zetu za elimu hapa Zanzibar” alifafanua Dk. Shein.
Alitumia fursa hiyo kuwapongeza wana CCM kwa kusimamia vyema Utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi kitendo ambacho kimeleta matunda yanayoonekana hivi sasa. Aidha aliwashukuru washirika wote wa maendeleo waliofanikisha ujenzi wa kituo hicho.
“Ni msaada mkubwa kwa nchi yetu na watu wake kwani kumpa mtu msaada wa elimu ni jambo kubwa” na kuongeza kuwa wananchi wa Zanzibar wanathamini sana msaada huo na mingine inayotolewa na washirika hao.
Kwa upande wake, Waziri wa Uwezeshaji, Ustawi wa Jamii,Vijana, Wanawake na Watoto Bi Zainab Omar Mohamed alieleza kuwa uzinduzi wa kituo hicho umefungua ukurasa mpya wa harakati za maendeleo ya wanawake nchini huku akimpongeza Dk. Shein kwa jitihada zake za kuwaendeleza wanawake na upendo mkubwa aliouonesha kwa wanawake katika uongozi wake.
Akitoa maelezo juu ya ujenzi wa kituo hicho Katibu Mkuu Wizara ya Uwezeshaji, Ustawi wa Jamii,Vijana, Wanawake na Watoto Bi Asha Abdalla alisema kituo hicho ambacho ni matokeo ya ziara ya Mheshimiwa Rais aliyoifanya nchini India mapema mwaka jana kimegharimu jumla ya shilingi mia moja na ishirini na nne (124) ambapo Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imetoa shilingi milioni 76 wakati shilingi milioni 48 zimetolewa na Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulia wanawake (UN-Women).
Alifafanua kuwa kituo hicho ambacho kinawalenga kinamama wa vijijini ambao baadhi yao hawajui kusoma wala kuandika kinaendeshwa kwa mashirikiano kati ya SMZ kupitia wizara yake, Chuo cha Barefoot cha India na Taasisi isiyo ya kiserikali inayojishughulisha na maendeleo ya wanawake ya Wanawake Kupanda.
Katibu Mkuu huyo aliongeza kuwa hadi sasa kituo kimeshapokea kinamama 12 kutoka vijiji vya Mbuyutende na Bumbwini Kiongwe kwa upande wa Unguja na Msuka na Makoongwe kwa upande wa Pemba.
Ili kutanua wigo, alieleza kuwa utakuwepo ushirikiano wa karibu kati ya kituo hicho na kituo cha kukuza Ujasiriamali kilichopo Taasisi ya Sayansi na Tekinolojia ya Karume Zanzibar.
Wakati huo huo Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein ameziagiza wizara za Ardhi, Makazi, Maji na Nishati pamoja na Wizara ya Kilimo na Maliasili kuhakikisha katika kipindi cha ndani ya mwezi mmoja inakipatia kituo hicho eneo zaidi kwa ajili ya upanuzi wa shughuli zake. Sambamba na agizo hilo Dk. Shein ameitaka Wizara ya Miundombinu na Mawasiliano kutengeneza barabara iendayo katika chuo hicho ambayo hivi sasa imewekwa kifusi tu.
Postal Address: 2422 Tel.+255 776 613 015, Fax: 024 2231822
No comments:
Post a Comment