Habari za Punde

Dk.Shein:Hospitali ya Abdalla Mzee Pemba Itakidhi Viwango vya Afya vya Kimataifa.

STATE HOUSE ZANZIBAR

OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
    Zanzibar                                                                                                   28 Agosti, 2015
---
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesema kujengwa upya kwa hospitali ya Abdalla Mzee huko Mkoani Pemba kutawezesha hospitali hiyo kuwa ya kisasa na inayokidhi viwango vya kimataifa.
 Akizungumza mara baada ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa hospitali hiyo jana, Dk. Shein aliishukuru serikali na wananchi wa Jamhuri ya watu wa China kwa msaada wao mkubwa katika kuimarisha sekta ya afya nchini ikiwemo ujenzi wa hospitali hiyo.
 “hawa (wachina) ni marafiki zetu wa kweli kwani akuufaaye kwa dhiki ndie rafiki” Dk. Shein aliwaeleza mamia ya wananchi wa mji wa Mkoani na viongozi wa serikali aliohudhuria hafla hiyo.
 Alitoa shukrani maalum kwa Rais Xi Jing Ping kwa kuendeleza udugu na urafiki kati ya watu wa Zanzibar na China kwa kufuata nyazo za viongozi waliomtangulia hayati Mao Dze Tung na Cho en Lai ambao walioasisi urafiki huo na viongozi wa kwanza Tanzania hayati Mwalimu Julius Nyerere na Marehemu Abeid Amani Karume.
 Alisema ni jambo la fahari kuona kuwa urafiki wa nchi zetu mbili umekuwa wa mafanikio makubwa na kutoa mfano wa mchango wa Serikali na wananchi wa Jamhuri ya Watu wa China kwa Zanzibar mara baada ya Mapinduzi hadi leo.
 “wametuunga mkono kujenga nchi yetu mara baada ya Mapinduzi katika sekta za miundombinu, maji, kilimo, viwanda na kwa upande wa afya wamekuwa wakileta timu za wataalamu na mabingwa wa utatibu sasa ni timu ya 31” Dk. Shein alifafanua na kuongeza kuwa wataalamu hao wamekuwa wakifayakazi katika hospitali kuu ya Mnazi Mmoja Unguja na hospitali hiyo ya Abdalla Mzee Pemba.
 Alibainisha kuwa alipoomba msaada kwa viongozi wa China kuhusu kujengwa hospitali hiyo alifanya hivyo kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya CCM 2010 ibara152 ambayo ilielekeza kuendeleza kuimarisha sekta ya afya ikiwemo kuifanya hospitali ya Abdalla Mzee kuwa hospitali ya Mkoa.
 Kuhusu ubora wa hospitali hiyo alieleza kuwa hospitali imezingatia vigezo vyote vya hospitali za kisasa na kwamba itakuwa na vifaa vyote vya kisasa vya uchunguzi wa maradhi ambavyo vitatolewa na Serikali ya Jamhuri ya watu wa China na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar itaweka kifaa kipya cha uchunguzi wa maradhi kijulikanacho kama Magnetic Resonance Imaging (MRI).
 Katika hotuba yake hiyo alitambua mchango wa mwasisi wa Afro Shirazi Hayati Abdalla Mzee ambaye hospitali hiyo ilipewa jina lake na Mzee Karume.
 Aidha alitambua na kupongeza kazi kubwa iliyofanywa na Mzee Aboud Jumbe Mwinyi ambaye akiwa Waziri wa kwanza Afya wa Zanzibar alitengeneza mpango wa kwanza afya ambao ndio chimbuko la maendeleo ya afya hivi sasa visiwani Unguja na Pemba.
 Dk. Shein alitumia fursa hiyo kuwashukuru kwa dhati wananchi waliokubali kuhama katika eneo la hospitali pamoja na waislamu wa mji huo kwa kukubali kuhamisha msikiti wao ili kupisha upanuzi wa hopsitali hiyo.
 “haikuwa jambo rahisi watu hao kuridhia kuhama katika eneo lao walilokulia. Wako waliokubali mara moja na wako waliosita lakini hatimae wote walikubali”alisema Dk. Shein.
Aliongeza kuwa kama wananchi hao wangekataa na serikali tayari imepata msaada huo basi Zanzibar ingekosa “kaa na gando” hivyo wananchi wengine wajifunze kutoka kwa wananchi hao yanapokuja masuala ya maslahi ya maendeleo ya taifa kama hayo.
 Waziri wa Afya Rashid Seif katika maelezo yake kumkaribisha mheshimiwa Rais, alieleza kufarijika kwake kuona hospitali hiyo inajengwa upya hivyo kuongeza ufanisi na huduma za afya kisiwani Pemba.
 Waziri huyo aliishukuru Serikali na wananchi wa Jamhuri ya Watu wa China kwa msaada wake huo mkubwa kwa wananchi wa Zanzibar .
 Akitoa salamu nchi yake katika hafla hiyo Balozi wa Jamhuri ya Watu wa China Nchini Mheshimiwa…….alieleza kuwa ujenzi wa hospitali hiyo ni uthibitisho mwingine wa udugu na urafiki wa watu wa China na Zanzibar uliodumu kwa miaka mingi.
 Alibainisha kuwa China inathamini sana udugu na urafiki huo na kwamba itauendeleza na kuuimarisha kwa manufaa ya wananchi wa pande zote na kuahidi kuendelea kuwasaidia wananchi wa Zanzibar katika harakati zao za kuijenga nchi yao.
 Kwa mujibu wa taarifa ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Dk. Mohamed Saleh Jidawi hospitali hiyo ambayo itagharimu shilingi bilioni 26 itakapokamilika itakuwa huduma zote muhimu zinazopatikana katika hospitali kubwa na itakuwa hospitali ya Mkoa wa Kusini na pia ya rufaa kwa Pemba.
 Postal Address: 2422 Tel.+255 776 613 015, Fax: 024 2231822 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.