Na. Benjamin Sawe
WHVUM
Hadithi moja ya ajabu inayosimuliwa na wazee wa
kizaramo ni ile ya Nyamihembe aliyolewa Unyamwezi. Msimulizi mmoja alisema haikuwa
Hadithi hii ni ya kweli, nayo ni hii: ( Hii ni Tanzu ya Fasihi simulizi)
Mzee mmoja wa Kizaramo alikuwa na binti mzuri
aliyeitwa Nyamihembe, mtoto wa kiti cha kwanza.(Mtoto wa kiti ni mwana Nyang’iti, ni utambulisho wa Mila na Desturi za
baadhi ya Makabila ya Pwani, hutumika katika shuhuri zote za kimila za
kurithisha na kujamiisha vijana katika kundi la utu uzima) Baada ya kuvunja
ungo akatokea Mnyamwezi mmoja akamposa, na kufunga pamvu(Harusi), kisha akapewa Bibi huyo akaishi naye. Lakini Yule Mnyamwezi
baadae alipendelea kurudi kwao Unyamwezi pamoja na mke yule, basi akataka
idhini kwa wazazi akakubaliwa. Akaondoka Uzaramo na mkewe hadi kwao
Unyamwezini.
Walipokuwa kule wakajaaliwa watoto wengi wa kiume
na wakike. Waliishi kule Unyamwezi kwa miaka mingi hadi wale watoto wakawa watu
wazima, wakaoa na kuolewa, wakazaa watoto kadha wa kadha waliokua wajukuu wa
Nyamihembe. Lakini watoto na wajukuu wa
Nyamihembe hawakupata bahati ya kufika Uzaramo
tangu kuzaliwa kwao ila kila mara Bibi Nyamihembe alikuwa akiwasimulia habari
za Uzaramo kama hadithi tu.
Nyamihembe aliishi kule hata akawa kizee ajuza,
maana hata wale wajukuu walizaa kisha wakajukuu, akawa na Virembwe kadha wa
kadha. Wakati ule yule Mzazi mwezake Mnyamwezi Uzee ulimkithiri akafariki Dunia.
Nyamihembe akawa anatunzwa na wanawe na wajukuze, nae kila mara aliwausia
akisema, ‘mimi nikifa msinizike hapa,
mnipeleke kwetu Uzaramo mkanizike huko’.
Mwanamke huyo aliishi kwa miaka mingi hata wale
wanae wengine wakafariki dunia, yeye akabaki kama Mzimu, macho yake yalikwisha
nguvu ya kuona akawa kipofu, nyama za mwili zikamkauka akabakiwa na mifupa
na ngozi ikakunjana kunjana, hakujimudu kutembea, mvi zake zikapukutika zote,
akabaki na Upara.
Ajabu nyingine iliyotokea mwilini mwake ziliota Pembe mbili zilizotokeza
katika paji lake,
baada pembe hizo zikakua zikawa ndefu
zilizo inama chini. Umbo alilokua nalo liliwaogofya watu, ila wale wajukuu zake
ndio waliokuwa wakimuhudumia, maana ilibidi kila asubuhi kumuinua na kumtoa nje
aote jua na jioni ni kumrejesha ndani na kumlaza kitandani. Alipokuwa
anakalishwa chini zile pembe zilikuwa zinagusa ardhi na kujichomeka kama mikuki.
Wajukuu walipata taabu sana kwa kumtunza Ajuza huyo. Baadaye mauti yalimfikia na kumuondolea taabu zake. Nyamihembe akaifariki
Dunia.
Basi, walipokuwa wakitangaza tanzia na kutayarisha
mambo ya mazishi wale wajukuu hawakujali
ule usia wake aliousia kwamba akifa akazikwe kwao Uzaramo. Waliona nijambo
lisilowezekana, maana kutoka Unyamwezi
mpaka Uzaramo ni mwendo wa miezi miwili.
Basi wakatayarisha mahali pa kuoshea maiti lakini
walipojaribu kumuinua Mfu yule
wakashindwa kabisa kwa maana alikuwa mzito sana wala hawakumudu
kumjongeza hata kidogo. Walifanya bidii
kwa nguvu zao zote wakashindwa, wake kwa waume wakashangazwa na muujiza ule.
Lakini baadae kidogo mjukuu mmoja alikumbuka usia na wimbo aliofundishwa na
Bibi yake wakati wa uhai, maana mara mbili tatu Nyamihembe alimfundisha wimbo Mjukuu wake akamuhusia
kuwa atakapokufa wazishi wake waimbe
wimbo huo, naye atawaongoza njia ya
kwendea Uzaramo katika nchi aliyozaliwa akazikwe huko.(Umuhimu wa kujiandikia Tarijima).
Basi Yule mjukuu akawaeleza habari ile watu
waliokuapo nao wakanena, ‘Natujaribu kuimba wimbo huo na tutazame matokeo yake
yatakuaje’ lakini wengine wakasema, ‘pengine
huenda Mfu akainuka kweli na kutuongoza njia ya kwenda kwao uzaramo, nasi
wajibu wetu kumfuata, basi si bora kama tutatayarisha Chakula kwa matumizi yetu
ya njiani kabla hatujaimba wimbo wenyewe?’ kwa shauri hilo, wote wakakubaliana
kutayarisha masurufu ya njiani.
Basi siku Ile wakalala bila kuigusa tena ile
maiti, hata asubuhi yake kulipokucha tu wakakusanyika Watu wengi waliokuwa na
shauku ya kujua mazishi ya bibi Nyamihembe. Yule mjukuu akawafundisha kiitikio
cha Wimbo na yeye mwenyewe akaanza kuimba:
‘Nyamihembe tuhilike ukaye gwee!’
Nawenzake wakaitikia wimbo,
‘Tuhilike kumwetu Zaramo’
Na maana yake:’Ewe Nyamihembe
tuongoze nyumbani!’
Na waitikiao husema:’ Tuongoze
kwetu Uzaramo.’
Wimbo ule ulipoanza kuimbwa tu, ibra (ajabu) ikaanza tena
kutokea, zile pembe zikaanza kunywea kidogo kidogo mpaka zikatoeka kabisa.
Kisha mwili wa Mfu ukaanza kutikisika, halafu Mfu mwenyewe akasimama wima, watu
wengine waliogopa wakaanza kukimbia
lakini wale wajukuu na ndugu wengine walibaki pale wakiendelea kuimba
ule wimbo.
Mara
Nyamihembe naye akaimba :
‘Mowana silawile behi niye,
Silawile behi m-m-m,
Ndawa Zaramo’.
Na maana yake,
ni (Tafsiri yake ‘Enyi watoto sikutoka karibu mimi, nimetoka Uzaramo.’)Nyamihembe
alipokuwa akiimba hivyo mara akaanza kutembea kwa miguu yake kama kwamba mtu mzima
mwenye nguvu. Wajukuu na jamaa wengine wakamfuata, Msafara ukaanza pale kuelekea
Uzaramo. Ndugu wa marehemu, mume wa Nyamihembe waliuandama msafara huo. Wengi
wao walifuata ili kujua mwisho wa miujiza ile. Lakini hakuna aliyesadiki kama Mfu yule atawaongoza mpaka Uzaramo.
Basi Wimbo uliendelea kuimbwa na Nyamihembe
aliendelea kuujibu Wimbo huo hali akiwa kiongozi wa msafara, alikuwa Kipofu,
lakini ajabu kwamba alikuwa Kiongozi mwenye mwendo wa haraka bila kupotea njia.
Siku ile ya kwanza walisafiri mpaka Mchana upatao saa saba, kwa ghafla
Nyamihembe akaanguka kando ya njia akajilaza kifudifudi akawa mfu tena.
Watu wakajua kuwa sasa ndio mwisho wa ajabu wa uhai wake, wakafanya shauri ya
kumwinua ili wamchukue na kumrudisha nyumbani walikotoka ili wakamzike.
Lakini
walipojaribu kumwinua, wakashindwa kabisa maana alikuwa ameambatana na ardhi
wala hawakuweza kumjongeza. Kwa kuwa wote walikuwa wamechoka kwa njaa wakatua
pale na kupika vyakula vyao wakala. Hata wakati wa alasiri, wakashauriana
kuimba tena Wimbo ule labda Nyamihembe atainuka. Basi walipoimba tu, Nyamihembe
akasimama na kuimba wimbo wake mara akaongoza tena msafara. Wakamfuata
katika hali hiyohiyo ya kuimba mpaka jua lilipokuchwa Nyamihembe akaanguka
kando ya njia akajilaza kifudifudi. Wafuasi nao walichoka kwa ule mwendo wa
kutwa, basi wakafanya kambi mahali pale wakalala.
Asubuhi
kulipokucha, wale waliofuata msafara kwa upelelezi wa kujua mwisho wa ajabu ile
wakarejea makwao. Lakini Wajukuu wa Nyamihembe pamoja na ndugu wachache wa mume
wa Bibi Nyamihembe waliendelea katika safari. Nyimbo zikaimbwa kama kawaida na Nyamihembe akaongoza msafara.
Mambo
yaliendelea hivyo kama siku ya kwanza, nao walisafiri katika hali hiyo kwa muda
wa Mwezi na nusu. Hata safari ilipobaki mwendo wa siku tatu Nyamihembe
hakufanya kituo tena wakati wa mchana isipokuwa alifululiza kusafiri na jioni
akafanya kituo.
Asubuhi moja waliposafiri hata mnamo saa tatu
hivi wakatokea katika Kijiji chenye nyumba nyingi pamoja, kwa ghafla Nyamihembe
akajitupa katikati ya Uga. Lakini badala ya kulala kifudifudi alilala
chali.
Watu wa Kijiji kile walistaajabishwa sana
kuona Kizee ajuza kikifuatwa na jeshi la watu, kisha kimejitupa uwanjani kwao.
Wale waliokuja na Nyamihembe waliendelea kuimba ule wimbo, lakini Nyamihembe
hakuinuka tena, akawa kama mfu wa kawaida, maana amekwisha fika nyumbani kwake
Uzaramo. Watu wa Kijiji wakakusanyika na kuwauliza habari wale wageni. Wageni
wakasimulia habari zote za Nyamihembe na jinsi hapo zamani alipopata kuolewa na
Mnyamwezi, habari za wosia wake aliousia wakati alipokuwa hai na jinsi walivyo
pata kuja naye mpaka pale.
Basi
kutokana na maelezo yale, Wazee wengi wa Kijiji kile walikumbuka nasaba yake,
wengine wakasema,’huyu ni Shangazi yetu,’ wengine wakasema,’ huyu ni Nyanya yetu’
mradi Kijiji kile kilijaa ukoo wote wa bibi Nyamihembe. Baada ya hivyo wakaleta
kitanda wakaichukua maiti bila ya taabu yoyote, wakailaza juu ya kitanda na
kuipeleka ndani. Na wengine wakashughulika kuwapokea wageni waliotoka
Unyamwezi.
Siku ile watani wakaarifiwa na majirani
wengine wakapelekewa Tanzia (Habari ya
kifo inayopelekwa kutoka mbali) kuwa Nyamihembe Mwanamhembe alieishi
Unyamwezi amerudi katika hali ya umauti na mazishi yake yatakuwa kesho.
Hapakuwa na kilio wakati ule, maana Nyamihembe alikuwa Tagala (mzee, kikongwe sana),
mpaka Magharibi Bendebende (Ngoma ya kuashiria kifo cha mtu mkubwa)
ikapigwa kuashilia kilio. Wacheza Songwa
na uzunguli (Ngoma zinazochezwa wakati wa maziko ya mtu mkubwa)
wakahudhuria kama desturi. Hata Siku
ya pili maandalizi ya mazishi yakafanyika, Nyamihembe
akazikwa kwa heshima kubwa.
Makala
haya yanatufundisha kwamba fahari ya mtu ni kwao. (Makala haya yana vionjo
vyote vya kidiaspora, yanatukumbusha ugenini ni matembezi, kwako ni maskani),yameandikwa
kwa ushirikiano wa Idara ya Utamaduni Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na
Michezo.
Fanani wa Hadithi ni Mwaruka
Ramadhani (1965)
No comments:
Post a Comment