Na Shemsia Khamis, PEMBA
SHIRIKA la Umeme Zanzibar (ZECO) Tawi
la Pemba limesema jukumu la kulinda na
kuhifadhi miundo mbinu ya Umeme ni la wananchi wote na sio Shirika hilo pekee kama wanavyodhani baadhi ya watu.
Kauli
hiyo ilitolewa na Meneja wa Shirika hilo
Pemba, Salum Massoud, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari wakati kazi ya kusambaza Waya baharini kwa ajili ya
kupeleka umeme Kisiwa panza na Makoongwe wilaya ya mkaoni kisiwani Pemba
ikiendelea.
Alisema ni
vyema wananchi wote wakawa mstari wa mbele katika kuhakikisha miundo mbinu ya
umeme inakuwa salama muda wote, ili kuunga mkono juhudi za Serikali katika
kuwasambazia huduma hiyo.
Alieleza
sio jambo la busara kwa wananchi
kuthubutu kuharibu miundo mbinu hiyo kwa njia moja au nyengine, kwani ni kurudisha
nyuma maendeleo yao na Serikali kwa ujumla.
Salim, alisema ahadi ya Serikali ni kusambaza umeme katika
visiwa vyote vidogo vidogo vya Unguja na Pemba, ndio maana wakaamua kuibua
mradi maalumu wa kwa ajili ya kutekeleza ahadi hiyo.
‘’Lengo
la Serikali, ni kuhakikisha kuwa wananchi wote wa mjini na vijijini wanapata
huduma ya umeme, bila ya ubaguzi wa aina yoyote ile’’, alisema Meneja.
Alifahamisha
Waya huo umechukuwa kilomita 1.7 kutoka
Chokocho hadi Kisiwapanza, ambapo Michenzani hadi Makoongwe umechukua kilomita
1.5, hivyo ni vyema wananchi wakawa makini kuulinda waya huo muda wote.
Akizungumzia
matumaini yao, mara baada ya kukamilika zoezi hilo visiwani humo, alisema endapo
Wananchi watashajihika kuunga Umeme ni kuongeza uzalishaji kwa Shirika na Serikali
kwa ujumla.
Kwa
upande wake, Sheha wa shehia ya Makoongwe Silima Hija Hassan, alisema kufika kwa huduma ya umeme Kisiwani kwao ni faraja iliyoje kwani walikuwa na hamu muda
mrefu.
Alifahamisha
mara baada ya kukamilika kwa zoezi hilo Kisiwa
chao kitakuwa cha aina yake kwani hata
shughuli za uzalishali zinaweza kuongezeka.
‘’Shughuli
za uzalishaji zitaongezeka maana wananchi
watanunua Mafriza wataeka Samaki na hata juisi wanaweza kufanya kwa biashara’’,
alisema Sheha.
Mmoja
kati ya wananchi wa Kisiwa hicho ,Omar
Moh’d Salum, alisema wamekuwa wakiitafuta huduma ya umeme masafa marefu, hivyo
kukamilika kwa zoezi hilo kutawaondoshea usumbufu.
Alieleleza
baadhi ya wananchi wanatumia umeme wa Sola
lakini mara baada ya kufika umeme Kisiwani kwao, huduma hiyo itakuwa ya
uhakika.
Waya
huo uliosambazwa katika bahari kwa ajili ya kufikisha umeme Visiwani humo,
umegharimu Tshilingi bilioni 1.5 na zoezi hilo linatarajiwa kukamilika baada ya
siku kumi.
No comments:
Post a Comment