Habari za Punde

Zantel yaingia ubia na Benki ya Watu wa Zanzibar (PBZ) kutoa huduma za kibenki kupitia simu za mkononi

 Waziri wa Fedha wa Zanzibar, Mheshimiwa Omari Yusuf Mzee, akisisitiza jambo wakati wa uzinduzi wa huduma ya Benki yako Kiganjani ya Zantel pamoja na benki ya PBZ. Kutoka kushoto ni Mkurugenzi wa Zantel, Pratap Ghose, akifuatiwa na Mwenyekiti wa bodi ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania, Salmin Senga, na mwisho kulia ni Mkurugenzi wa benki ya PBZ, Juma Mohammed

 Mkurugenzi wa Zantel, Pratap Ghose akizungumza wakati wa uzinduzi wa huduma mpya kati ya kampuni yake na benki ya PBZ, Benki Yako Kiganjani.

 Mkurugenzi wa Huduma ya Kifedha za simu za mtandao, Hashim Mkudi akielezea namna ya kutumia huduma ya Benki Kiganjani Mwako iliyozinduliwa kwa ushirikiano wa kampuni yake na benki ya PBZ.
Mkurugenzi wa benki ya PBZ, Juma Mohammed akizungumza wakati wa kuzindua huduma ya Benki Kiganjani Mwako, inayoendeshwa na kwa ushirikiano wa benki yake na kampuni ya Zantel.


Zanzibar, 31/8/2015: Kampuni ya simu ya Zantel leo imeingia ubia na Benki ya Watu wa Zanzibar, kwa ajili ya kutoa huduma za kibenki kwa wateja wao kupitia huduma ya simu ya Ezypesa.

Makubaliano haya yatawawezesha wateja wa Ezypesa wenye akaunti za PBZ kufanya miamala kupitia simu zao za mkononi, kujua salio katika akaunti zao pamoja na kupata taarifa fupi za akaunti zao.
                                             
Akizungumza wakati wa kuzindua ushirikiano huo, Waziri wa Fedha wa Serikali ya Zanzibar, Mheshimiwa Omari Yusuf Mzee, ambaye alikuwa mgeni rasmi katika uzinduzi huo amesema ushirikiano kati ya Zantel na Benki ya Watu wa Zanzibar ni faraja kubwa kwa wananchi kwani itaongeza wigo na kurahisisha huduma za kibenki.

‘Ushirikiano kati ya benki ya PBZ na Zantel ni wa muda mrefu, na kwa uzinduzi wa huduma hii leo ambao umekuwa ukisubiriwa na Wazanzibari kwa muda mrefu wameweka historia’ alisema Mheshimiwa Mzee.

Mheshimiwa Mzee pia alisema huduma hii imekuja kwa wakati muafaka, kwani asilimia kubwa ya Wazanzibar wana simu za Zantel na akaunti katika benki ya PBZ huku akiwachagiza makampuni kuoungeza huduma zaidi za kijamii kwa watu wa Zanzibar.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Zantel, Pratap Ghose alisema ushirikiano baina ya PBZ na Zantel utawezesha ukuaji wa huduma ya EzyPesa ambayo imekuwa ni sehemu ya maisha ya watu wa Zanzibar


“Ubia huu baina ya Zantel na PBZ utawarahishia wateja wetu katika kutumia huduma za benki katika kufanya miamala ya kifedha kutoka katika akaunti zao za PBZ kwenda kwenye akaunti zao za EzyPesa kwa njia rahisi na salama” alisema Ghose.

Ghose aliongeza kwa kusema kuwa wateja wa Zantel sasa wataweza kutumia simu zao kufanya shughuli za kibenki na hivyo kuondoa usumbufu wa upatikanaji wa huduma za PBZ kwa mwananchi wa kawaida.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mkurugenzi Mkuu wa PBZ, Juma Mohammed, alisema kwamba ubia huo utawawezesha wateja kutoa na kuweka fedha kwenye akaunti zao, kulipia huduma, kujua salio, kufanya miamala kutoka akaunti moja kwenda nyingine pamoja na kununua muda wa maongezi.

‘Huduma hii itafanya huduma za kifedha zipatikane kwa urahisi zaidi kwa wateja wetu kuliko ilivyokuwa awali, na pia itaboresha ubora wa huduma pamoja na kupunguza msongamano wa wateja hasa kipindi cha mwisho wa mwezi’ alisema Mohammed.

Uzinduzi wa huduma hii kwa kushirikiana na PBZ inakuja kama ongezeko baada ya huduma ya awali ya TUKUZA inayotolewa na Ezypesa kwa wateja wote wa Zanzibar, wateja wanaweza kuanza kufurahia huduma hii moja kwa moja kwa kubonyeza namba *150*02#.

‘Zantel ina miundombinu ya kisasa na imara kuwezesha kufanya kazi sawasawa na kwa viwango vya dunia, hivyo wizara ya miundombinu inawahakikishia wazanzibar waipokee huduma hii kwa mikono miwili’ alisema Mkurugenzi wa Mawasiliano Zanzibar, Dkt Mzee Suleiman Mndewa.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.