Na Khamsi Haji OMKR
Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi CUF, Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad amewahakikishia wanachama wa chama hicho kuwa uamuzi wa Mwenyekiti, Profesa Ibrahim Haruna Lipumba kujiuzulu wadhifa wake hautausambaratisha Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) na CUF kimeendelea kubaki katika mikono salama.
Maalim Seif amesema hayo jana usiku huko Makao Makuu ya Chama hicho Buguruni mara baada ya kuwasili na kukuta mamia ya wanachama wakisubiri kusikia msimamo wa chama kufuatia hatua ya Profesa Lipumba kutangaza kujiuzulu.
Maalim Seif amesema hata baada ya Profesa Lipumba kuondoka yeye akiwa Katibu Mkuu na viongozi wenzake waliobaki watahakikisha kwamba chama hicho kinafikia malengo ya kuanzishwa kwake, ambayo ni kuhakikisha kinakamata dola.
Katibu Mkuu wa CUF, ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar amesema chama cha siasa ni kama usafiri wa treni watu hupanda na kushuka lakini bado safari huendelea mbele hadi katika eneo lililokusudiwa.
“Kama ni treni inayokwenda Mwanza ikifika Morogoro abiria watashuka, lakini wengine watapanda, ikifika Kaliua watashuka abiria lakini wengine watapanda …Profesa Lipumba kajiuzulu CUF, wale waliojiunga CUF kwa sababu ya Profesa wanayo fursa ya kuamua kubaki CUF au kutoka”, alisema Maalim Seif.
Amesema chama hicho mwishoni mwa wiki hii kitaanza kufanya vikao vyake kuzingatia hatua iliyotokea, ili baadaye kuchukua maamuzi thabiti ya kukiongoza chama hicho na kuhakikisha kinabaki katika mikono salama, hadi hapo uchaguzi wa kumtafuta Mwenyekiti utakapofanyika.
Akizungumzia UKAWA, Maalim Seif alisema baada ya hatua hiyo ya Profesa Lipumba alizungumza na viongozi wakuu wa umoja huo, akiwemo, Freeman Mbowe, James Mbatia na Emmanuel Makaidi pamoja na mgombea Urais wa umoja huo, Edward Lowassa na wamehakikisiana hawatarudi nyuma.
“Tumehakikishiana kwamba UKAWA upo na umeimarika zaidi na hatutarudi nyuma, na tumeona kwa namna unavyoungwa mkono na wananchi walio wengi Magufuli Ikulu ya Magogoni hataiona”, alisema Maalim Seif.
Hata hivyo, amesema anampongeza sana Profesa Lipumba kwa kuwaachia wananchi wa Tanzania Umoja wa Katiba yao UKAWA, ambapo yeye Profesa ndiye aliyekuwa muasisi na Mwenyekiti wa wenyeviti wa vyama vinavyounda umoja huo.
Baada ya kauli hiyo ya Katibu Mkuu wananchi hao ambao walianza kukusanyika tokea asubuhi hadi usiku kumsubiri Katibu Mkuu walitawanyika.
Profesa Lipumba alijiuzulu wadhifa wa Mwenyekiti wa CUF juzi na kuwaomba radhi wanachama wa chama hicho kutokana na uamuzi wake huo.
No comments:
Post a Comment