Habari za Punde

‘MEO’ kuramba 35.5 m/= wakivuna miti


NA HAJI NASSOR PEMBA 
WANAKIKUNDI cha upandaji miti na uhifadhi wa mazingira ‘MEO’ kilichopo Mchekeni Wawi wilaya ya Chake chake Pemba, wanatarajia kujipatia shilingi 35.5 milioni miaka michache ijayo, mara watakapoanza kuvuna miti yao ya aina mbali mbali zaidi ya 25,000.
MEO tayari imeshatumia shilingi 19 milioni, kwa ajili ya kuliimarisha shamba la miti hiyo, ambapo kati ya fedha hizo shilingi 9 milioni ni kutoka Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Tanzania ‘TASAF’ huku nguvu kazi yao ikiwa ni shilingi 10 milioni.
Miti ambayo wanatarajia kuivuna baada ya maelekezo ya kutoka kwa wataalamu, ni Mivinje 9000, Mitondoo 300, Mikungu 700, Misaji 100, Mikeshia 250, ambapo pia wameshaotesha Miembe ya muda mfupi 250, Mikorosho 200 na minanasi 4000.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi, Mwenyekiti wa ‘MEO’ Khamis Ali Juma, alisema lengo la hasa la kupanda miti hiyo ni uhifadhi mazingira.
Alieleza kuwa sualala uvunaji kwa miti isiokuwa ya chakula, sio kupaumbele, bali kwanza ni kuangalia suala zima la kulirejesha eneo hilo uoto wake wa asili, baada ya kuathiriwa kwa ukataji miti kiholela.
“Eneo hili la ekeari zaidi ya 8.5 liliharibiwa sana na wanaokata kuni, miti ya ujenzi na wapiga mkaa, sasa sisi tumeshalirejesha katika uasili wake, hivyo hata uvunaji wa miti wakati ukifika hautoathiri’’,alifafanua.

Kwa upande wake Katibu wa ‘MEO’ Kombo Yahay Juma alisema, sasa jamii ya Wawi na vijiji jirani, imeanza kufahamu lengo lao, na wapo wanaothamini jitihada zao.
“Wengine wanainyemelea na kutaka kuikata, lakini ni wachache na hadi sasa hakuna uharibifu wa kasi unaotuathiri’’,alifafanua Katibu huyo.
Hata hivyo alisema wameshatoa tamko, iwapo watamkamata mtu akifanya uharibifu kwenye shamba lao hilo, wameazimia apande miti 100 katika eneo ambalo wao hawajalimalizia.
Nae mwanachama wa ‘MEO’ Ali Khamis Omar alisema kazi kubwa ilipita hadi kufanikiwa kuwa na idadi kubwa ya miti katika eneo hilo, ambalo lilikuwa jangwa.
“Kazi kubwa tuliifanya kwenye eneo hili hadi kufanikiwa kuwa na shamba lenye miti mchanganyiko, na tayari wengine wanataka na wao waingizwe’’,alifafanua.

Kikundi cha upandaji miti na uhifadhi wa mazingira ‘MEO’ cha Mchekeni Wawi wilaya ya Chake chake Pemba, ambacho kimeanzishwa mwishoni mwa mwaka 2010, kinawanachama 19  wakiwa wanawake wakiwa sita, na wanalima pia kilimo cha alizeti.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.