Habari za Punde

Polisi: Marufuku magari ya mizigo kubeba wafuasi kwenye Kampeni

NA HAJI NASSOR, PEMBA
VYAMA vya siasa kisiwani Pemba, vimeonywa mara moja kuacha tabia ya kutumia gari za mizigo kwa kuwasafirisha wafuasi wao, na chama kitakachokiuka amri hiyo, kitachukuliwa hatua za kisheria.
Kamanda wa Polisi mkoa wa kusini Pemba Juma Yussuf Ali, alitoa karipio hilo mbele ya wanadishi wa habari afisini kwake Madungu Chake chake Pemba juu ya kuanza kwa kampeni.
Alisema kumekuwa na kawaida, kwa vyama vya siasa wakati wote wa kampeni, kutumia magari yaliosajiliwa kwa kubeba mizigo na huwaingiza wafusi wao.
Alieleza kuwa, kufanya hivyo ni kosa, na sasa Jeshi la Polisi limeahidi kula sahani moja na chama chochote kitakachokwenda kinyume na agizo hilo.
Kamanda Yussuf alisema, katika Jeshi la Polisi katika kutekeleza hilo, halitokionea haya chama chochote, ambacho kitakwenda kinyume na kuvunja sheria ya usalama barabarani.
Alieleza kuwa, kumekuwa na mtindo mbaya kwa vyama vya siasa wakati wote wa mikutano ya kampeni, kutumia gari za mizigo au vikeri jambo ambalo sio sahihi.

“Tunasema Jeshi la Polisi, hatutokivumilia chama chochote kitakachotumia gari zisizorasmi kubebea wafuasi wao, na badala yake watumie gari za abiria’’, alifafanua.
Hata hivyo, alisema pia Jeshi la Polisi litakuwa makini kuhakikisha gari za abiria kama vile haisi au basi hayajazi kupita kiasi, badala yake wanachukua abiria kwa muijibu wa usajili wa gari.
Katika hatua nyengine, Kamanda huyo w aPolisi mkoa wa kusini Pemba, amewataka wagombea kuhakikisha wanatumia lugha nzuri na kunadi sera zao na sio maneno ya kashfa.
“Kila chama kinasera zake, sasa sisi hatupendelei kuona mgombea ameacha sera za chama chake na kutoa lugha za matusi na kejeli’’, alisema Kamanda.
Aidha, amewageukia waandishi wa habari kuzitumia vyema kalamu zao na kuacha ushabiki na badala yake wazingatie maadili na sheria zinazowaongoza.
Akizungumza na mwandishi wa habari kwa njia ya simu Mgombea urais wa chama cha TADEA Juma Ali Khatib, alisema suala la kubeba wafuwasi wao kwenye gari za wazi sio salama sana.
“Kama Jeshi la Polisi limepiga marufu, ni vyema sisi viongozi wa vyama kuyakataa magari hayo, maana huwa yanajaza pomoni na kusababisha ajali zinazoweza kuepukika’’,alisema.
Hata hivyo amevishauri vyama vyengine kutii agizo hilo bila ya shuruti kwa vile limezingatia usalama wa wapiga kura wao.

Kampeni kwa ajili ya uchaguzu mkuu wa vyama vingi nchini zimeanza tokea Agosti 22 na zikitarajiwa kufungwa saa 12:00 jioni siku moja kabla ya uchaguzi mkuu mwezi Oktoba mwaka huu.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.