Habari za Punde

WAHENGA walisema….. ‘mgeni awiya mwenyeji apone’

Na Mwandishi wetu, PEMBA
Huu ni usemi maarufu, ambao tumekuwa tukiusikia kila uchao kwa kisiwa cha Zanzibar (Unguja na Pemba).
Usemi huu, kwa kawaida umekuwa ukisikika mara tu baada ya kuzuka jambo ambalo lina maslahi, wakati hapo awali halikuwepo.
Kwa madhumuni hayo, makala haya ikaona ipo haja ya kufuatilia kwanini wananchi wa shehia ya Jombwe wilaya ya Mkoani Pemba, watamke mara kwa mara usemi huo.
Ahaaaaa…… ‘kumbe usilolijua ni sawa na usiku wa kiza’ walisema wahenga hapo zamani za kale.
Kumbe sababu pekee ya kuwa wimbo usemi huo kwa wananchi wa Jombwe, ni mara tu baada ya kukamilika kwa mradi wa maji safi na salama katika shehia hiyo.
Tukiangazia katika historia, Shehia ya Jombwe ni moja kati ya shehia zilizomo ndani ya wilaya ya Mkoani, waliokuwa wakikabiliwa na usumbufu mkubwa wa huduma ya maji safi na salama kwa muda mrefu.
Kutokana na hali hiyo, wananchi hao waliamua kuibua mradi wa maji safi na salama, ambao utaweza kuwasaidia kuondokana na kadhia hiyo.
Mradi wa maji wa Jombwe, uliibuliwa na wananchi mapema Machi 19 mwaka jana, kutokana na usumbufu mkubwa wa ukosefu wa maji waliokuwanao wananchi hao.
Bila shaka katika kufanikisha hilo, ushirikiano wa watu mbali mbali ulionekana ndio maana maji safi na salama katika shehia hiyo, limekuwa kama karafuu Pemba.

Akisoma risala mmoja ya wananchi wa shehia hiyo, katika uzinduzi wa mradi huo Agosti 18 mwaka huu, Mussa Juma alitoa ufafanuzi wa kina juu ya michango iliyotolewa katika kufanikisha suala hilo.
Ama kweliiiii……….. aliyemo hatoki na asiyekuwemo haingi …alidakia msoma risala kwa kutaka kuitaja Mamlaka ya Maji Zanzibar ‘ZAWA’ tawi la Pemba kwamba ilichangia shilingi milioni 1,500,000 katika hilo.
‘’Sisi wananchi wenyewe kwa hiari yetu, tulichangia uchimbaji wote wa kisima kiasi cha fedha taslimu shilingi milioni 14,200,000’’, aliweka wazi hilo.
Kama ilivyo ada kwa viongozi wetu wa majimbo kuchangia katika miradi ya mbali mbali ya wananchi, ambapo Mbunge wa Jimbo la Kiwani alichangia shilingi milioni 4,750,000.
Mwakilishi wa Jimbo hilo bila ya kuwa nyuma naye alichangia shilingi milioni 5,400,000, ili kuhakikisha mradi huo unakamilika kwa wakati na lengo linafikiwa.
‘’ Mbunge wa Jimbo la Wawi wakati huo akiwa CUF na sasa mgombea urais wa ADC Hamad Rashid Mohamed, amesaidia shilingi milioni 1,500,000 pamoja na tenki moja la lita 5000, lenye thamani ya shilingi 1,700,000’’, alieleza Mussa.
Uchimbaji huo wa kisima katika mradi huo, uliambatana na ujenzi wa mnara na vifaa vyake uligharimu shilingi milioni 29,600,000 bila kupunguwa.
Bila ya kuisahau Taasisi ya ‘THE LADY FATEMAH CHARITABLE TRUST’ ambapo imechangia mipira ya kusambazia maji, mifereji na gharama za mafundi.
 Afisa mdhamini Wizara ya Ardhi, Makaazi, Maji na Nishati kisiwani Pemba Hemed Suleiman Abdallah katika uzinduzi wa mradi huo, alisema mafanikio makubwa yaliyopatikana kupitia mradi ni uwekaji wa mifereji 89 katika shehia.
‘’ Alivitaja vijiji vilivyopitiwa na mabomba hayo kuwa ni Jombwe 24, Misikiti ya Jombwe nane, kwa sanani 24, Misikiti ya kwa sanani matano, Chanjaani 22, Misikiti ya Chanjaani matatu, Jombwe mvumoni nane  na Chuo cha Qurani moja’’, alifafanua Mdhamini.
Afisa mdhamini hakusita kusema, Mamlaka ya maji ZAWA itaendelea kushirikiana na wananchi wa Jombwe katika kuulea mradi huo, ili isije kukatokea uharibifu wa aina yoyote.
Wananchi walipo hoji kuhusu ada ya kulipia umeme katika kisima hicho, Mamlaka ya Maji ZAWA imewatoa hofu kwamba, itabeba gharama za umeme, ili kuhakikisha huduma hiyo inapatikana masaa 24.
 Mdhamini alieleza gharama ya shilingi 750,000 kwa mwezi ambayo ni ununuzi wa umeme wa ujazo wa uniti 2700 kwamba, wananchi hao hawatokuwa na uwezo huo, ndio maana wizara imeamua kubeba jukumu hilo.
 “Kwa kisima hichi kutokana na umuhimu wake mkubwa kwa wananchi, Wizara kupitia ZAWA, tumeamua kulibebea suala la gharama za umeme kila mwezi’’, alifafanua.
Mgeni rasmi katika uzinduzi wa mradi huo Makamu wa pili wa rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idd, aliipongeza ZAWA kutokna na juhudi zake za kushirikiana na wananchi, katika kuwapatia huduma hiyo.
Balozi Seif alisema, nia na lengo la Serikali ni kuona wananchi wake wananeemeka na huduma hiyo kila kijiji na ndio maana kumekuwa na juhudi za makusudi zinazochukuliwa na taasisi zake.
Alisema, Serikali kupitia ZAWA imeweza kushirikiana na wananchi vyema na kuamua kulibeba suala la gharama za umeme kwa wananchi lililobakia kwao ni kuuenzi mradi huo.
“Wananchi mnajukumu na wajibu mkubwa wa kukienzi kisima hichi cha maji safi na salama, ili mtumie nyie mliopo sasa na hata kizazi kijacho, maana hakuna asiefahamu umuhimu wa maji safi na salama’’, alifafanua.
Mkuu wa mkoa wa Kusini Pemba Bi. Mwanajuma Majid akizungumza katika hafla hiyo alisema ushiriki wa wananchi katika mambo ya kuleta maendeleo ni jambo la msingi.
Aliwapongeza wananchi wa shehia ya Jombwe kwa kujitolea kwa hali na mali, ili kuhakikisha mradi huo unafikia ukomo sambamba na lengo husika.
‘’Pongezi za hali ya juu nazileta kwenu wananchi wa shehia ya Jombwe maana naamini mumeonesha mfano mkubwa wa kuigwa na shehia nyengine katika mkoa huu’’, alieleza bi Mwanajuma.
 Wahenga walisema ‘’mgeni na mwenyeji ndio mambo yakawa’’.
Makala haya yalifika mbali zaidi na kukutana na Sheha wa shehia ya Jombwe Hakim Khamis Omar ambapo alisema, ushirikiano ndio kitu pekee, kilichofanikisha kukamilika kwa mradi huo.
Sheha hakusita kusema, muda umefika sasa kwa wananchi kushikamana na kuwa kitu kimoja kwa lengo la kuleta maendeleo katika shehia zao.
‘’Hata dini yetu ya kislamu, imesisitiza sana suala la umoja na mshikamano hivyo ni vyema tukalitekeleza hili, kwa maslahi ya hapa duniani na kesho tunakokwenda’’, alieleza Sheha.
Mmoja kati ya wananchi hao Maryam Juma Ali alisema, awali wakipata maji kutoka kisima cha Kengeja ambako yalikuwa yakisuasua, lakini sasa maji kwao kama karafuu Pemba.
Hakuacha kukumbushia walikotoka kwamba, awali wakipata maji saa 8:00 usiku na alfajiri hufungwa bila ya kujali nani kapata na nani kakosa.
‘’Tukikosa hapo tulikuwa tunatumia maji ya visima ambapo wakati wa kiangazi vengine vinakauka na kuendelea kuhangaika’’, aliipasha makala.
Kisima hicho, ambacho kimechimbwa kupitia mradi huo wa Shehia ya Jombwe ambao ulioibuliwa na wananchi kinatoa maji lita 10,000 kwa saa moja.

Mradi wa maji wa wananchi wa shehia ya Jombwe wilaya ya Mkoani Pemba, ulianza mwezi Machi mwaka jana na umegharimu zaidi ya shilingi 44 milioni, ambapo asilimia 80 ni nguvu za wananchi wenyewe

1 comment:

  1. Naomba kuuliza hivi Afisa Mdhamini Wizara ya Ardhi Makaazi Maji na Nishati ni ndugu Hemed Suleiman Abdalla au Ndugu Hemed Salim Hemed. Nauliza hivi kwa sababu kwa sababu hii ni Mara ya piling ktk mtandao huu Afisa mdhamini wizara hi I huandikwa Hemed Suleiman waksti ninavyojua Mimi ni Hemed Salim Hemed. Au kuna mabadiliko? Naomba kueleweshwa.

    ReplyDelete

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.