Na WMJJWM- Dar Es Salaam
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima amesema Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan imefanikiwa kutekeleza mipango na mikakati mbalimbali katika kutoa haki kwa watoto nchini.
Ameyasema hayo Juni 17, 2025 mkoani Dar Es Salaam katika Maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika iliyofanyika katika viwanja vya Chuo cha Ustawi wa Jamii Kijitonyama.
Waziri Dkt. Gwajima amesema katika kipindi cha miaka minne ya Uongozi wa Rais Samia imetekeleza mipango na mikakati mbalimbali katika kuhakikisha haki za Mtoto zinazingatiwa na kutolewa kwako.
"Kipekee nachukua fursa hii kumshukuru sana Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa uongozi wake mahiri na dhamira yake ya dhati katika kuimarisha mifumo na mazingira ya utoaji wa haki kwa watoto nchini.
“Tumeshuhudia maboresho makubwa katika miundombinu na huduma za afya, lishe, elimu, maji, umeme na ustawi wa ujumla wa jamii wakiwemo watoto." amesema Waziri Dkt. Gwajima
Ameongezea kuwa Kaulimbiu ya Maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika kwa mwaka 2025 ni "Haki za Mtoto: Tulipotoka, Tulipo na Tuendako”. Kaulimbiu ambayo inahitaji kutafakari upatikanaji wa haki za watoto tangu zilipoainishwa na Sera ya Maendeleo ya Mtoto mwaka 2008.
Wakieleza kwa kifupi mafaniko hayo ya utekelezaji wa Haki za Mtoto nchini baadhi ya watoto wa Baraza la Watoto wamesema Serikali imejenga mbiundombinu ya kutolea huduma za afya ya mama na mtoto kote nchini ambapo jumla ya Hospitali za kanda 6, Hospitali za Rufaa 28, Hospitali za Wilaya 129, Vituo vya Afya 345 na Zahanati 1,158 huduma ambazo zipo katika haki ya Mtoto kuishi.
Wameongeza kuwa katika kutekeleza haki ya kuendelezwa ya mtoto, Serikali imeimarisha miundombinu ya shule za msingi na sekondari ili kuongeza wigo wa idadi ya watoto wanaopata elimu nchini.
Kwa mujibu wa Taarifa ya Ofisi ya Rais – TAMISEMI, idadi ya shule za msingi zimeongezeka kutoka shule 16,406 mwaka 2021 hadi kufikia shule 17,986 kwa mwaka 2024/2025.
Wamesema Serikali imefanya jitihada kubwa za kumlinda mtoto dhidi ya vitendo vya ukatili nchini kwa kufanya marekebisho ya baadhi ya Sheria za kumlinda mtoto ikiwemo Sheria ya Mtoto Sura ya 13, Sheria ya Makosa ya Mtandao Sura ya 443 na Sheria ya Msaada wa Kisheria Sura ya 23 kwa kuingiza masharti yatakayoimarisha ulinzi na usalama wa mtoto.
Aidha, wameeleza Maadhimisho hayo yanalenga kuwaelimisha na kuwakumbusha wazazi au walezi na watoa huduma wote wajibu wao katika kutekeleza haki tano za msingi za mtoto ambazo ni haki ya kuishi kwa mtoto bila kukatisha uhai wake, haki ya kuendelezwa kielimu, kiutamaduni na vipaji vya mtoto, haki ya kulindwa dhidi ya ukatili wa aina yoyote, haki ya kushiriki kutoa maoni katika masuala yanayomuhusu mtoto kulingana na umri wake na haki ya kutobaguliwa kwa mtoto kutokana na hali yake.
Pia Watoto hao wamewaasa Wazazi au Walezi na Wadau wengine wa Watoto ikiwa pamoja na viongozi wa dini kusimamia malezi ya Watoto katika jamii kwa kuwapata mahitaji yao ya msingi ili kuwaepusha na vishawishi kutoka kwa watu wasio na nia njema na usalama wa mtoto liwe ni jukumu la kipaumbele kwa wazazi.
Kwa upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. John Jingu amesema Serikali inaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali katika kutoa elimu kwa wazazi walezi na watoto hasa katika upatikanaji wa haki za Mtoto na kupambana na vitendo vya Ukatili dhidi yao.
Mwakilishi Mkazi wa Shirika la UNICEF Elke Wisch amesema Shirika hilo litaendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika kuweka mazingira mazuri katika utoaji wa haki za Mtoto na kupambana na vitendo vya Ukatili dhidi ya Watoto katika kutekeleza mipango na mikakati mbalimbali ya Serikali.
Naye Mwenyekiti wa Baraza la Watoto la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Daniel Maghembe amesema wanatambua jitihada za Serikali katika kupambana na vitendo vya Ukatili dhidi ya Watoto na wakiomba kuendelea kuongeza nguvu zaidi katika kuwalinda Mtoto.
"Tunamshukuru Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuweka mazingira mazuri ya utekelezaji wa Haki za Mtoto Tanzania kwa kuweka Mikakati madhubuti ya upatikanaji wa haki hizo" amesisitiza Daniel.
No comments:
Post a Comment