Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na
Mazingira) Mhe. Khamis Hamza Khamis (katikati) akipanda mti aina ya mwembe
katika Kituo cha Afya cha Kambarage Manispaa ya Shinyanga ikiwa ni sehemu ya Maadhimisho ya Siku ya Umoja wa Mataifa Ya
Kupambana na Kuenea kwa Hali ya Jangwa na Ukame Duniani leo tarehe 17 Juni,
2025. Kushoto ni Naibu Katibu Mkuu (Muungano) Ofisi ya Makamu wa Rais Bw.
Abdallah Hassan Mitawi na Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Mazingira Dkt. Paul
Deogratius.
Washiriki wakiwa katika Maadhimisho ya Siku ya Umoja wa Mataifa Ya Kupambana na Kuenea kwa Hali
ya Jangwa na Ukame Duniani yaliyofanyika leo tarehe 17 Juni, 2025 katika
Manispaa ya Shinyanga.
Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Khamis Hamza Khamis akihutubia wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Umoja wa Mataifa Ya Kupambana na Kuenea kwa Hali ya Jangwa na Ukame Duniani yaliyofanyika leo tarehe 17 Juni, 2025 katika Manispaa ya Shinyanga.
Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Khamis Hamza Khamis ametoa rai kwa wadau wa mazingira katika ngazi zote na wananchi kwa ujumla kuungana na Serikali kwa hali na mali katika mampambano dhidi ya kuenea kwa hali ya jangwa na ukame kwa faida ya vizazi vilivyopo na vijavyo.
Pia, amewaomba wananchi kuendelea kupanda miti na
kuitunza ili kukabiliana na athari za ukame ambao unaathiri sekta mbalimbali
ikiwemo maji, mifugo na kilimo ambazo zina umuhimu mkubwa kwa binadamu.
Ametoa wito huo wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Umoja wa Mataifa ya
Kupambana na Kuenea kwa Hali ya Jangwa na Ukame Duniani yaliyofanyika kitaifa
leo tarehe 17 Juni, 2025 katika Manispaa ya Shinyanga.
Akizungumza na viongozi na wananchi, Mhe. Khamis amesema pamoja
na mambo mbalimbali Tanzania pamoja na jumuia za kimataifa kwa kushirikisha
vizazi vilivyopo na vijavyo, imejitolea kuongoa hekta bilioni moja ya ardhi
iliyoharibika kufikia mwaka 2030.
Alisema Tanzania ni
moja ya waathirika wa hali ya ukame hivyo Serikali imechukua hatua mbalimbali
kuhakikisha inakabiliana na tatizo hilo kwa ufanisi mkubwa kwa kushirikisha wizara
za kisekta, taasisi za umma, washiriki wa maendeleo, mashirika yasiyo ya kiserikali,
sekta binafsi na taasisi za kidini.
Halikadhalika, Naibu Waziri
Khamis alibainisha kuwa Serikali imeandaa Mpango wa Kitaifa wa Kupambana na
Kuenea kwa Hali ya Jangwa na Ukame, imefanya mapitio ya Sera ya Taifa ya
Mazingira.
Kwa upande
mwingine alisema Serikali imeendelea kuhakikisha kuwepo kwa ufugaji wenye tija pasipo
kuharibu mazingira kwani ufugaji usiokuwa endelevu huchangia kuenea kwa hali ya
jangwa na ukame.
Akizungumzia siku hiyo
alisema ina madhumuni ya kukuza uelewa miongoni mwa jamii juu ya Mkataba wa
Umoja wa Mataifa wa Kupambana na Kuenea kwa Hali ya Jangwa na Ukame na umuhimu
wa utekelezaji wake duniani kote, hususan katika nchi zilizoathirika zaidi hasa
Afrika.
Kwa upande wake Mkuu wa
Wilaya ya Shinyanga Mhe. Julius Mtatiro aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa, aliishukuru
Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kuona umuhimu wa kuadhimisha siku
hii mkoani humo.
Alisema kutokana na
mkoa huo kukabiliwa na hali ya ukame hivyo ni jambo jema kuitumia siku hiyo
kuhamasisha upandaji wa miti kuepuka changamoto ya kugeuka kuwa jangwa.
Mhe. Mtatiro alitumia
nafasi hiyo kuishukuru Serikali chini ya Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa
kutekeleza mkradi mbalimbali ya maendeleo kwa wananchi ambayo si tu inasaidia
katika utunzaji wa mazingira bali pia inachagiza uchumi.
Aliongeza kuwa mradi wa
maji ya Ziwa Victoria kutoka mkoani Mwanza ni chachu ya zoezi la upandaji wa
miti kwani unasaidia pamoja na matumizi mbalimbali lakini pia kuyatumia
kumwagilia miti.
Maadhimisho haya
yalikwenda sanjari na zoezi la upandaji wa miti katika Kituo cha Afya cha
Kambarage kilichopo Manispaa ya Shinyanga na maadhimisho ya mwaka 2025
yanachagizwa na kaulimbiu ‘Ongoa
Ardhi Kufungua Fursa’.
No comments:
Post a Comment